Mama na Binti Zake Kumi
Mama na Binti Zake Kumi
KAMA ILIVYOSIMULIWA NA ESTHER LOZANO
MAMA na Baba walizaliwa huko Bitlis, Uturuki, na wazazi Waarmenia. Mapema katika karne iliyopita, kulipokuwa na mauaji mengi ya Waarmenia, baba yetu aliondoka Uturuki na kuelekea Marekani. Alikuwa na umri wa miaka 25 hivi. Mama yetu Sophia, aliondoka baadaye, alipokuwa na umri wa miaka 12.
Inaonekana kwamba wazazi wa familia hizo mbili walikubaliana kumpeleka mama yetu Marekani akaolewe na baba yetu, Aram Vartanian. Sophia alikuwa mchanga sana kuweza kuolewa alipofika Fresno, California, kwa hiyo aliishi pamoja na yule ambaye angekuwa mama-mkwe wake hadi alipofikia umri wa kuolewa.
Mtoto wa kwanza wa wazazi wetu alikuwa mvulana ambaye walimwita Antranig, kisha baadaye akabadili jina lake kuwa Barney. Alizaliwa Agosti 6, 1914. Watoto kumi wengine wote waliofuata walikuwa wasichana. Baba yetu akawa Mwanafunzi wa Biblia, kama vile Mashahidi wa Yehova walivyojulikana wakati huo, wakati ambapo Shield Toutjian alitembelea Fresno na kuwatolea hotuba Waarmenia mwaka wa 1924. Baada ya hapo, familia yetu nzima ilihudhuria mikutano ya Kikristo pamoja.
Tulihamia Oakland, California, mwaka wa 1931 na kushirikiana na kutaniko la huko. Barney alimtumikia Yehova kwa uaminifu huko Napa, California,
hadi alipokufa mwaka wa 1941. Mimi nilikuwa msichana wa tatu kuzaliwa baada ya Barney na nilionyesha wakfu wangu kwa Yehova mwaka wa 1935. Dada yetu Agnes alibatizwa hivi karibuni baada ya kuhudhuria mikutano kwa miaka 75 hivi! Sisi sote tulikuwepo wakati wa ubatizo wake, nasi tulifurahi sana kwamba msichana wa mwisho kati ya kumi sasa alikuwa amebatizwa.Kwa kusikitisha, Mama hakuwepo. Alikufa mwaka mmoja tu kabla ya tukio hilo akiwa na umri wa miaka 100 na siku 2. Kifo chake kilitangazwa kwenye gazeti Hayward News la California la Mei 14, 1996. Gazeti hilo lilisema kwamba “alifanya utumishi wa kujitolea kwa jamii akiwa Shahidi wa Yehova kwa kufundisha . . . watu wanaopendezwa na Biblia kwa miaka 54.” Pia habari hiyo ilimnukuu dada yetu Elizabeth akisema: “Nyumba yake ilikuwa wazi sikuzote na alikuwa mkaribishaji sana . . . Sikuzote angesema, ‘Njoo unywe kahawa chungu,’ na kama ungeenda wakati ametengeneza kitobosha (aina fulani ya mkate) chake kilichopendwa sana, ungefurahia wakati huo kwelikweli.”
Dada yetu mkubwa, Gladys, ana umri wa miaka 85 na yule mdogo zaidi ana umri wa miaka 66. Sisi sote ni Mashahidi wenye bidii. Watatu kati yetu tulitumikia tukiwa mishonari baada ya kuhitimu kutoka Shule ya Biblia ya Gileadi ya Watchtower. Elizabeth, ambaye sasa anaishi Newport Beach, California, alikuwa katika darasa la 13 la shule hiyo na akatumikia huko Callao, Peru, kwa miaka mitano. Ruth alihudhuria darasa la 35. Yeye na mume wake, Alvin Stauffer, walitumikia wakiwa mishonari katika Australia kwa miaka mitano. Nilikuwa katika darasa la nne la Gileadi na mwaka wa 1947 nikapewa mgao wa kwenda Mexico, ambako mnamo mwaka wa 1955, niliolewa na Rodolfo Lozano. * Sisi wawili tumetumikia nchini Mexico tangu hapo.
Tukiwa dada kumi tunashukuru sana kuwa na afya nzuri kiasi. Afya hiyo huturuhusu twendelee kumtumikia Yehova kwa akili, moyo, na nguvu yetu yote kadiri anavyoturuhusu—sasa na hata milele katika ulimwengu wake mpya.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 8 Simulizi lake la maisha laweza kupatikana katika Mnara wa Mlinzi la Januari 1, 2001.
[Picha katika ukurasa wa 20]
Agnes alipokuwa anabatizwa, 1997
[Picha katika ukurasa wa 20, 21]
Elizabeth, siku aliyohitimu kutoka Gileadi, 1949
[Picha katika ukurasa wa 21]
Esther (kulia) katika ofisi ya tawi ya Mexico, 1950
[Picha katika ukurasa wa 21]
Ruth na Alvin Stauffer wakitumikia wakiwa watumishi wa kimataifa katika ofisi ya tawi ya Mexico, 1987