Hamia kwenye habari

DESEMBA 29, 2017
BOLIVIA

Mashahidi wa Yehova Wapewa Tuzo kwa Kuwa na Maonyesho ya Utamaduni wa Asili Katika Kusanyiko la Eneo Nchini Bolivia

Mashahidi wa Yehova Wapewa Tuzo kwa Kuwa na Maonyesho ya Utamaduni wa Asili Katika Kusanyiko la Eneo Nchini Bolivia

SANTA CRUZ, Bolivia—Kuanzia Oktoba 27-29, 2017, karibu watu 17,000 kutoka nchi 20, walihudhuria kusanyiko la eneo lililofanywa na Mashahidi wa Yehova huko Cochabamba, Bolivia. Kwa kuwa mashirika mawili nchini Bolivia yalipendezwa sana na tukio hilo, yaliwapatia Mashahidi tuzo kwa marekebisho makubwa waliyofanya katika eneo la kusanyiko na kwa maonyesho waliyoandaa yaliyoonyesha utamaduni uliogawanyika wa nchi ya Bolivia.

Mashahidi wa Yehova wamekuwa wakifanya kusanyiko lao la kila mwaka katika uwanja wa Fundación para la Feria Internacional de Cochabamba (FEICOBOL) tangu mwaka 2012. Siku chache kabla ya kusanyiko kuanza, Mashahidi husafisha uwanja huo. Lakini ili kuandaa uwanja huo kwa ajili ya maelfu ya watu ambao wangehudhuria mwaka huu, Mashahidi karibu 4,900 walijitolea kurekebisha sehemu ya ndani na nje ya jengo hilo kwa muda wa siku 15. Kazi walizofanya zilitia ndani kupaka rangi, kutengeneza mfumo wa maji, pamoja na kuweka mifumo ya video na sauti. Vilevile walifanya kazi za nje kama vile kutengeneza bustani, na kurekebisha viti vya kukalia nje pamoja na taa za barabarani.

Mashahidi wakipewa tuzo kutoka kwa FEICOBOL.

Mashahidi walio katika eneo hilo waliandaa pia sehemu ya makumbusho yaliyoonyesha utamaduni wa asili wa Bolivia ili kuwaelimisha wahudhuriaji zaidi ya 1,800 wa kimataifa walioalikwa. Makumbusho hayo yalitia ndani maonyesho ya mazao ya kilimo pamoja na michoro mbalimbali. Pia, makumbusho hayo yalitia ndani aina tatu za nyumba za mfano zinazopatikana nchini Bolivia peke yake. Mashahidi walitoa nyumba hizo kama mchango kwa uwanja wa FEICOBOL.

Tuzo kutoka kwa Idara ya Baraza la Utamaduni wa Cochabamba.

Aldo Vacaflores, rais wa baraza la wakurugenzi la FEICOBOL, ambaye aliwapatia Mashahidi tuzo hiyo kwa sababu ya kazi yao, alisema hivi: “Tumevutiwa sana na jinsi washiriki wa kanisa lenu walivyo tayari kujitoa. Mmeonyesha shauku nyingi na mmefanya kazi kwa moyo wote ili kufanya kusanyiko hili livutie kwa wati wote waliokuja. Kazi iliyofanywa katika kusanyiko hili ni mfano wa kuiga.”

Wakiwa wamevutiwa sana na maonyesho ya makumbusha hayo, Idara ya Baraza la Utamaduni wa Cochabamba, ambayo ni ofisi ya serikali ya mkoa wa Cochabamba, iliwapa Mashahidi tuzo. Sdenka Fuentes, rais wa baraza hilo, aliwashukuru Mashahidi kibinafsi kwa kuchagua mji wa Cochabamba kuwa eneo ambalo kusanyiko hilo lingefanyika, na kusema kwamba makumbusho hayo yamekuwa ya kipekee katika kuonyesha utamaduni mpana wa Bolivia.

Makumbusho ambayo Mashahidi walitengeneza ilitia ndani maonyesho ya utamaduni wa asili wa Bolivia.

Garth Goodman, msemaji wa Mashahidi wa Yehova nchini Bolivia, anasema hivi: “Kusanyiko hili limekuwa nafasi nzuri sana kwa jumla ya watu 49,320 kuabudu pamoja, ikitia ndani miji mingine sita iliyounganishwa na programu hii. Tunafurahi kwamba jamii ya Cochabamba imethamini namna tulivyoonyesha heshima kwa nchi ya Bolivia na utamaduni wake wa asili na wa kipekee.”

Mashahidi wa Yehova wamekuwa wakitoa elimu ya Biblia nchini Bolivia tangu mwaka 1924. Mwanzoni mwa mwaka 2017, walifikia miradi miwili mikubwa kwa kutoa tafsiri ya Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo (“Agano Jipya”) katika lugha za Kwechua na Aymara.

Wanahabari wanaweza kuwasiliana na:

Kimataifa: David A. Semonian, Ofisi ya Habari za Umma,+1-845-524-3000

Bolivia: Garth Goodman, +591-3-342-3442