Vyombo vya Angani Vyenye Kusisimua
Vyombo vya Angani Vyenye Kusisimua
“BABA yangu alifanya kazi katika mfumo wa mawasiliano katika chombo cha angani cha Zeppelin, na aliipenda sana kazi yake,” Ingeborg Waldorf alimwambia mwandishi wa Amkeni! Mapema katika miaka ya 1900, watu wengi ulimwenguni walivutiwa sana na vyombo hivyo vikubwa ajabu. Popote ambapo vyombo hivyo vilienda, vilivutia watu sana.
Vyombo hivyo vilitumiwa mapema katika miaka ya 1900. Mafanikio ya kurusha vyombo hivyo angani yalivifanya viwe maarufu ulimwenguni pote—ingawa safari hizo zilikumbwa na mikasa mikubwa. Vyombo hivyo vilitokomea ghafla katika mwaka wa 1937 wakati chombo kimoja kilichoitwa Hindenburg kilipoanguka huko Lakehurst, New Jersey, Marekani. Hata hivyo, historia ya vyombo hivyo inasisimua sana.
Toka Maputo ya Hewa Moto Hadi Vyombo vya Angani
Kwa karne nyingi wavumbuzi walijaribu kutafuta jinsi ambavyo wanadamu wangeruka angani. Katika miaka ya 1700 Wafaransa Joseph-Michel na Jacques-Étienne Montgolfier waliona moshi ukipaa na kutambua kwamba ulikuwa na nguvu fulani ambazo huenda wanadamu wangetumia kuruka angani. Kwa hiyo, walitengeneza mfuko mkubwa wa karatasi na kitambaa na kuushikilia juu ya moto wenye moshi mwingi. Wanakijiji waliomiminika hapo walipigwa na butwaa mfuko huo ulipopaa. Ndugu hao wawili walifanya uvumbuzi huo wa puto la hewa moto mnamo Juni 1783. Miezi mitano baadaye, mwanadamu aliruka kwa mara ya kwanza akitumia puto la hewa moto la Montgolfier.
Hata hivyo, maputo yalipeperushwa na upepo na hayangeweza kuelekezwa upande fulani hususa. Yalihitaji njia ya kuyaelekeza. Katika mwaka wa 1852, Mfaransa Henri Giffard alikuwa mtu wa kwanza kuelekeza chombo angani, aliporuka katika chombo kilichotumia mvuke. Badala ya kutumia hewa moto, Giffard alitumia haidrojeni, ambayo ni nyepesi kuliko hewa.
Karibu miaka kumi baadaye, mwanajeshi mmoja Mjerumani alienda Amerika Kaskazini kujionea ile Vita ya Wenyewe kwa Wenyewe, ambapo puto zilitumiwa na pande zote mbili za vita kupeleleza eneo la adui. Puto la kwanza alilosafiria juu sana ya Mto Mississippi lilimvutia sana hivi kwamba alikuja kuwa mtu maarufu kuhusiana na vyombo vya angani. Mtu huyo aliitwa Ferdinand von Zeppelin.
Vyombo Vikubwa vya Angani vya Zeppelin
Kulingana na vyanzo fulani vya habari, Zeppelin aliunda chombo kikubwa cha angani kwa alumini akitumia mchoro wa mvumbuzi Mkroatia David Schwarz. Zeppelin alitamani sana kuunda chombo kikubwa ambacho kingeweza kubeba abiria wengi au mizigo mizito. Aliunda vyombo vikubwa ajabu vyenye muundo wa mcheduara. Vyombo vya Zeppelin vilikuwa na nguzo za vyuma ambazo zilifunikwa kwa kitambaa. * Ndani au chini ya nguzo kulikuwa na behewa la marubani. Abiria walikaa katika behewa la marubani au katika behewa lingine la ndani. Haidrojeni iliyokuwa katika mitungi karibu na nguzo ilitumiwa kurusha chombo hicho angani. Mota zilizofungwa kwenye nguzo zilielekeza chombo hicho. Zeppelin alipokifanyia chombo chake majaribio, watu walimwona kuwa mjinga sana. Lakini alifanikiwa hatimaye.
