Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Maji Huenda Wapi?

Maji Huenda Wapi?

Maji Huenda Wapi?

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI AUSTRALIA

NILISHTUKA! Maji yenye kunuka yenye rangi ya kijivu yalikuwa yakibubujika kwenye shimo la kuondoshea maji machafu katika bafu langu na kuenea ndani ya nyumba. Nilimwita fundi mara moja. Nilipokuwa nikisubiri nikiwa na wasiwasi mwingi, huku mdomo wangu ukiwa umekauka na soksi zangu zikizidi kulowa, nilijiuliza hivi, ‘Maji hayo yote yametoka wapi?’

Fundi alipokuwa akizibua bomba la maji machafu, alinieleza hivi: “Kila siku, mkazi mmoja wa jiji hutumia lita 200 hadi 400 za maji. Kila mwaka, kila mwanamume, mwanamke, na mtoto hutumia karibu lita 100,000 za maji.” Nikamwuliza fundi huyo hivi: “Je, kweli ninaweza kutumia maji mengi hivyo? Mimi sinywi maji mengi hivyo!” Fundi akasema, “Ni kweli, lakini kila siku wewe huoga mwili, huvuta maji msalani, na labda hutumia mashine ya kuosha nguo au vyombo. Kwa njia hizo na nyinginezo, maisha ya sasa yanatufanya tutumie kiasi cha maji ambacho ni mara mbili ya kile kilichotumiwa na babu na nyanya zetu.” Kisha nikajiuliza hivi kwa ghafula, ‘Maji yote hayo huenda wapi?’

Niligundua kwamba maji yaliyokwisha kutumiwa hushughulikiwa kwa njia tofauti katika nchi au majiji mbalimbali. Katika nchi fulani maji hayo ni muhimu sana. (Ona masanduku kwenye ukurasa wa 27.) Ungana nami ninapotembelea mtambo wa kusafisha maji machafu katika eneo letu na ujionee mahali ambapo maji hayo huenda na kwa nini ni muhimu kuwa mwangalifu kabla ya kutupa vitu ndani ya sinki au msalani ili vipelekwe na maji, hata iwe unaishi wapi.

Kutembelea Mtambo wa Kusafisha Maji Machafu

Ninajua kuwa kutembelea mtambo wa kusafisha maji machafu si jambo linaloonekana kuwa lenye kupendeza sana. Hata hivyo, wengi wetu hutegemea mtambo kama huo ambao unazuia jiji letu lisifunikwe na maji machafu—na sote tunatimiza daraka fulani kuwezesha mitambo hiyo iendelee kufanya kazi ipasavyo. Tunaelekea kwenye mtambo mkuu wa kusafisha maji machafu huko Malabar, kusini ya Bandari maarufu ya Sydney. Maji ya bafu langu hufikaje kwenye mtambo huo?

Ninapovuta maji msalani, ninapotumia sinki, au ninapooga, maji hayo huenda kwenye mtambo wa kusafisha maji machafu. Baada ya kusafiri kilometa 50, maji hayo huchangamana na lita milioni 480 za maji zinazoingia katika mtambo huo kila siku. Kiasi cha maji kinachoingia katika mtambo huo kila dakika kinalingana na kiasi cha maji kinachohitajiwa kujaza vidimbwi viwili vya kuogelea vya michezo ya Olimpiki.

Ross, afisa wa mtambo huo anayeshughulikia uhusiano pamoja na jamii, alinieleza ni kwa nini mtambo huo hauna takataka zenye kuchukiza wala uvundo mkali. Alisema hivi: “Sehemu kubwa ya mtambo huo iko chini ya ardhi. Hiyo hutuwezesha kunasa gesi na kuzipeleka kwenye mitambo ya kusafisha hewa (mabomba makubwa ya kutoa moshi), ambayo huondoa uvundo. Kisha hewa iliyosafishwa huachwa ienee angani. Ijapokuwa kuna maelfu ya nyumba kandokando ya mtambo huo, kila mwaka mimi hupigiwa karibu simu kumi tu kutoka kwa watu wanaolalamika kuhusu uvundo.” Ross sasa anatupeleka mahali ambapo “uvundo” huo hutoka.

