Hamia kwenye habari

URUSI

Wamefungwa kwa Sababu ya Imani Yao​—Urusi

Wamefungwa kwa Sababu ya Imani Yao​—Urusi

Historia ya Mashahidi wa Yehova nchini Urusi imejaa ukandamizaji na mateso. Kwa muda mrefu katika karne ya 20, wenye mamlaka nchini Urusi waliwatendea Mashahidi isivyo haki, hata ingawa walijulikana kuwa watu wanaopenda amani, na raia wanaotii sheria. Serikali ya Muungano wa Sovieti ilikusudia kuwalazimisha Mashahidi wawe wafuasi wa itikadi za Kisovieti. Hawakuruhusiwa kuwa na Biblia au machapisho ya kidini. Kwa kuwa walikuwa wakifuatiliwa sana walilazimika kufanya mikutano kwa siri. Ikiwa wangegunduliwa, basi wangepigwa sana au kuhukumiwa vifungo vya muda mrefu gerezani. Serikali hiyo iliwapeleka maelfu ya Mashahidi uhamishoni huko Siberia.

Hali hiyo ilianza kubadilika mwaka wa 1991 wakati serikali ya Urusi ilipowasajili kisheria Mashahidi wa Yehova na kuwaruhusu kuabudu kwa uhuru bila kuingiliwa na serikali. Hata hivyo, kipindi hicho cha amani hakikudumu kwa muda mrefu.

Mwaka wa 2009, upinzani ulianza tena wakati Mahakama ya Juu ya Urusi ilikubali uamuzi wa mahakama ya chini iliyodai kwamba kutaniko fulani la Mashahidi wa Yehova ni lenye “msimamo mkali.” Baada ya kesi zilizodumu kwa miaka kadhaa, Aprili 2017, Mahakama ya Juu nchini Urusi ilipiga marufuku mashirika ya kisheria ya Mashahidi wa Yehova kwa tuhuma za kuwa na msimamo mkali. Muda mfupi baada ya hapo wenye mamlaka nchini Urusi walitaifisha mali za Mashahidi, wakafunga maeneo yao ya ibada, na wakatangaza kwamba machapisho yao yanawachochea watu kuwa na “msimamo mkali.”

Baada ya kupiga marufuku mashirika ya kisheria ya Mashahidi wa Yehova wenye mamlaka walianza kuwashambulia Mashahidi mmoja-mmoja. Kwa kweli, wanavuka mipaka kwa kuhusianisha ibada ya Shahidi mmoja-mmoja na shirika lililopigwa marufuku. Polisi wanapovamia nyumba za Mashahidi, wanawahoji kwa ukali na kuwaonea. Mashahidi wa umri mbalimbali wa kike na wa kiume wamekamatwa, na wakahukumiwa kwenda gerezani au kupewa vifungo vya nyumbani.

Tangu marufuku ilipotangazwa Aprili 2017, mamia ya Mashahidi wamepelekwa kizuizini au kufungwa gerezani kwa kutuhumiwa kwamba wana msimamo mkali. Kufikia Julai 18, 2024, jumla ya Mashahidi 137 wako gerezani.

Malalamiko Kuhusu Jinsi Urusi Inavyowatesa Mashahidi wa Yehova

Mamlaka nchini Urusi zinaendelea kuwahukumu Mashahidi kwa madai kwamba wanashiriki utendaji wenye msimamo mkali licha ya malalamiko kutoka kwenye mashirika ya kimataifa yanayosihi Urusi iache kuwatesa Mashahidi. Wachunguzi mbalimbali na mahakama zilizo nje ya Urusi wameikaripia serikali ya nchi hiyo kwa kukataa kusikiliza maombi wanayopokea na kuendelea kuwatesa Mashahidi wa Yehova.

Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu: Juni 7, 2022, Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu ilitoa hukumu muhimu dhidi ya Urusi na kuishutumu nchi hiyo kwa sababu ya kuwatesa Mashahidi wa Yehova (Taganrog LRO and Others v. Russia, nos. 32401/10 and 19 others). Mahakama hiyo ilitoa uamuzi dhidi ya Urusi kwa sababu ya kutenda kinyume na sheria na kuwapiga marufuku Mashahidi wa Yehova mwaka wa 2017. Urusi iliamuriwa “kufanya yote inayoweza ili kufuta kesi zote zinazoendelea za Mashahidi wa Yehova . . . na kuwaachilia . . . Mashahidi wa Yehova [walio gerezani].” Kwa kuongezea, Urusi iliamuriwa irudishe mali zote ilizotaifisha au ilipe zaidi ya dola milioni 60 kama fidia, na pia iwalipe wale waliopeleka malalamiko yao zaidi ya dola milioni 3 kama fidia.

Barua Kutoka kwa Katibu Mkuu wa Baraza la Ulaya: Barua ya Desemba 9, 2022, iliyotumwa kwa Waziri wa Urusi wa Mambo ya Nje, Marija Pejčinović Burić ilisema: “Katika kesi ya Jehovah’s Witnesses of Moscow and Others na kesi ya Krupko and Others, zinazohusu kupigwa marufuku kwa shirika la Mashahidi kutia ndani utendaji wao, kuvurugwa kwa mkutano wenye amani wa kidini na kufungwa gerezani kwa baadhi ya waabudu, Kamati yetu iliwasihi wenye mamlaka kuondoa marufuku dhidi ya utendaji wa mashirika yote ya Mashahidi wa Yehova na kusitisha kesi zote za uhalifu zinazoendelea dhidi yao.”

Uamuzi wa Halmashauri ya Mawaziri wa Baraza la Ulaya: Katika mkutano waliofanya Septemba 2023, Halmashauri ya Mawaziri wa Baraza la Ulaya [CoM] iliandika “jambo hili ni lenye kuhangaisha kwa sababu [Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu] ilikuwa wazi kwa kutaja Kifungu cha 46 cha Mkataba na uamuzi uliotolewa katika kesi ya Taganrog LRO and Others lakini wenye mamlaka nchini Urusi wameipuuza kimakusudi kabisa, tukizungumzia kihususa . . . amri ya kuwaachilia huru Mashahidi wa Yehova waliofungwa.” Kwa sababu hiyo, CoM “imeamua kuwasilisha kesi hizi kwenye Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Kibinadamu, Kamati ya Vifungo Visivyo vya Haki ya Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa na pia kwenye mashirika mengine ya kimataifa yanayoweza kushughulikia tatizo la kuwatesa Mashahidi wa Yehova katika Shirikisho la Urusi. CoM ikiwa na kusudi la kuhakikisha kwamba wanatenda kupatana na maamuzi yaliyotolewa.”

Mifano ya Hukumu Kali Iliyotolewa Hivi Karibuni

  • Januari 25, 2024, Sona Olopova ni mwanamke aliyeolewa mwenye umri wa miaka 37, amehukumiwa adhabu ya miaka miwili ya kazi ya kulazimishwa katika kambi ya kurekebisha tabia katika Eneo la Samara. Maofisa wa usalama walikuwa wamefanya msako kwenye nyumba yake mnamo Mei 2023. Baada ya hapo, kesi ya uhalifu ilifunguliwa dhidi yake, naye alishtakiwa kuhusika katika utendaji wenye msimamo mkali. Kwa kweli, “uhalifu” anaodaiwa kuwa alifanya ni kumwabudu Mungu kwa amani pamoja na waamini wenzake. Sona mwenyewe alisema hivi: “Mwendesha mashtaka hakuzingatia kwamba huwezi kuwa Shahidi wa Yehova na wakati uleule uwe mtu mwenye msimamo mkali.”