Zeppelin aliacha utumishi wa kijeshi ili afanye kazi ya kubuni na kuunda vyombo vya angani.
Chombo chake cha kwanza kiliruka kwa mara ya kwanza mnamo Julai 1900, karibu na Friedrichshafen, Ujerumani. Watu walijipanga kandokando ya Ziwa Constance ili kutazama chombo hicho chenye urefu wa meta 127 kikivuka ziwa hilo kwa dakika 18. Kampuni ya kutengeneza vyombo vya angani ilianzishwa na vyombo zaidi vikaundwa. Zeppelin hakuonwa tena kuwa mjinga; bali sasa alikuwa mtu mashuhuri duniani. Kiongozi wa Ujerumani alimtaja kuwa Mjerumani mashuhuri zaidi katika miaka ya 1900.Chombo cha Kwanza cha Kusafirishia Abiria Angani
Zeppelin aliona uvumbuzi wake wa vyombo vikubwa vya angani kuwa njia ya kuipatia Ujerumani umaarufu katika anga. Katika Vita ya Kwanza ya Ulimwengu, majeshi ya Ujerumani yalitumia vyombo vya Zeppelin kupeleleza eneo la adui na hata kushambulia kwa mabomu. Shambulizi baya zaidi la angani huko London lilifanywa kwa kutumia chombo hicho.
Hata hivyo, watu wengine waliona inawezekana kuwasafirisha abiria angani. Katika mwaka wa 1909, kampuni ya kwanza ulimwenguni ya kuwasafirisha abiria angani ilianzishwa, nayo iliitwa Shirika la Ujerumani la Uchukuzi wa Anga. Katika miaka ya baadaye, huduma hiyo ilienea mpaka nje ya Ulaya. Vyombo kama Graf Zeppelin na Hindenburg vilisafiri kwenda na kurudi kutoka Ujerumani hadi Rio de Janeiro na vilevile Lakehurst.
Watu wa Marekani walipenda sana vyombo vya Zeppelin. Baada ya chombo cha Graf Zeppelin kuvuka Bahari ya Atlantiki mara ya kwanza kutoka Friedrichshafen kikielekea Pwani ya Mashariki ya Marekani katika mwaka wa 1928—mwaka ambapo kiliharibika—Rais Coolidge alikimbia kwenye uwanja wa ikulu ya White House kukitazama. Watu wa New York walisisimuliwa sana na chombo hicho hivi kwamba walipanga gwaride ya heshima kwa ajili ya wafanyakazi wake.
Kusafiri kwa Chombo cha Hindenburg
Kusafiri katika vyombo hivyo kulikuwa tofauti na kusafiri katika ndege za kisasa. Wazia ukiingia katika chombo cha Hindenburg ambacho urefu wake ulikuwa mara tatu zaidi ya ndege kubwa na kimo chake kilikuwa kama jengo la orofa 13. Badala ya viti vya abiria, ungepewa chumba kilichokuwa na kitanda, choo na bafu. Hakukuwa na haja ya kufunga mkanda wa usalama wakati chombo kilipoanza safari. Badala yake, ungepumzika chumbani au hata kutembea-tembea sebuleni, ukitazama nje kupitia madirisha ambayo yangeweza kufunguliwa. Huduma zote za abiria zilipatikana katika chombo.
Kulingana na kitabu Hindenburg—An Illustrated History, abiria 50 waliketi katika chumba cha kulia kilichokuwa na meza zilizopambwa kwa vitambaa vyeupe na vyombo vya fedha na kauri. Katika safari ya kawaida ya kuvuka Bahari ya Atlantiki, wapishi walitumia kilogramu 200 za nyama ya ng’ombe na ya kuku, mayai 800, na kilogramu 100 za siagi. Kulikuwa na meko za umeme, joko, mashine ya kutengeneza madonge ya barafu, na friji. Piano kubwa ilitumiwa kuwatumbuiza abiria sebuleni, ambapo mhudumu aliwahudumia abiria.
