Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kochinili Ni Mdudu wa Pekee Sana

Kochinili Ni Mdudu wa Pekee Sana

Kochinili Ni Mdudu wa Pekee Sana

NA WAANDISHI WA AMKENI! NCHINI MEXICO NA PERU

RANGI nyekundu nyangavu ya midomo na ya vipodozi vingine inatokana na nini? Huenda ukashangaa kusikia kwamba mara nyingine rangi hiyo inatokana na mdudu anayeitwa kochinili ambaye chakula chake ni dungusi-kakati aina ya mpungate-miiba. Acha tuchunguze huyo mdudu wa pekee.

Je, Ni Mdudu Anayedhuru au Mwenye Faida?

Mdudu wa kochinili wa kike ana urefu wa milimeta tatu hivi. Ukubwa wake ni sawa na ukubwa wa kichwa cha kibiriti. Ukubwa wa wadudu wa kiume ni karibu nusu ya ule wa kike. Lakini ijapokuwa mdudu huyo ni mdogo anaweza kusababisha uharibifu mkubwa sana. Kitabu kimoja cha wasomi kinasema hivi: “Mdudu huyo ni mmojawapo wa wadudu waharibifu sana.” Hata hivyo, baadhi ya wakulima huwazalisha. Kwa nini? Wao hufanya hivyo ili kutengeneza rangi nyekundu kwa kutumia miili iliyokaushwa na kupondwa ya wadudu wa kochinili wa kike.

Tangu siku za watu wa kale wa Mixtec, walioishi katika sehemu ambayo sasa ni jimbo la Oaxaca huko Mexico, wadudu hao wametumiwa kutengeneza rangi. Washindi Wahispania walivutiwa sana na rangi hiyo nyekundu, na punde Wazungu wengi wakaanza kutumia rangi hiyo nyangavu. Rangi nyekundu iliyotokana na wadudu hao ilitumiwa kuyatia rangi mavazi maalumu ya askari-jeshi huko Uingereza. Rangi hiyo ilitumiwa sana hivi kwamba kuanzia mwaka wa 1650 hadi mwaka wa 1860 iliuzwa kwa faida kubwa kuliko dhahabu na fedha huko Mexico.

Utumizi Ulipunguka kwa Muda

Katikati ya miaka ya 1800, rangi zilizotengenezwa kwa kemikali zilianza kupendwa badala ya rangi zilizotengenezwa kwa vitu vya asili. John Henkel, mwandishi wa gazeti la FDA Consumer anaeleza hivi: “Ilikuwa rahisi kutengeneza rangi kwa kemikali, zilikuwa za bei nafuu, na rangi hizo zilikuwa bora kuliko rangi zilizotengenezwa kwa vitu vya asili.” Hivyo, upesi rangi za kemikali ndizo zilizotumiwa kutia rangi kwenye vyakula, dawa, na vipodozi. “Lakini,” Henkel anasema kwamba “utumizi wa rangi hizo ulipozidi, watu walianza kuwa na wasiwasi kuhusu athari zake.”

Uchunguzi mbalimbali uliofanywa miaka ya 1970 ulionyesha kwamba huenda ikawa rangi fulani za kemikali zinasababisha kansa. Ilipojulikana kwamba rangi hizo za kemikali zinaweza kusababisha magonjwa, watu walianza kutumia tena rangi zilizotengenezwa kwa vitu vya asili. Kwa mfano, kwa sasa, asilimia 85 ya rangi yote inayotokana na mdudu wa kochinili inatengenezwa nchini Peru. Rangi hiyo inatengenezwa pia katika Visiwa vya Canary, katika sehemu ya kusini mwa Hispania, Algeria, na nchi mbalimbali za Amerika ya Kati na Kusini. Hata hivyo, leo uhitaji wa rangi hiyo unaongezeka, kwa hiyo, serikali ya Mexico inajitahidi kuitengeneza kwa wingi zaidi.

Jinsi Rangi Nyekundu Inavyotengenezwa

Mdudu huyo wa kochinili huishi maisha yake yote kwenye dungusi-kakati inayoitwa mpungate-miiba. Yeye hujilinda kwa kutoa kitu kama ungaunga unaofanana na nta. Kitu hicho humfunika mdudu kabisa na huwa makao yake. Lakini kwa sababu ya kifuniko hicho mdudu huyo anaonekana kwa urahisi wakati wa mavuno.

Ni wadudu wa kike pekee ndio walio na rangi hiyo nyekundu. Wadudu wa kike wenye mimba ndio walio na rangi nyingi zaidi. Kwa hiyo, ili kupata rangi bora, wafanyakazi huvuna wadudu wa kike kabla hawajataga mayai. Katika Milima ya Andes huko Peru, wadudu hao huvunwa mara tatu katika muda wa miezi saba. Burashi au kisu butu hutumiwa kuondoa wadudu hao kutoka kwenye dungusi-kakati. Baada ya kuwakausha, kuwasafisha, na kuwaponda, wadudu hao wanakuwa kama unga, na unga huo huwekwa katika kemikali aina ya amonia au sodiamu kaboneti. Sehemu za miili za wadudu huondolewa kwa kuchujwa na umajimaji unaobaki huwa safi. Chokaa inaweza kuongezwa pia ili kutengeneza rangi ya zambarau.

Huenda mtu akachukizwa kujua kwamba vipodozi anavyotumia vimetengenezwa kwa wadudu. Lakini kama vile Henkel anavyosema, unaweza kuwa na uhakika kwamba ‘rangi zinazotengenezwa kwa vitu vya asili zimechunguzwa kwa makini sana, tena na tena.’ Kwa hiyo, ukiambiwa kwamba uso wako umeng’ara, huenda ikawa ni kwa sababu vipodozi unavyotumia vinatokana na kochinili ambaye ni mdudu wa pekee sana.

[Picha katika ukurasa wa 23]

1. Wadudu wa kochinili kwenye dungusi-kakati

2. Picha iliyokuzwa ya wadudu wa kike walio na mimba

3. Wadudu wa kochinili waliokaushwa

4. Kutayarisha umajimaji unaotumiwa kutengeneza vipodozi

[Hisani]

Picha kwenye ukurasa wa 23: #1: The Living Desert, Palm Desert, CA; #3 and products: Cortesía del Centro de Investigaciones Económicas, Sociales y Tecnológicas para la Agroindustria y la Agricultura Mundial, Universidad Autónoma de Chapingo, fotografía de Macario Cruz; #4: David McLain/AURORA

[Picha katika ukurasa wa 23]

Vitu vilivyotengenezwa kwa rangi hiyo nyekundu