  • Februari 6, 2024, mahakama ya rufaa iliunga mkono uamuzi wa kumfunga Dmitriy Barmakin. Alipelekwa kizuizini moja kwa moja kutoka mahakamani ili akakamilishe kifungo chake cha miaka minane. Julai 2018, maofisa wa polisi waliobeba silaha walivamia nyumba ambayo Dmitriy na mke wake, Yelena, walikuwa wakiishi. Walikuwa hapo kwa sababu walikuwa wakimtunza nyanya yake Yelena mwenye umri wa miaka 90. Dmitriy na mke wake walichukuliwa na kurudishwa jijini kwao, Vladivostok, kisha wakamweka Dmitriy kizuizini. Baada ya hapo, kesi ya uhalifu ilifunguliwa dhidi yake kwa mashtaka ya “kupanga utendaji wa shirika lenye msimamo mkali.” Kwa sasa amezuiliwa katika mahabusu katika Eneo la Khabarovsk naye ataachiliwa Novemba 2029. Pia, kesi ya Yelena iko mahakamani kwa sababu ya imani yake.

  • Februari 29, 2024, Aleksandr Chagan, mwanamume mwenye umri wa miaka 53 ambaye amefunga ndoa, alihukumiwa na Mahakama ya Wilaya ya Tsentralniy iliyo Tolyatti katika Eneo la Samara kifungo cha miaka nane gerezani. Yeye ni mmoja kati ya wanaume wachache ambao ni Mashahidi waliopewa vifungo virefu kiasi hicho gerezani nchini Urusi. Kesi yake ilipokamilishwa alipelekwa kizuizini moja kwa moja kutoka mahakamani. Hivi sasa yupo Gereza Na. 4 katika Eneo la Samara naye ataachiliwa Januari 2032.

  • Machi 5, 2024, mahakama katika Eneo la Irkutsk iliyoko mashariki mwa Siberia ilitoa uamuzi wa kwamba wanaume tisa ambao ni Mashahidi ni wenye msimamo mkali. Mwanamume mwenye umri mkubwa zaidi kati yao ana umri wa miaka 72. Wote tisa walihukumiwa vifungo vyenye urefu tofauti, kirefu zaidi kikiwa miaka saba. Kesi zao zilianza Oktoba 2021 baada ya nyumba zao kufanyiwa msako na maofisa wa polisi. Kufikia siku ya hukumu, mmoja wa wanaume hao, Yaroslav Kalin, alikuwa kizuizini kwa zaidi ya miaka miwili. Anasema maisha ya gerezani yalikuwa magumu sana, “katika jela mbaya zaidi na hali mbaya sana.”

  • Aprili 2024, Rinat Kiramov, ambaye anatumikia kifungo cha miaka saba, alihamishwa na wasimamizi wa gereza na kupelekwa kwenye gereza linalotoa huduma za afya eti kwa msingi wa kwamba alishukiwa kuwa na kifua kikuu. Novemba 2021 kesi ya uhalifu ilifunguliwa dhidi ya Rinat aliyekuwa na umri wa miaka, naye alishtakiwa kwa kujihusisha katika utendaji wenye msimamo mkali. Baada ya kukaa mahabusu kwa mwaka mmoja na nusu, alihukumiwa kifungo cha miaka saba gerezani. Rinat alipohamishiwa kwenye gereza hilo la huduma za afya, kikundi cha wafungwa kilimtendea vibaya kimwili, hata walimtesa kwa kumpiga kwa umeme. Mbali na hilo, alizuiwa asilale wala asile kwa siku nne. Mei 17, 2024 Rinat alirudishwa kwenye gereza la kawaida baada ya uchunguzi wa daktari kuonyesha kwamba hakuwa na kifua kikuu. Inatarajiwa ataachiliwa kutoka gerezani mnamo Desemba 2027.

  • Juni 20, 2024, wanaume watatu Mashahidi wanaoishi katika eneo la Khabarovsk walihukumiwa kifungo kirefu zaidi cha gerezani kuwahi kutolewa na mahakama yoyote ya Urusi dhidi ya Shahidi tangu mashirika ya kisheria ya Mashahidi wa Yehova yalipofungwa nchini humo. Nikolay Polevodov alihukumiwa kifungo cha miaka nane na miezi sita, Vitaliy Zhuk alihukumiwa kifungo cha miaka nane na miezi minne, na Stanislav Kim alihukumiwa kifungo cha miaka nane na miezi miwili. Wanaume hao walishtakiwa kuwa na hatia ya kupanga utendaji wa shirika lenye msimamo mkali. Hata hivyo, ukweli ni kwamba walikuwa wamekutana kwa amani pamoja na familia na waamini wenzao ili kujifunza Biblia.