Chombo cha Hindenburg kilistarehesha sana, lakini hakikuenda kwa kasi. Mnamo mwaka wa 1936, chombo hicho kilisafiri mwendo wa kasi zaidi wa kilometa 130 kwa saa kikiwa meta 200 kutoka ardhini na kuvuka Bahari ya Atlantiki Kaskazini kwa saa 43. Kwa kawaida, safari hiyo ilikuwa yenye kustarehesha sana. Wakati wa safari moja kutoka Lakehurst, mwanamke aliyekuwa amechoka sana aliingia chomboni, na kulala
chumbani mwake. Baadaye alimwita mhudumu mmoja wa chombo na kumwuliza kwa nini chombo hakikuwa kimeanza safari. Kwa mshangao, mhudumu alimwambia kwamba walikuwa wameanza kusafiri saa mbili mapema. “Sikuamini,” mwanamke huyo akafoka. Aliamini tu alipoenda sebuleni na kutazama dirishani, na kuona pwani ya New England mamia ya meta chini.Vyombo Maarufu Zaidi vya Angani
Safari za vyombo hivyo vya angani ilifikia kilele mwaka wa 1929 wakati Graf Zeppelin ilipozunguka ulimwengu. Safari hiyo ilichukua siku 21 kutoka magharibi hadi mashariki. Ilianza rasmi huko Lakehurst, kisha chombo hicho kikatua huko Friedrichshafen, kisha kikatua Tokyo—ambako watu 250,000 walienda kukikaribisha—halafu kikaenda San Francisco na Los Angeles. Miaka miwili baadaye chombo hicho kiliweka rekodi nyingine wakati kiliposafiri hadi eneo la Aktiki ambapo kilikutana na meli ya Urusi. Kitabu Hindenburg—An Illustrated History kinasema: “Kufikia wakati huo chombo cha Graf Zeppelin kilikuwa kimepata umaarufu mwingi sana. Popote kilipoenda watu walisisimuka. Tunaweza kusema kwamba hicho ndicho chombo maarufu zaidi kuwahi kusafiri angani—hata zaidi ya ndege aina ya Concorde ya kisasa.”
Mataifa mengine pia yalitazamia kutengeneza vyombo thabiti vya angani. Uingereza ilipanga kuwa na vyombo vingi vya angani ambavyo vingerahisisha usafiri katika makoloni yake yaliyokuwa katika maeneo mbalimbali kama India na Australia. Nchini Marekani, chombo kilichoitwa Shenandoah kilikuwa cha kwanza kutumia gesi ya heli kuruka badala ya haidrojeni ambayo hushika moto kwa urahisi. Vyombo kama Akron na Macon vilikuwa na uwezo wa kupakia na kurusha ndege ndogo ambazo ziliwekwa katika sehemu ya kati ya chombo. Kwa kuwa kilikuwa na vifaa maalumu, chombo cha Macon kilikuwa cha kwanza kutumiwa kubeba ndege.
Maafa Makubwa
“Naam, baba yangu alipenda safari za angani,” asema Ingeborg Waldorf aliyetajwa mwanzoni. “Lakini aliogopa hatari zake.” Baba yake alisafiri angani wakati wa Vita ya Kwanza ya Ulimwengu, lakini hata wakati wa amani, kusafiri katika chombo cha angani kulikuwa hatari sana licha ya maendeleo yaliyokuwa yamefanywa. Kwa nini?
Hatari kubwa ya Zeppelin ilitokana na
mabadiliko ya hali ya hewa. Kati ya vyombo 24 vya kwanza vilivyoundwa na Zeppelin na kampuni yake, 8 viliharibiwa na hali mbaya ya hewa. Mnamo mwaka wa 1925, chombo cha Marekani kilichoitwa Shenandoah, kilipasuliwa mara mbili na pepo kali kilipokuwa safarini. Hatimaye, Wamarekani waliacha kutumia vyombo thabiti vya angani mwaka wa 1933 wakati chombo cha Akron kilipoanguka na kabla ya miaka miwili kuisha, chombo kingine kiitwacho Macon kikaanguka.Uingereza iliweka matumaini yake katika chombo kilichoitwa R 101. Kwenye safari yake ya kwanza kutoka Uingereza hadi India mnamo mwaka wa 1930, chombo hicho kilifika tu Ufaransa, ambako kilikabili hali mbaya ya hewa na kuanguka. Mwandishi mmoja aripoti kwamba “hakuna maafa yaliyowashtua Waingereza kama hayo tangu kuzama kwa meli ya Titanic katika mwaka wa 1912.” Umaarufu wa vyombo vya angani nchini Uingereza ulikoma.
