Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Vitabu Milioni Kumi Katika Nyumba ya Vioo

Vitabu Milioni Kumi Katika Nyumba ya Vioo

Vitabu Milioni Kumi Katika Nyumba ya Vioo

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI UFARANSA

MGENI anapopanda ngazi ya mbao kuelekea uwanja, hakosi kuvutiwa—hata kuhofu—anapoona ile minara minne mirefu ya vioo. Hili si jengo la kawaida. Jengo hilo ni Maktaba ya kisasa kabisa ya Kitaifa ya Ufaransa. Katika maana fulani, ujenzi wake umechukua karne nyingi.

Historia ya Mapema

Mnamo mwaka wa 1368, Charles wa Tano alikusanya karibu hati 1,000 na kuziweka katika mnara wa ngome ya Louvre huko Paris. Lakini ilikuwa baada ya Vita vya Miaka Mia Moja ambapo wafalme wa Ufaransa walianza kuwa na maktaba ya kudumu. Zawadi na urithi ulioachwa na wale waliotaka kupendelewa na mfalme, pamoja na vitabu vilivyoletwa kutoka Ulaya na nchi za Mashariki na wasafiri, mabalozi, au wanajeshi vikiwa nyara, viliwekwa katika maktaba hiyo. Kisha, katika miaka ya 1500, Francis wa Kwanza akatunga sheria iliyoamuru nakala moja ya kila kitabu kilichochapishwa iwekwe katika Maktaba ya Mfalme.

Baada ya kuhamishwa hadi kwenye makao mbalimbali ya kifalme katika mikoa mbalimbali, maktaba hiyo ilirudishwa Paris, hadi ilipoporwa katika Vita vya Kidini (1562-1598). Maktaba hiyo ilihamishwa mahali ambapo ilibaki kwa muda mrefu mwaka wa 1721. Baada ya Mapinduzi ya Ufaransa, vichapo vya kidini na vya maktaba za makabaila vilipotwaliwa, maktaba hiyo iliongezewa mamia ya maelfu ya vitabu, hati, na picha. Ingawa vitu hivyo vilikuwa vya thamani kubwa, hakukuwa na nafasi ya kutosha katika majengo yaliyokuwako.

Upanuzi Mkubwa

Mnamo mwaka wa 1868, chumba cha kusomea kilichofunikwa kwa kuba tisa za vioo kilijengwa na kuzinduliwa. Chumba hicho kilibuniwa na mchoraji wa ramani Henri Labrouste, na kilikuwa na nafasi ya kuketi wasomaji 360 na kuweka vitabu 50,000. Rafu zilizokuwa karibu zilikuwa na nafasi ya vitabu milioni moja zaidi. Lakini baada ya miaka sitini, idadi ya vitabu ilizidi milioni tatu!

Ijapokuwa marekebisho na upanuzi, nafasi haikutosha kwa rafu za urefu wa kilometa tatu zilizohitajiwa kila mwaka kwa sababu vitabu na magazeti yaliongezeka sana. Hatimaye, mnamo mwaka wa 1988, Rais François Mitterrand alitangaza mradi wa kujenga labda “maktaba kubwa na ya kisasa zaidi ulimwenguni.” Kusudi lilikuwa “kuwa na vitabu vya elimu zote, watu wote waweze kufaidika navyo, kutumia mbinu za kisasa zaidi za mawasiliano, kufikika kutoka mbali, na kuunganika na maktaba nyingine za Ulaya.”

Ili kuchora ramani ya maktaba hiyo mpya, shindano la kimataifa lilifanywa na michoro 250 hivi ilitumwa. Hatimaye, mchoro wa mchoraji wa ramani, Mfaransa asiye mashuhuri, Dominique Perrault, ulikubaliwa. Mchoro wake ulionyesha jengo kubwa la mraba lenye mnara katika kila pembe uliofanana na kitabu kilichofunguliwa. Wachambuzi walipinga mchoro huo wakisema haingefaa kuweka vitabu katika mnara uliotengenezwa kwa vioo ambapo vitabu vingeharibiwa na mwangaza na joto la jua. Ili kutatua tatizo hilo, iliamuliwa kwamba vizuizi vya mbao viwekwe nyuma ya madirisha ili vitabu visiharibiwe na jua. Vichapo vya thamani vingewekwa katika mraba wa chini.

Kazi Ngumu ya Kuhamisha Vitabu

Tatizo kubwa lilikuwa kuhamisha zaidi ya vitabu milioni kumi, kukiwa na vingi ambavyo vingeharibika kwa urahisi na visivyoweza kupatikana tena, kama nakala mbili za Biblia ya Gutenberg. Matatizo yalitokea vitabu hivyo vilipohamishwa. Kulingana na mtu mmoja aliyekuwapo vitabu hivyo vilipohamishwa mwaka wa 1821, vitabu vingi vilianguka kutoka kwa magari yaliyokokotwa na farasi na kuingia kwenye matope barabarani. Wakati huu, vitabu vingehamishwa kwa utaratibu wa kitaalamu.

Mnamo mwaka wa 1998 kikundi cha wataalamu kilianza kazi kubwa ya kuhamisha mamilioni ya vitabu. Ili kuzuia visiharibike, visiibwe, au visipotee, vitabu vilifungwa ndani ya masanduku ambayo maji hayakuweza kupenya, kushika moto, na ambayo yangezuia vitabu visiharibike hata kama yangeanguka. Kwa muda wa mwaka mmoja hivi, malori kumi ya mizigo, yasiyotambulishwa kwa ajili ya usalama, yalisafiri kwenye barabara za Paris zenye msongamano mkubwa wa magari yakipeleka vitabu 25,000 hadi 30,000 kila siku hadi kwenye maktaba mpya.

Nyumba Yenye Vitabu Vingi

Maktaba hiyo mpya ina orofa mbili. Katika orofa ya haut-de-jardin (bustani ya juu), watu wote wanaweza kupata vitabu 350,000 kwa urahisi na kina nafasi 1,600 za kuketi. Orofa ya rez-de-jardin (bustani ya chini) ina viti 2,000, kwa ajili ya watafiti.

Maktaba hiyo imejengwa kuzunguka msitu mdogo. Mazulia mekundu na kuta na fanicha za mbao huchangia hali ya utulivu inayowaruhusu watu kusoma na kutafakari. Katika chumba kimoja watu wanaweza kutumia CD-ROM, video, kaseti, na maelfu ya picha na vitabu vinavyoweza kutazamwa na kusomwa kwa kutumia kompyuta.

Maktaba hiyo ya Ufaransa ina rafu zinazoweza kutoshea vitabu vipya kwa miaka 50 ijayo. Jitihada ambayo imekuwapo ili kujenga na kuhifadhi nyumba hiyo iliyo na vitabu vingi vya elimu ni jambo linalovutia sana!

[Picha katika ukurasa wa 24]

Chumba cha kusomea cha mwaka wa 1868

[Hisani]

© Cliché Bibliothèque nationale de France, Paris

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 25]

©Alain Goustard/BNF. Mchoraji: Dominique Perrault. © 2002 Artists Rights Society (ARS), New York/ADAGP, Paris