Jitihada Zinazoendelea za Kukomesha Vifungo vya Gereza Visivyo vya Haki

Mashahidi wa Yehova ulimwenguni pote wanahuzunika sana kwa sababu waabudu wenzao wanateswa nchini Urusi. Mamilioni ya Mashahidi ulimwenguni pote wametuma barua kwa maofisa wa serikali nchini Urusi, kuwaomba waache kuwatesa Mashahidi. Mawakili wa Mashahidi wamekata rufaa kwenye ngazi zote za mahakama za Urusi na wametuma kesi nyingi kwenye Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu. Mashahidi wa Yehova pia wametuma malalamiko yao kwa Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Kibinadamu na Kikundi cha Umoja wa Mataifa Kinachoshughulikia Vifungo Vilivyo Kinyume cha Sheria na wamepeleka ripoti mbalimbali kwenye mashirika ya kimataifa yanayofuatilia ukiukaji wa haki za kibinadamu. Mashahidi wa Yehova wataendelea kufanya yote wanayoweza ili kuwafahamisha wengine kuhusu mateso wanayopata waamini wenzao nchini Urusi ili mateso hayo yakomeshwe.

Mfuatano wa Matukio

  1. Julai 18, 2024

    Jumla ya Mashahidi 137 wako gerezani.

  2. Oktoba 24, 2023

    Kamati ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (CCPR) ilitoa Maoni yake katika kesi zinazohusu Mashirika ya Kidini ya Mashahidi wa Yehova ya Abinsk na Elista. Katika kesi zote mbili, CCPR ilifikia uamuzi wa kwamba Urusi iliwatendea Mashahidi kinyume na haki kulingana na Vifungu vya 18.1 (“haki ya kuwa na uhuru wa kufikiri, wa dhamiri, na wa kidini”) na 22.1 (“haki ya uhuru wa kushirikiana”) vya Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa. Maamuzi hayo yanathibitisha kwamba machapisho yao yote ya kidini hayachochei chuki au jeuri.

  3. Juni 7, 2022

    ECHR ilitoa hukumu muhimu inayowaunga mkono Mashahidi, Taganrog LRO and Others v. Russia, na kuishutumu Urusi kwa sababu ya kuwatesa Mashahidi wa Yehova.

  4. Januari 12, 2022

    Wizara ya Haki ya Shirikisho la Urusi inaongeza programu ya JW Library kwenye Orodha ya Serikali ya Vitabu na Habari Zinazowachochea Watu Kuwa na Msimamo Mkali wa Kidini. Hiyo ndiyo mara ya kwanza kwa programu kupigwa marufuku nchini Urusi kwa msingi wa kuwa yenye msimamo mkali.

  5. Septemba 27, 2021

    Mahakama ya jiji la Saint Petersburg yakataa rufaa dhidi ya uamuzi wa Machi 31, 2021, uliotangaza kwamba programu ya JW Library ni yenye msimamo mkali na kuipiga marufuku isitumiwe kotekote katika eneo la Shirikisho la Urusi na Crimea. Uamuzi wa awali wa mahakama utaanza kutumika mara moja.

  6. Aprili 26, 2019

    Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Vifungo Visivyo vya Haki iliona kwamba Dimtriy Mikhailov alitendewa isivyo haki na kutangaza wazi kwamba nchi ya Urusi inawatendea Mashahidi wa Yehova kikatili.

  7. Aprili 20, 2017

    Mahakama Kuu ya Shirikisho la Urusi iliamua kufunga ofisi ya Mashahidi wa Yehova na kufuta mashirika 395 ya kidini (LRO) ya Mashahidi wa Yehova.