Hata hivyo, Wajerumani bado walitumaini vyombo hivyo. Ndipo kukawa na msiba uliowashtua watu ulimwenguni pote. Mnamo Mei 1937, chombo cha Hindenburg kilianza safari yake kutoka Frankfurt kuelekea New Jersey. Ghafula, kilipokuwa kikijaribu kutua katika Kituo cha Angani cha Majeshi huko Lakehurst, moto ulionekana ukiwaka upande wa nyuma. Gesi ya haidrojeni iliyokuwa kwenye mitungi ilishika moto na chombo chote kikawaka kama tanuru. Watu 36 walikufa.
Kwa mara ya kwanza, wapiga-picha wa habari walikuwapo kurekodi tukio hilo wakati lilipotokea. Picha za habari kuhusu msiba huo uliochukua sekunde 34—kuanzia wakati moto ulipoonekana hadi chombo kilipoanguka—zilionyeshwa ulimwenguni kote, huku sauti ya msomaji wa habari hiyo iliyojawa na majonzi ilisikika ikisema: “Chombo kinateketea, kinateketea kabisa . . . Ole kwa wanadamu na abiria wote!” Chombo hicho kilisafiri kwa miaka 30 lakini kilifikia mwisho wake kwa sekunde 34.
Aina Mpya ya Vyombo vya Angani
Mji wa Friedrichshafen haujaacha kusisimukia vyombo vya angani. Jumba la Makumbusho la Vyombo vya Zeppelin huwaonyesha wageni vyombo vya zamani, likiwapa fursa ya kuingia ndani ya sehemu ya Hindenburg iliyorekebishwa. Mwelekezi mmoja katika jumba hilo la makumbusho, ambaye aliona chombo halisi cha Hindenburg katika michezo ya Olimpiki ya Berlin mwaka wa 1936, alimwambia mwandishi wa Amkeni! hivi: “Ni vigumu kuelezea jinsi mtu alivyohisi alipoona chombo cha Zeppelin. Ilistaajabisha sana.”
Inasemekana kwamba aina mpya za vyombo vya angani vinaundwa sasa hivi kwa kutumia ufundi wa kisasa. Vyombo hivyo ni vidogo kuliko vile vya kale na vinakusudiwa vitumiwe na “watu wachache, wanaopenda kutalii katika hali tulivu.” Je, vyombo hivyo vitafikia umaarufu wa vile vya zamani? Tutaona itakavyokuwa.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 9 Chombo hicho kiliitwa Zeppelin au chombo thabiti kwa sababu kilikuwa na nguzo za kukitegemeza. Chombo kisicho thabiti hakikuwa na nguzo zozote bali kilikuwa puto tu lililojaa gesi. Chombo cha tatu kilifanana na chombo kisicho thabiti lakini kilikuwa na nguzo upande wa chini. Tofauti na puto, vyombo hivyo viliendeshwa kwa mota.
[Picha katika ukurasa wa 10]
Ferdinand von Zeppelin
[Hisani]
Photos on page 10: Archiv der Luftschiffbau Zeppelin GmbH
[Picha katika ukurasa wa 11]
Ndege aina ya Boeing 747
“Hindenburg”
“Titanic”
[Picha katika ukurasa wa 12, 13]
Kushoto hadi kulia: “Graf Zeppelin” katika anga ya Philadelphia; chumba cha kuelekeza chombo; sebule
[Hisani]
Archiv der Luftschiffbau Zeppelin GmbH
[Picha katika ukurasa wa 14]
Msiba uliokipata “Hindenburg” katika mwaka wa 1937 huko Lakehurst ulichangia kukomesha vyombo vya angani
[Hisani]
Photos: Brown Brothers