Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Siku Ambayo Msitu wa Jiji Kuu Uliteketea

Siku Ambayo Msitu wa Jiji Kuu Uliteketea

Siku Ambayo Msitu wa Jiji Kuu Uliteketea

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI AUSTRALIA

MNAMO Januari 18, 2003, wakazi wa Canberra, jiji kuu la Australia, waliamka na kuona moto mkubwa wenye kuogopesha. Moshi mzito ulifanya jua la asubuhi liwe jekundu kama damu. Kulikuwa na joto jingi lenye kuumiza. Nchi ya Australia ilikuwa imekumbwa na ukame uliofanya miti, majani, na vichaka vidogo vikauke kama ngozi ngumu. Kwa majuma kadhaa, moto ulikuwa umeharibu misitu ya mikalitusi iliyozunguka jiji hilo, linaloitwa Jiji Kuu la Msituni.

Alasiri hiyo, pepo kali zenye joto zilisababisha mkasa. Moto ulivuka maeneo yasiyokuwa na miti, ukasambaa hadi kwenye misitu ya misonobari iliyokuwa kusini-magharibi mwa Canberra.

Msitu Wateketea

Elliot, mzimamoto wa kujitolea, anasema: “Moto mkali sana ulilipuka katika misitu ya misonobari saa tisa alasiri, kiasi cha kwamba majivu ya moto yakafika katika eneo letu na maeneo mengine ya karibu. Ilishtua sana kuona mwale wa moto wenye urefu wa meta 40 ukisonga haraka kutuelekea.” Joto jingi na pepo kali zilisababisha moto mkali uliosambaa haraka katika eneo la Chapman na kung’oa miti na kuharibu nyumba. Nguzo nyingi za umeme ziliungua, zikavunjika, na kuangusha nyaya zenye umeme. Baada ya saa moja, nyumba 230 zilikuwa zimeteketea.

Vikosi vya wazimamoto vililemewa sana na moto huo mkubwa. Elliot anasema: “Ilihuzunisha kuona nyumba zikiteketea kwani ilitubidi kuchagua nyumba ambazo tungeokoa na zile ambazo tungeacha ziungue. Ilihuzunisha hata zaidi kuona watu wakilia kwa huzuni huku wakirudi kwenye nyumba zao zilizoteketea.”

Matokeo

Watu wanne walikufa kutokana na moto huo na mamia wakajeruhiwa. Mwanamke mmoja mwenye umri wa miaka 36 alirudi ndani ya nyumba yake ili kuokoa picha. Paa la nyumba liliporomoka na hivyo hangeweza kuokolewa.

Pepo hizo na moto huo ulipodidimia, nyumba 530 zilikuwa zimeharibiwa na watu 2,500 wakaachwa bila makao. Mifumo ya umeme, ya gesi, na ya kuondoa maji machafu iliharibiwa sana, na kusababisha hatari za kiafya. Watu wengi wenye magonjwa ya kupumua walienda kwenye kituo cha dharura cha Hospitali ya Canberra. Inasikitisha kwamba watu walipoenda kwenye vituo vya msaada, wahalifu wasio na huruma walipora nyumba zao. Hata hivyo, watu wengi walifanya matendo ya ujasiri na yenye fadhili. Majirani walisaidiana, wengine waliokoa wanyama wa watu wasiowajua, shule ziliwapa makazi watu wasio na makao, na watu wakajitolea kuzima moto kwenye nyumba za wengine huku nyumba zao zikiteketea.

Ijapokuwa baada ya muda miti itakua na nyumba zitajengwa tena, Waziri Mkuu John Howard alisema kwamba uharibifu uliosababishwa na moto huo “hautasahauliwa . . . na wakazi wa Canberra.”

[Maelezo ya Picha katika ukurasa wa 25 zimeandaliwa na]

AP Photo/Fairfax, Pat Scala