Mawimbi Yanayofisha Hekaya na Ukweli
Mawimbi Yanayofisha Hekaya na Ukweli
JUA limetua hivi punde. Siku hiyo tulivu ya Ijumaa, Julai 17, 1998, wanaume, wanawake, na watoto wa vijiji kadhaa vidogo kwenye pwani ya kaskazini ya Papua New Guinea waligutushwa ghafula na tetemeko la dunia lenye kipimo cha 7.1. “Tetemeko kuu,” lasema gazeti la Scientific American, “lilitikisa ukanda wa pwani wenye umbali wa kilometa 30 (takriban maili 19) . . . na ghafula lilibomoa sakafu ya bahari karibu na ufuo. Uso wa bahari ambao kwa kawaida huwa mtulivu uliyumbayumba kwa nguvu kama tokeo, kisha kukazuka tsunami (mawimbi yenye nguvu) yenye kutisha.”
Mtazamaji mmoja asema kwamba alisikia sauti kama ya mngurumo wa radi toka mbali, sauti hiyo ilididimia polepole bahari iliposhuka taratibu chini ya kimo cha chini cha maji. Dakika chache baadaye, aliona wimbi la kwanza, lililokuwa na kimo cha meta tatu hivi. Lilimpiga alipokuwa akijaribu kutoroka. Wimbi la pili lililo kubwa zaidi, lilifagia kijiji chao na kumsomba kwa umbali wa kilometa moja hivi, na kumbwaga kwenye msitu wa mikoko ulio karibu. “Vifusi vilivyoning’inia kwenye michikichi vilionyesha kwamba mawimbi hayo yalifikia kimo cha meta 14 [futi 46],” laripoti gazeti la Science News.
Jioni hiyo mawimbi makubwa kupindukia yaliangamiza angalau watu 2,500. Jambo kinyume la kustaajabisha ni kwamba, kampuni moja ya mbao ilichanga mbao kwa ujenzi wa shule mpya, lakini ilionekana ni kana kwamba hakukuwa na watoto waliosalia kwenda shuleni. Karibu watoto wote—zaidi ya 230—walikuwa wameangamizwa na mawimbi hayo ya tsunami.
Tsunami Ni Nini?
Tsunami ni neno la Kijapani limaanishalo “wimbi la bandarini.” Neno hilo “lafaa,” chasema kitabu Tsunami!, “kwa sababu mawimbi hayo makubwa kupindukia mara nyingi
yamesababisha vifo na uharibifu kwenye bandari na vijiji vilivyo kwenye pwani ya Japani.” Ni nini kinachofanya mawimbi hayo yenye kutisha yawe makubwa mno na yawe na nguvu nyingi sana?Nyakati nyingine Tsunami huitwa mawimbi ya bahari iliyojaa. Hata hivyo, kwa kweli mawimbi ya bahari iliyojaa ni mawimbi tu yanayoinuka na kutapakaa ambayo husababishwa na nguvu za uvutano za jua na mwezi. Hata mawimbi makubwa—ambayo nyakati nyingine huwa na kimo cha zaidi ya meta 25—yanayoinuliwa juu na pepo kali sana hayawezi kulinganishwa na tsunami. Ikiwa ungepiga mbizi katika mawimbi hayo ya bahari iliyojaa, ungegundua kwamba huwa hafifu zaidi kadiri unavyoenda chini. Kwenye kina fulani, maji hubaki matulivu tu. Lakini sivyo ilivyo na tsunami. Mawimbi hayo huanza kwenye uso wa maji na kufika kwenye sakafu ya bahari, bila kujali kina cha maji!
Mawimbi ya tsunami hufika chini kabisa baharini kwa sababu kwa kawaida yanasababishwa na mabadiliko makali ya umbo la miamba kwenye sakafu ya bahari. Kwa sababu hiyo, nyakati nyingine wanasayansi hurejezea tsunami kuwa mawimbi ya tetemeko la dunia. Sakafu ya bahari yaweza kuinuka, na hivyo kuinua maji yaliyo juu yake na kutokeza wimbi laini, ambalo laweza kusambaa kwenye eneo lenye ukubwa wa kilometa 25,000 za mraba. Au huenda sakafu ya bahari ikazama, na ghafula kukatokea shimo kwenye sakafu hiyo.
