Mwanzo 19:1-38
19 Wale malaika wawili wakafika Sodoma jioni, na Loti alikuwa ameketi katika lango la Sodoma. Loti alipowaona, akasimama ili awapokee, akainama chini kifudifudi.+
2 Naye akasema: “Tafadhali, bwana zangu, tafadhali, karibuni nyumbani mwangu mimi mtumishi wenu, mlale hapa usiku wa leo, nasi tuioshe miguu yenu. Kisha mnaweza kuamka asubuhi na mapema na kuendelea na safari yenu.” Wakamwambia: “Hapana, tutakaa usiku kucha kwenye uwanja wa jiji.”
3 Lakini akawasihi sana hivi kwamba wakaingia pamoja naye ndani ya nyumba yake. Kisha akawaandalia karamu, akaoka mikate isiyo na chachu, nao wakala.
4 Kabla hawajalala, wanaume wa jiji—wanaume wa Sodoma kuanzia mvulana mpaka mzee, wote—wakaizingira nyumba hiyo wakiwa umati.
5 Nao walikuwa wakimwambia Loti kwa sauti: “Wako wapi wale wanaume waliokuja kwako usiku wa leo? Walete nje kwetu ili tufanye nao ngono.”+
6 Ndipo Loti akatoka nje kukutana nao mlangoni, naye akaufunga mlango nyuma yake.
7 Akasema: “Tafadhali, ndugu zangu, msitende uovu.
8 Tafadhali, humu nina mabinti wawili ambao hawajawahi kufanya ngono na mwanamume. Tafadhali, acheni niwalete nje kwenu muwatendee lolote mnaloona kuwa jema. Lakini msiwatendee lolote wanaume hawa, kwa sababu wamekuja chini ya kivuli cha* paa langu.”+
9 Ndipo wakasema: “Ondoka!” Halafu wakasema: “Mgeni huyu aliye peke yake alikuja kuishi hapa, na sasa anathubutu kutuhukumu! Sasa tutakutendea wewe jambo baya zaidi kuliko wao.” Wakamzingira Loti na kumbana* na kusogea mbele ili wauvunje mlango.
10 Basi wale wanaume* wakanyoosha nje mikono yao na kumwingiza Loti ndani ya nyumba walimokuwa, nao wakafunga mlango.
11 Lakini wakawapiga kwa upofu wanaume waliokuwa mlangoni, kuanzia mdogo zaidi mpaka mkubwa zaidi, hivi kwamba wakajichosha wakijaribu kuutafuta mlango.
12 Kisha wale wanaume* wakamwambia Loti: “Je, una mtu mwingine yeyote hapa? Wakwe zako, wanao, mabinti wako, na watu wengine wote wa ukoo jijini, waondoe mahali hapa!
13 Kwa maana tutaliangamiza jiji hili, kwa sababu kilio dhidi ya wakaaji wake kwa kweli kimeongezeka sana* mbele za Yehova,+ hivi kwamba Yehova ametutuma tuliangamize jiji hili.”
14 Kwa hiyo Loti akatoka nje na kuanza kuzungumza na wakwe zake ambao wangewaoa mabinti zake, akawaambia tena na tena: “Ondokeni! Ondokeni mahali hapa, kwa sababu Yehova ataliangamiza jiji hili!” Lakini machoni pa wakwe zake alionekana kama mtu anayefanya mzaha.+
15 Kulipokuwa kukipambazuka, malaika wakaanza kumhimiza Loti kwa uharaka, wakisema: “Fanya haraka! Mchukue mke wako na mabinti wako wawili walio hapa pamoja nawe, ili usifagiliwe mbali pamoja na uovu wa jiji hili!”+
16 Alipozidi kukawia, basi kwa sababu Yehova alimhurumia,+ wale wanaume* wakaushika mkono wake na mkono wa mke wake na mikono ya mabinti zake wawili, wakamtoa na kumpeleka nje ya jiji.+
17 Mara tu walipokuwa wamewatoa nje ya jiji, mmoja wao akawaambia: “Kimbieni msije mkafa! Msitazame nyuma+ wala msisimame mahali popote katika wilaya hii!+ Kimbilieni eneo lenye milima msije mkafagiliwa mbali!”