Maji Machafu

Tunapoteremka chini kwenye mtambo huo, yule anayetutembeza anatuambia hivi: “Maji machafu hufanyizwa kwa asilimia 99.9 ya maji pamoja na kinyesi, kemikali, na vitu vingine vidogo. Maji machafu yanayotoka kwenye nyumba na viwanda vilivyo kwenye eneo la eka 130,000 hupitia kwenye mabomba yenye urefu wa kilometa 20,000 na kuingia ndani ya mtambo huo meta mbili chini ya usawa wa bahari. Maji yanapoingia mtamboni yanapitishwa kwenye machujio mbalimbali ambako vitambaa, mawe, karatasi, na plastiki huondolewa. Kisha, katika vyumba vinavyofuata, mapovu hufanya uchafu unaoweza kuoza uelee majini na mchanga na vijiwe huzama chini polepole. Uchafu wote huo usioweza kuoza hukusanywa na kupelekwa kwenye sehemu ya takataka. Maji machafu yanayosalia husukumwa meta 15 kwa pampu hadi juu kwenye matangi ambako uchafu unaobaki huzama.”

Matangi hayo ni makubwa kama uwanja wa mpira. Unapokuwa kwenye matangi hayo, unatambua kwamba majirani wangelalamika sana kuhusu uvundo iwapo mfumo wa kusafisha hewa haungefanya kazi ipasavyo. Maji yanapoingia ndani ya matangi hayo polepole, mafuta huelea na kuondolewa. Vipande vidogo vya uchafu huzama, na mashine fulani kubwa huondoa uchafu na kuupeleka mahali ambapo unasukumwa kwa pampu ili kusafishwa zaidi.

Maji yaliyosafishwa huelekea baharini kupitia mfereji wa chini ya ardhi wenye urefu wa kilometa tatu. Maji hayo yanapotoka kwenye mfereji chini ya bahari yanachangamana na maji ya bahari, meta 60 hadi meta 80 chini ya mawimbi. Mikondo yenye nguvu hutawanya maji hayo, na maji ya chumvi ya baharini huua vijidudu vinavyobaki. Uchafu uliosalia kwenye mtambo wa kusafisha maji husukumwa kwa pampu hadi kwenye matangi makubwa, ambako vijidudu fulani hugeuza uchafu unaoweza kuoza kuwa gesi ya methani na kuufanya usibadilike tena.

Uchafu Huo Wageuzwa Kuwa Udongo

Ninafurahi sana ninapomfuata Ross tunaporudi juu ili kupata hewa safi, na tunapanda tangi moja lenye uchafu uliosalia ambalo limefunikwa ili hewa isiingie. Ross anaendelea kusema hivi: “Gesi ya methani inayofanyizwa na vijidudu hivyo hutumiwa kuendesha jenereta za umeme na hutoa zaidi ya asilimia 60 ya nguvu zinazotumiwa kuendesha mtambo huu. Uchafu uliosalia husafishwa kabisa, na kuchanganywa na chokaa ili utumiwe kama mbolea. Mbolea hiyo ina virutubisho tele. Kila mwaka, Mtambo wa Kusafisha Maji Machafu huko Malabar hutengeneza tani 40,000 za mbolea hiyo. Miaka kumi iliyopita uchafu huo ulikuwa ukiteketezwa au kumwagwa baharini; sasa uchafu huo unatumiwa kuleta faida.”

Ross ananipa kijitabu kinachosema hivi: “Misitu ya [New South Wales] imesitawi zaidi kwa asilimia 20 hadi 35 baada ya mbolea hiyo kutumiwa.” Pia, kijitabu hicho kinasema kwamba kupanda ‘ngano katika udongo wenye mbolea hiyo kumeongeza mazao ya ngano kufikia asilimia 70.’ Ninatambua kwamba mbolea hiyo si hatari na hivyo ninaweza kuitumia ili kukuza maua ya bustani yangu.