Kwa vyovyote vile, nguvu za uvutano hufanya maji hayo yapande na kushuka—kusogea huko husababisha mawimbi mfululizo yanayoibuka kwenye kitovu kimoja, kama yale yanayotokea jiwe linapotumbukia kwenye kidimbwi. Utaratibu huo unafutilia mbali hekaya inayopendwa sana ya kwamba tsunami ni mawimbi ya pekee tu yenye balaa. Badala yake, kwa kawaida mawimbi hayo husambaa na kufanyiza ule unaoitwa mkondo wa mawimbi ya tsunami. Mawimbi ya tsunami yaweza pia kusababishwa na milipuko ya volkano au maporomoko ya ardhi yanayotukia baharini.
Mojawapo ya tsunami zenye uharibifu mkubwa zaidi katika historia yote zilitokea mnamo Agosti 1883, na zilisababishwa na mlipuko wa Mlima Krakatau, ambao ni mlima wa volkano nchini Indonesia. Baadhi ya mawimbi yake yalifikia kimo cha kustaajabisha cha meta 41 juu ya uso wa bahari na yalifagilia mbali takriban miji na vijiji 300 vya pwani. Yaelekea idadi ya watu waliokufa ilizidi 40,000.
Pande Mbili za Tsunami
Mawimbi yanayosababishwa na upepo hayazidi mwendo wa kilometa 100 kwa saa, na kwa kawaida husonga polepole. “Kwa upande mwingine, mawimbi ya tsunami,” chasema kitabu Tsunami!, “yaweza kusonga kasi kama jeti, kwa mwendo wa kustaajabisha wa kilometa 800 kwa saa au zaidi katika sehemu yenye kina kwenye bonde la baharini.”
Lakini, licha ya mwendo wake, huwa si hatari katika maji yenye kina. Kwa nini?Kwanza, kwa sababu wimbi moja kwa kawaida huwa na kimo kinachopungua meta tatu baharini; na pili, kwa sababu wimbi hilo laweza kuwa na upana wa mamia ya kilometa toka kilele hadi kilele, na hivyo huwa na mteremko laini. Kwa hiyo, mawimbi ya tsunami yanaweza kupita chini ya meli bila hata kugunduliwa. Nahodha mmoja wa meli iliyokuwa imetia nanga karibu na pwani ya mojawapo ya Visiwa vya Hawaii hakujua kabisa kwamba tsunami ilikuwa imepita hadi alipoona mawimbi makubwa sana yakipiga ufuo ulio mbali. Sheria ya kawaida ya usalama wa meli baharini ni kwamba zapasa kuabiri katika maji yenye kina cha angalau meta 180, au futi 600.
Mawimbi ya tsunami hubadilika-badilika yanapokaribia barani na kufika kwenye maji yasiyo na kina. Hapo, msuguano na sakafu ya bahari hupunguza mwendo wa mawimbi hayo—lakini si kila mahali. Sehemu ya nyuma ya wimbi sikuzote huwa katika maji yenye kina kuliko sehemu ya mbele na kwa hiyo inasonga kasi zaidi. Kama tokeo, wimbi hilo husongamana, na kufikia kimo cha juu sana kwa sababu ya kupungua kwa mwendo wake. Wakati huohuo, mawimbi yaliyo nyuma katika mkondo huo hufika, na kurundamana kwenye mawimbi yaliyo mbele.
