Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Misitu ya Mvua Je, Inaweza Kuokolewa?

Misitu ya Mvua Je, Inaweza Kuokolewa?

Misitu ya Mvua Je, Inaweza Kuokolewa?

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI BOLIVIA

RAMIRO ana bonde lililojaa msitu wa mvua. * Bonde hilo liko chini ya Milima ya Andes, huko Amerika ya Kusini na ni mojawapo ya mabonde machache yenye miti ya kale sana katika eneo hilo. Katika eneo hilo lote, milima haina misitu. Wanasayansi kutoka nchi za mbali huja kuchunguza wanyama wa pori katika msitu wa Ramiro, na wamegundua jamii kadhaa ambazo hazijawahi kuonekana. Ramiro anapenda sana kuhifadhi misitu. Anasema: “Sitaruhusu miti ikatwe kwenye msitu wangu.”

Naye Roberto anatunza msitu wa mvua wenye ukubwa wa kilometa 5,600 za mraba kwenye nyanda za chini za bonde la Amazoni. Yeye ni mtunzaji stadi wa misitu naye hukata miti na kuuza mbao za misitu ya mvua katika nchi mbalimbali. Lakini pia Roberto anapenda sana kulinda misitu ya mvua na wanyama wa pori waliomo. “Miti ya misitu ya mvua inaweza kukatwa bila kuangamiza kabisa mimea na wanyama mbalimbali,” anasisitiza.

Ingawa hali zao zatofautiana, Ramiro na Roberto wanahangaishwa sana na uharibifu wa misitu ya mvua. Na bila shaka si wao peke yao wanaohangaishwa na jambo hilo. Katika miaka ya karibuni misitu ya mvua imekuwa ikikatwa ovyoovyo.

Je, hangaiko hilo limepita kiasi? Kwa kweli, watu wameharibu misitu mingi kwenye nchi zenye joto la wastani katika karne zilizopita, hasa kwa ajili ya kilimo. Basi, kwa nini tuhangaike tukiona watu wakifanya vivyo hivyo katika nchi zenye joto? Kuna tofauti kubwa. Kwa mfano, mara nyingi misitu ya mvua hukua kwenye ardhi isiyo na rutuba ambayo haifai kilimo. Pia, kuna viumbe na mimea mingi sana katika misitu ya mvua, na uharibifu wa misitu hiyo huwaathiri wanadamu wote.

Hasara ya Kuharibu Misitu

Zaidi ya nusu ya viumbe wote ulimwenguni hupatikana katika misitu ya mvua. Kuanzia tumbili wadogo na simba-marara hadi kuvumwani zisizo za kawaida na okidi, kuanzia nyoka na vyura hadi vipepeo na kasuku wasiopatikana kwa urahisi. Idadi ya viumbe ni kubwa sana isiweze kuhesabiwa.

Viumbe tofauti-tofauti husitawi katika misitu mbalimbali ya mvua. Kuna misitu ya mvua inayokua polepole milimani, misitu ya mvua yenye giza na majani mengi, misitu ya mvua inayokua katika maeneo yenye majira marefu ya kiangazi, na misitu ya mvua yenye nafasi kubwa. Hata hivyo, watu wengi hawajawahi kufika kwenye msitu wa mvua. Labda wewe pia hujafika kwenye msitu huo. Basi, kwa nini uhangaikie maeneo hayo?

Kuhifadhiwa kwa misitu ya mvua ni muhimu kwako kwa sababu mimea mingi ya chakula na ya biashara ambayo unategemea, kwa njia fulani hutokana na mimea inayokua yenyewe ambayo bado inasitawi kwenye misitu hiyo. Nyakati nyingine mimea hiyo hutumiwa kuzalisha mimea mipya ambayo ina uwezo zaidi wa kukinza magonjwa na wadudu-waharibifu. Kwa hiyo chembe za urithi zinazopatikana katika aina mbalimbali za mimea hiyo ni muhimu.

Pia watafiti wanatengeneza bidhaa muhimu kutokana na misitu ya mvua. Kwa mfano, kiasi kikubwa cha dawa tunazotumia sasa zilitengenezwa kutokana na mimea ya misitu ya mvua. Kwa hiyo, aina mbalimbali za mimea na wanyama katika misitu ya mvua mara nyingi zinaitwa maktaba iliyo hai ambayo ina “vitabu” vingi ambavyo havijafunguliwa bado.

Mimea na Viumbe Wanaoweza Kuangamia kwa Urahisi

Mazingira yenye unyevunyevu ya misitu ya mvua yanaweza kuharibiwa kwa urahisi na ni tata sana. Idadi kubwa sana ya mimea na viumbe wanategemeana. Kwa mfano, mimea mingi hutegemea ndege, wadudu, au wanyama hususa kwa ajili ya uchavushaji na usambazaji wa mbegu. Misitu hutumia ifaavyo vitu vyote hai vilivyomo kutia ndani mimea, wanyama, wadudu, na vijidudu vidogo kupitia kwa mzunguko tata wa maisha. Jambo la kushangaza ni kwamba mfumo huo wote tata kwa kawaida huwa kwenye udongo usio na rutuba. Ukishaharibiwa, huenda ikawa vigumu au huenda isiwezekane kwa msitu kama huo kusitawi tena.

Watu wengi hujiruzuku kutokana na misitu ya mvua. Mbali na utafiti wa kisayansi na utalii, misitu ya mvua ni muhimu kiuchumi kwa ajili ya bidhaa kama mbao, kokwa, asali, mashina ya mchikichi, mpira, na utomvu. Lakini misitu ya mvua inatoweka haraka sana. Idadi hususa haijulikani lakini jambo moja ni hakika: Misitu hiyo inapungua haraka.

Hasara hiyo ya kimazingira inahuzunisha sana hasa kwa sababu mara nyingi misitu ya mvua inaharibiwa bila sababu nzuri. Misitu mingi imeharibiwa ili kupata sehemu za kulisha ng’ombe. Lakini mara nyingi mimea hushindwa kukua kwenye sehemu hizo na hivyo zinaachwa tu. Imeripotiwa kwamba huko Amazonia, Brazili, ardhi yenye ukubwa wa kilometa 165,000 za mraba imeachwa kwa sababu hiyo.

Je, misitu ya mvua na wanyama-pori waliojaa humo wataokolewa? Ramiro, Roberto, na watu wengine wengi wanajitahidi kulinda misitu ya mvua isiharibiwe na biashara ya ulimwenguni pote, ongezeko kubwa la watu, wauzaji wa wanyama-vipenzi, wakataji-miti na wawindaji haramu. Lakini visababishi vikuu vya uharibifu wa misitu ni vipi? Je, kuna njia yoyote ya kutumia rasilimali nyingi za misitu ya mvua bila kuiharibu?

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 3 Msitu wa mvua unaopatikana milimani hukua kwenye kimo cha zaidi ya meta 1,000.

[Blabu katika ukurasa wa 3]

Jamii nyingi za wanyama ulimwenguni hupatikana katika misitu ya mvua, pamoja na aina nyingi sana za mimea

[Picha katika ukurasa wa 4, 5]

Wakataji-miti na barabara wanazotengeneza zinaweza kuharibu misitu ya mvua