Mtu Hukumbuka Alichofanya

Baada ya kuzunguka mtambo huo, mtu aliyetutembeza ananikumbusha kwamba kumwaga rangi, kemikali za kuua wadudu waharibifu, dawa, au mafuta katika bomba la maji machafu kunaweza kuua vijidudu vilivyo kwenye mtambo huo na kuvuruga utaratibu wa kusafisha maji. Anakazia kwamba ‘mafuta huziba mabomba pole kwa pole kama vile yanavyoziba mishipa yetu na kwamba haifai kutupa nepi, vitambaa, na plastiki msalani. Badala yake, vitu hivyo huziba mabomba hayo.’ Nimejifunza kwamba, mtu anaweza kuondosha takataka kwa kuzitupa msalani na kuvuta maji, lakini takataka hizo zinapozuia maji yasipite, ndipo mtu anapojutia kitendo chake. Basi, utakapokuwa ukioga, ukivuta maji msalani, au kutumia sinki, fikiria mahali ambapo maji hayo huenda.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 25]

Maji Machafu Yawa Maji ya Kunywa

Mamilioni ya wakazi wa Mkoa wa Orange—eneo la California, Marekani, ambalo hupata mvua chache—hufaidika na mbinu mpya ya kusafisha maji machafu. Badala ya mamilioni ya lita za maji machafu kusukumwa kila siku hadi baharini, kiasi kikubwa cha maji hayo hurudishwa kwenye hifadhi ya maji. Kwa miaka mingi, mtambo fulani wa kusafisha maji machafu ndio umewezesha jambo hilo. Maji machafu yakiisha kusafishwa kwa mara ya kwanza, yanasafishwa mara ya pili na mara ya tatu. Hiyo inatia ndani kusafisha maji hayo ili yawe safi kama maji ya kunywa. Kisha maji hayo huchanganywa na maji ya kisima na kuingia chini ya ardhi. Maji hayo huongeza kiasi cha maji yaliyomo chini ya ardhi na kuzuia chumvi isiingie humo kuchafua maji hayo. Asilimia 75 ya maji yanayotumiwa katika eneo hilo hutoka kwenye kisima hicho cha chini ya ardhi.

[Sanduku katika ukurasa wa 27]

Njia Tano za Kutumia Maji kwa Busara

▪ Rekebisha mifereji yenye kasoro—mfereji unaovuja maji unaweza kuvuja lita 7,000 kwa mwaka.

▪ Hakikisha kwamba msala wako hauvuji maji—unaweza kuvuja lita 16,000 kwa mwaka.

▪ Tumia mfereji wa kuoga unaomimina maji machache. Kwa kawaida mfereji wa kumimina maji hutoa lita 18 za maji kila dakika; mfereji unaomimina maji machache hutoa lita 9 kila dakika. Kwa kutumia mfereji huo, familia ya watu wanne itahifadhi lita 80,000 za maji kila mwaka.

▪ Iwapo msala wako huvuta maji mara mbili, urekebishe ili uvute maji mara moja wakati inapowezekana—familia ya watu wanne inapofanya hivyo itahifadhi lita 36,000 za maji kila mwaka.

▪ Weka kifaa kinachoingiza hewa katika maji yanayotoka miferejini. Kifaa hicho si bei ghali na hupunguza kiasi cha maji kinachotoka kwa asilimia 50.

[Sanduku katika ukurasa wa 27]

Tatizo la Maji Machafu Ulimwenguni

“Zaidi ya watu bilioni 1.2 hawapati maji safi ya kunywa na watu bilioni 2.9 wanaishi katika maeneo yasiyo na mfumo mzuri wa kuondoa takataka na maji machafu. Hilo husababisha vifo vya watu milioni 5 kila mwaka, hasa watoto, kutokana na magonjwa yanayosababishwa na maji machafu.”—Mkutano wa Pili Kuhusu Maji Ulimwenguni ambao ulifanywa huko Hague, Uholanzi.

[Mchoro/Picha katika ukurasa wa 26]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Jinsi Maji Machafu Yanavyosafishwa Huko Malabar (Mchoro rahisi)

1. Maji machafu yanaingia mtamboni

2. Kuchuja maji

3. Vyumba ambamo mchanga na vijiwe huondolewa

4. Kupelekwa kwenye sehemu ya takataka

5. Matangi ambamo uchafu huzama

6. Yanaelekea baharini

7. Matangi ambamo gesi hufanyizwa

8. Jenereta za umeme

9. Tangi la kuhifadhi mbolea

[Picha]

Katika matangi haya, vijidudu hufanyiza mbolea na gesi ya methani kutokana na uchafu

Gesi ya methani hutumiwa kuzalisha umeme