Katika hatua zake za mwisho, mawimbi ya tsunami yanaweza kupiga sehemu ya pwani yakiwa mawimbi yenye nguvu au wimbi kubwa sana, lakini kwa kawaida, huwa mafuriko yanayopanda kwa kasi sana ambayo hutapakaa na kuzidi kimo cha kawaida cha maji. Maji yameonekana yakifurika kwa zaidi ya kimo cha meta 50 juu ya usawa wa kawaida wa bahari na kusomba vifusi, samaki, hata vipande vya matumbawe kwa umbali wa maelfu ya meta barani, huku yakiharibu kabisa kila kitu kilicho mbele yake.
Mawimbi ya tsunami huhadaa kwa sababu, mwanzoni huwa hayaonekani sikuzote kuwa wimbi kubwa linalokuja kasi kuelekea ufuoni. Huenda ikawa kinyume kabisa—maji kupwa isivyo kawaida na kuacha fuo, ghuba, na bandari zikiwa kavu kabisa huku samaki wakitapatapa mchangani au matopeni. Hali hiyo hutegemea jinsi mawimbi yanavyofika ufuoni—yakiwa yameinuka au kushuka. *
Ufuo Unapokauka
Kisiwa cha Hawaii cha Maui kilikuwa shwari jioni ya Novemba 7, 1837. Mwendo wa saa moja jioni, chaeleza kitabu Tsunami!, maji yalianza kupungua ufuoni, na kuacha miamba ikiwa wazi na samaki wakiwa wametatanika. Wanakisiwa wengi wenye msisimko walikimbia kukusanya samaki hao, lakini watu wachache, waliokuwa chonjo zaidi, walikimbilia sehemu zilizoinuka, yaelekea walifahamu kutokana na matukio ya kale jambo ambalo lingetukia hivi punde. Muda si muda, wimbi kubwa lenye kutisha la maji lilipiga eneo hilo na kusomba kijiji kizima chenye nyumba za nyasi 26, pamoja na wakazi na mifugo, kwa umbali wa meta 200 barani na kuwabwaga katika ziwa dogo.
Jioni hiyohiyo, maelfu ya watu walikuwa wamekusanyika ufuoni kwa ajili ya ibada ya kidini
kwenye kisiwa kingine. Kwa mara nyingine tena, kupwa ghafula kwa maji kulifanya halaiki ya wakazi wa Hawaii wenye udadisi wamiminike ufuoni. Kisha, wimbi kubwa kupindukia, lenye kuzidi kimo cha kawaida cha bahari kwa meta sita, lilizuka ghafula na kuelekea ufuoni “kasi sana kama farasi mbioni,” akasema mtazamaji mmoja. Maji yaliyokuwa yakirejea yaliwabeba hata waogeleaji hodari hadi baharini, ambako baadhi yao walikufa maji kwa sababu ya uchovu.Mawimbi Hayo Huzuka Mara Nyingi Kadiri Gani?
“Tangu mwaka wa 1990,” lasema gazeti la Scientific American, “zaidi ya watu 4,000 wamekufa katika misiba 10 ya tsunami. Kwa ujumla, iliripotiwa kwamba tsunami 82 zilizuka ulimwenguni pote—idadi ya juu sana kupita wastani wa kihistoria wa 57 kwa mwongo mmoja.” Hata hivyo, ongezeko hilo lililoripotiwa, gazeti hilo laongezea, linatokana hasa na mawasiliano yaliyoboreshwa, ilhali idadi kubwa ya vifo inasababishwa kwa sehemu na kuongezeka kwa idadi ya watu katika maeneo ya pwani.
Bahari ya Pasifiki hupatwa sana na tsunami hasa kwa sababu matetemeko mengi ya dunia hutukia katika bonde lake. Kwa kweli, “ni nadra sana kwa mwaka kupita bila kuzuka kwa angalau tsunami moja yenye uharibifu mkubwa sehemu fulani ya Pasifiki,” chasema kichapo kimoja ambacho chasema pia kwamba “katika miaka hamsini iliyopita, asilimia 62 ya vifo vyote vinavyotokana na matetemeko ya dunia nchini Marekani vimesababishwa na tsunami.”
Je, Zaweza Kutabiriwa?