18 Kisha Loti akawaambia: “Tafadhali Yehova,* acha nisiende huko!
19 Sasa tafadhali, mimi mtumishi wako nimepata kibali machoni pako, nawe unanionyesha fadhili nyingi* kwa kunihifadhi hai,+ lakini siwezi kukimbilia eneo lenye milima kwa sababu ninaogopa kwamba huenda msiba ukanikumba nami nikafa.+
20 Sasa tafadhali, mji huu uko karibu nami ninaweza kukimbilia humo; ni mji mdogo tu. Tafadhali, ninaweza kukimbilia humo? Ni mji mdogo tu. Kisha nitaokoka.”*
21 Kwa hiyo akamwambia: “Sawasawa, nitakutendea pia kwa fadhili,+ sitauangamiza mji uliotaja.+
22 Fanya haraka! Kimbilia huko, kwa sababu sitafanya jambo lolote mpaka utakapofika huko!”+ Ndiyo sababu aliuita mji huo Soari.*+
23 Jua lilikuwa limechomoza nchini Loti alipofika Soari.
24 Kisha Yehova akaleta mvua ya kiberiti na moto juu ya Sodoma na Gomora—ilitoka kwa Yehova, kutoka mbinguni.+
25 Kwa hiyo akayaangamiza majiji hayo, naam, wilaya yote, pamoja na wakaaji wote wa majiji hayo na mimea yote.+
26 Lakini mke wa Loti, aliyekuwa nyuma ya Loti, akaanza kutazama nyuma, naye akawa nguzo ya chumvi.+
27 Sasa Abrahamu akaamka asubuhi na mapema na kwenda mahali alipokuwa amesimama mbele za Yehova.+
28 Alipotazama chini kuelekea Sodoma na Gomora na nchi yote ya wilaya hiyo, aliona jambo la kushangaza. Kulikuwa na moshi mzito uliokuwa ukipanda juu kutoka nchini kama moshi mzito wa tanuru!*+
29 Kwa hiyo Mungu alipoyaangamiza majiji ya wilaya hiyo, Mungu alimkumbuka Abrahamu kwa kumtoa Loti katika majiji aliyoyaangamiza, ambamo Loti alikuwa akiishi.+
30 Baadaye Loti akapanda kutoka Soari pamoja na mabinti zake wawili na kuanza kuishi katika eneo lenye milima,+ kwa sababu aliogopa kuishi Soari.+ Kwa hiyo akaanza kuishi pangoni pamoja na mabinti zake wawili.
31 Na mzaliwa wa kwanza akamwambia mdogo: “Baba yetu amezeeka, na hakuna mwanamume yeyote nchini anayeweza kulala nasi kama ilivyo desturi ya dunia yote.
32 Basi, tumpe baba yetu divai anywe, kisha tulale naye na kuhifadhi uzao wa baba yetu.”
33 Basi usiku huo wakampa baba yao divai nyingi anywe; kisha mzaliwa wa kwanza akaingia ndani na kulala na baba yake, lakini baba yake hakujua wakati alipolala naye wala alipoondoka.
34 Kisha siku iliyofuata, mzaliwa huyo wa kwanza akamwambia mdogo: “Jana usiku nililala na baba yetu. Na tumpe divai anywe usiku wa leo pia. Kisha uingie ndani na kulala naye, ili tuhifadhi uzao wa baba yetu.”
35 Basi usiku huo pia wakampa baba yao divai nyingi anywe; kisha yule binti mdogo akaingia ndani na kulala naye, lakini baba yake hakujua wakati alipolala naye wala alipoondoka.
36 Kwa hiyo mabinti wote wawili wa Loti wakapata mimba kutoka kwa baba yao.
37 Mzaliwa wa kwanza alizaa mwana na kumpa jina Moabu.+ Yeye ndiye baba ya Wamoabu wa leo.+
38 Yule mdogo pia alizaa mwana, akampa jina Ben-ami. Yeye ndiye baba ya Waamoni+ wa leo.
Maelezo ya Chini
^ Au “ulinzi wa.”
^ Au “Wakasongamana kumzunguka Loti.”
^ Yaani, malaika waliovaa miili ya kibinadamu.
^ Yaani, malaika waliovaa miili ya kibinadamu.
^ Au “kimekuwa kikubwa.”
^ Yaani, malaika waliovaa miili ya kibinadamu.
^ Yaani, malaika waliomwakilisha Yehova.
^ Au “upendo mshikamanifu.”
^ Au “nafsi yangu itaendelea kuishi.”
^ Maana yake “Udogo.”
^ Au “kalibu.”