Je, Ni Watoto wa Wakati Ujao?
Je, Ni Watoto wa Wakati Ujao?
Ni mwaka wa 2050. Melissa atazama skrini ya kompyuta akiwa katika kliniki ya uzazi. Anawaza na kuwazua. Kwani, kuchagua mtoto ni jambo zito, si jambo la kufanywa hima-hima. Skrini yaonyesha picha ya msichana mwenye tabasamu ambaye tayari Melissa na mumewe, Curtis, wamemwita Alice. Picha hiyo na habari zilizoandikwa kando yake hueleza mengi kuhusu atakavyokuwa Alice, kimwili na kiakili.
Alice hajazaliwa bado. Kijana huyo wa wakati ujao angali kiinitete, amehifadhiwa salama katika baridi kali ya nyuzi Selsiasi 200 pamoja na viinitete vingine vingi katika chumba kilicho karibu. Umbile la chembe za urithi za kila kiinitete lilipigwa picha na kuhifadhiwa kwenye kompyuta ili kuwasaidia wazazi wachague kiinitete kitakachopandikizwa kwenye tumbo la uzazi la Melissa.
Viinitete vya kiume havichunguzwi kwa kuwa Melissa na Curtis wanataka msichana. Kisha wazazi hao wanachunguza afya, sura, na tabia ambazo viinitete vinavyosalia vitakuwa nazo. Hatimaye Melissa na Curtis wafanya uchaguzi. Miezi tisa baadaye wanafurahia kumzaa binti waliyemchagua—Alice, aliye halisi na hai.
KISA hicho ni muhtasari wa simulizi lililoandikwa na Lee Silver, profesa wa biolojia ya molekuli katika Chuo Kikuu cha Princeton, New Jersey, Marekani. Ni kisio la mambo anayoamini yaweza kutukia miaka mingi ijayo. Alitegemeza dhana zake kwa utafiti na tekinolojia iliyopo sasa. Hivi sasa, viinitete vya wanadamu vyaweza kuchunguzwa kwa makini iwapo vina kasoro fulani za chembe za urithi. Zaidi ya miaka 20 imepita tangu kuzaliwa kwa mtoto wa kwanza ambaye mimba yake ilitungiwa kwenye maabara. Mimba yake ilitungiwa kwenye kibakuli cha kioo, hivyo akawa mwanadamu wa kwanza kutungiwa nje ya tumbo la uzazi la mamaye.
Jina la mtoto huyo, Alice, alilopewa na Dakt. Silver yamkini latukumbusha hadithi mashuhuri ya kubuniwa ya Alice in Wonderland. Kwa kweli, wakati ujao unaotarajiwa na wengi ni kama nchi ya kustaajabisha. Safu ya mhariri katika gazeti Nature lililo maarufu yasema: “Ukuzi wa utaalamu wa chembe za urithi na molekuli hutupa tumaini la kuweza kubadili umbile la viumbe wakati ujao.”
Katika makala ifuatayo, tutachunguza baadhi ya maendeleo katika sayansi ya kurekebisha chembe za urithi, tutakazia hususan taraja la “kuboresha” jamii ya kibinadamu. Je, kazi inayofanywa kwenye maabara leo itaathiri maisha yako au ya watoto wako? Wengi wanaamini kwamba itaathiri.