Kati ya mwaka wa 1948 na 1998, asilimia 75 hivi ya maonyo yote ya tsunami yaliyotolewa huko Hawaii yalikuwa bandia. Ni wazi kwamba, rekodi hiyo huwafanya watu wasitahadhari. Lakini, mfumo bora zaidi wa kutabiri, unaotegemea tekinolojia ya kisasa, sasa unatumiwa. Mfumo huo bora wa kutabiri hasa una kifaa cha kupima kanieneo ya kilindi (BPR), ambacho, kama jina linavyodokeza, hutiwa maelfu ya meta chini, kwenye kilindi cha bahari.
Chombo hicho chenye kupima kwa wepesi chaweza kupima tofauti katika kanieneo ya maji huku mawimbi ya tsunami yakipitia juu—hata inapopungua sentimeta moja tu. Mfumo wa BPR hutumia mawimbi ya sauti kutuma ujumbe kwa boya maalumu, ambayo hutuma ujumbe huo kwa setilaiti. Kisha, setilaiti hurusha ujumbe huo kwa kituo kinachotoa maonyo ya tsunami. Wanasayansi wana hakika kwamba mfumo huu sahihi unaotoa onyo la mapema utapunguza maonyo bandia.
Labda harakati muhimu sana za usalama ni kufahamisha na kuelimisha umma. Hata mfumo bora zaidi wa kuonya ni bure tu ikiwa watu wataupuuza. Kwa hivyo ikiwa unaishi kwenye mwambao wa pwani ulio chini ambao hukumbwa sana na tsunami, halafu wenye mamlaka wanatangaza onyo la tsunami au unagundua tetemeko la dunia au waona maji yakipwa isivyo kawaida, hakikisha kwamba unahamia mara moja eneo lililo juu. Kumbuka kwamba, mawimbi ya tsunami yanaweza kusonga kasi baharini kama jeti, na yanaweza kusonga kasi sana karibu na ufuo. Kwa hiyo, mara tu uonapo mawimbi hayo, yaelekea kwamba hutaweza kamwe kutoroka hatari. Hata hivyo, iwapo unakumbana na tsunami ukiwa melini au ukivua samaki sehemu yenye kina baharini, usiwe na wasiwasi—yaelekea kwamba hayatakudhuru hata kidogo wala kukutikisa.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 16 Gazeti la Discover linasema kwamba, mwendo wa mzunguko au wa duara wa maji unaotukia katika mawimbi yote unachangia kupungua kwa maji. Watu wanaoogelea baharini huhisi wakivutwa baharini kabla tu ya wimbi kuwafikia. Mvuto huo huwa na nguvu sana katika tsunami na ndio unaosababisha kupwa kwa maji kwenye fuo au bandari kabla tu ya wimbi la kwanza kupiga.
[Picha katika ukurasa 25]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Mara nyingi “tsunami” husababishwa na tetemeko la dunia kwenye sakafu ya bahari
UFA
KUIBUKA
KUSAMBAA
MAFURIKO
[Mchoro katika ukurasa wa 27]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Tekinolojia mpya, inayotumia vyombo vya kupima katika vilindi vya bahari, hujaribu kutabiri “tsunami”
MAWASILIANO YA SETILAITI
BOYA
KIPIMA-SAUTI
NANGA
MAWIMBI YA SAUTI
KIPIMIO CHA TSUNAMI
Meta 5,000
[Hisani]
Karen Birchfield/NOAA/Pacific Marine Environmental Laboratory
[Picha katika ukurasa 25]
“Tsunami” ilivurumisha ubao uliotoboa gurudumu hili la lori
[Hisani]
U.S. Geological Survey
[Picha katika ukurasa 26]
Mnara wa taa wa Scotch Cap huko Alaska kabla ya pigo la “tsunami” la mwaka wa 1946 (kushoto)
Uharibifu mkubwa sana uliotokea (juu)
[Hisani]
U.S. Coast Guard photo
[Picha katika ukurasa 24 zimeandaliwa na]
U.S. Department of the Interior