Kuwa “Msamaria Mwema” Kunamaanisha Nini?
Jibu la Biblia
Jina “Msamaria Mwema” mara nyingi hutumiwa kumfafanua mtu anayetenda ili kuwasaidia wengine walio na uhitaji. Jina hilo linatokana na hadithi, au mfano, ambao Yesu alisimulia ili kuonyesha kwamba jirani mwema huwasaidia wengine kwa rehema bila kujali taifa au malezi ya yule mtu mwingine. a
Katika makala hii
Ni simulizi gani hilo kumhusu yule “Msamaria Mwema”?
Ufuatao ni muhtasari wa hadithi ambayo Yesu alisimulia: Mwanamume Myahudi alikuwa akisafiri kutoka Yerusalemu kwenda Yeriko. Njiani, alivamiwa na wezi, wakampiga, na kumwacha akiwa karibu kufa.
Kuhani fulani Myahudi alipita mahali ambapo msafiri huyo aliyejeruhiwa alikuwa na baadaye kiongozi wa dini ya Kiyahudi akapita hapo pia. Hata ingawa wote wawili walikuwa wa taifa lilelile na msafiri huyo, hakuna yeyote kati yao aliyesimama ili kumsaidia mwanamume huyo.
Hatimaye, mwanamume wa taifa lingine akapita. Alikuwa Msamaria. (Luka 10:33; 17:16-18) Msamaria huyo alimsikitikia na kutibu majeraha yake. Kisha akampelekea mwanamume huyo aliyejeruhiwa kwenye nyumba ya wageni. Alimtunza usiku wote. Siku iliyofuata akamlipa msimamizi wa nyumba hiyo na akasema atalipa gharama zozote za ziada zitakazotokea.—Luka 10:30-35.
Kwa nini Yesu alisimulia mfano huo?
Yesu alimsimulia mfano huo mwanamume aliyefikiri kwamba watu wa jamii au dini yake tu ndio jirani zake. Yesu alitaka kumfundisha somo muhimu—alihitaji kupanua mawazo yake na kutambua kwamba “jirani” zake wanatia ndani pia watu ambao si Wayahudi wenzake. (Luka 10:36, 37) Simulizi hilo lilitiwa ndani ya Biblia kwa manufaa ya kila mtu anayetaka kumpendeza Mungu.—2 Timotheo 3:16, 17.
Tunajifunza nini kutokana na mfano huo?
Hadithi hiyo inatufundisha kwamba jirani mwema huonyesha huruma yake kwa matendo. Anachukua hatua ili kumsaidia mtu anayeteseka licha ya malezi, jamii, au taifa la mtu huyo. Jirani wa kweli huwatendea wengine kama ambavyo yeye angependa kutendewa.—Mathayo 7:12.
Wasamaria walikuwa nani?
Wasamaria waliishi katika eneo lililokuwa kaskazini ya Yudea. Walitia ndani watoto waliozaliwa kutokana na ndoa za Wayahudi na Wasio Wayahudi.
Kufikia karne ya kwanza W.K., Wasamaria walikuwa wamefanyiza dini yao wenyewe. Walikubali vitabu vitano vya kwanza vya Maandiko ya Kiebrania lakini walikataa vitabu vingine vyote.
Wayahudi wengi wa siku za Yesu waliwadharau Wasamaria na kuepuka kushirikiana nao. (Yohana 4:9) Baadhi ya Wayahudi walitumia neno “Msamaria” kama tusi.—Yohana 8:48.
Je, hadithi ya “Msamaria Mwema” ni tukio halisi?
Maandiko hayaonyeshi ikiwa mfano wa Msamaria ulitegemea tukio hususa. Hata hivyo, mara nyingi Yesu alitumia desturi na maeneo yaliyojulikana sana katika mafundisho yake ili wasikilizaji wake waelewe kwa urahisi jambo kuu ambalo alikuwa akifundisha.
Habari nyingi kuhusu mahali ambapo hadithi hiyo ilitokea ni sahihi kihistoria. Kwa mfano:
Barabara kutoka Yerusalemu hadi Yeriko—iliyokuwa na urefu wa zaidi ya kilomita 20—ilikuwa na mteremko wa kilomita 1 hivi. Simulizi hilo linasema kwa usahihi kwamba wasafiri waliokuwa wakielekea Yeriko ‘walikuwa wakishuka kutoka Yerusalemu.’—Luka 10:30.
Makuhani na Walawi walioishi Yeriko walisafiri kwenda Yerusalemu kwa ukawaida kupitia barabara hiyo.
Mara nyingi wezi walijificha kwenye barabara hiyo ambayo haikuwa na watu wengi wakiwasubiri wasafiri ambao hasa walisafiri peke yao.
a Mfano wa “Msamaria Mwema” unajulikana pia kama mfano wa “Msamaria Mwenye Ujirani.”