Vitu vya Asili Vinatufundisha Nini?
Vitu vya Asili Vinatufundisha Nini?
“Tafadhali uliza wanyama wa kufugwa, nao watakufundisha; pia viumbe vya mbinguni vyenye mabawa, navyo vitakuambia. Au onyesha kupendezwa kwako na dunia, nayo itakufundisha; na samaki wa baharini watakutangazia.”—AYUBU 12:7, 8.
KATIKA miaka ya karibuni, wanasayansi na mainjinia wamekubali mimea na wanyama iwafundishe. Wao huiga uumbaji wanapobuni mashine mpya na kuboresha mashine za zamani. Unapofikiria mifano ifuatayo, jiulize hivi, ‘Ni nani kwa kweli anayestahili kusifiwa kwa ubuni huo?’
Kujifunza Kutokana na Mapezi ya Nyangumi
Wabuni wa ndege za abiria wanaweza kujifunza nini kutokana na nyangumi mwenye nundu? Inaonekana wanaweza kujifunza mengi. Nyangumi mwenye nundu aliyekomaa huwa na uzito wa tani 30, uzito sawa na wa lori lililojazwa, na ana mwili mgumu na mapezi makubwa yanayofanana na mabawa. Mnyama huyo mwenye urefu wa meta 12 anaweza kusonga kasi majini. Kwa mfano, anapokula, nyangumi mwenye nundu anaweza kuogelea akielekea juu kwa mzunguko chini ya krasteshia au samaki, huku akitokeza mawimbi ya mapovu. Mawimbi hayo yaliyo kama wavu yana kipenyo cha meta 1.5, nayo hukusanya viumbe hao juu ya maji. Kisha nyangumi huyo anawanyafua kwa ghafula.
Jambo ambalo liliwashangaza watafiti ni jinsi kiumbe huyo aliye na mwili mgumu anavyoweza kuogelea kwa kuzunguka katika eneo dogo jinsi hiyo. Waligundua kwamba mapezi yake ndiyo humwezesha kuzunguka hivyo. Ncha ya mbele ya mapezi yao si laini kama bawa la ndege ya abiria, lakini imechongoka na ina sehemu zinazotokeza.
Nyangumi anapoogelea kwa kasi, sehemu hizo humsaidia kusonga juu. Kwa njia gani? Jarida
Natural History linasema kwamba sehemu hizo hufanya maji yapite kasi na kuyazunguka mapezi kwa utaratibu, hata nyangumi anapoogelea kwenda juu akiwa wima kwa kadiri fulani. Ikiwa mapezi ya nyangumi huyo yangekuwa na ncha laini, hangeweza kuogelea kwenda juu kwa kuzunguka katika eneo dogo jinsi hiyo kwani maji yangekuwa yakizunguka chini ya mapezi na kuzuia asiinuke.Ugunduzi huo unaweza kutumiwaje? Mabawa ya ndege za abiria yaliyoundwa kwa kuiga ubuni huo yatahitaji sehemu chache za mabawa zinazokunjwa au vifaa vingine vya kusaidia ndege kupaa. Mabawa kama hayo yangekuwa salama zaidi na rahisi kudumisha. John Long mtaalamu wa kuunda vitu kwa kuiga uumbaji anaamini kuwa hivi karibuni “kuna uwezekano mkubwa kwamba ndege zote za usafiri zitakuwa na mabawa yaliyo kama mapezi ya nyangumi mwenye nundu.”
Kuiga Mabawa ya Korongo
Bila shaka, mabawa ya ndege za abiria yanafanana na mabawa ya ndege wa angani. Hata hivyo, hivi karibuni mainjinia wamefanya maendeleo katika kuiga mabawa hayo. Gazeti New Scientist linaripoti hivi: “Watafiti katika Chuo Kikuu cha Florida wameunda ndege ndogo isiyoendeshwa na rubani iliyo na uwezo kama wa korongo wa kuelea, kuruka, na kupaa kwa kasi.”
Korongo hufaulu kuruka kwa njia hiyo kwa kukunja na kunyoosha mabawa yao kwenye viwiko na mabega. Gazeti New Scientist linasema kwamba kwa kuiga ubuni huo, “ndege hiyo ndogo ya sentimeta 60 isiyoendeshwa na rubani hutumia mtambo fulani na vyuma kadhaa kukunja na kupanua mabawa yake.” Mabawa hayo yaliyoundwa kwa ustadi yatawezesha ndege hiyo ndogo kuelea na kuruka katikati ya majengo marefu. Jeshi la Angani la Marekani linajitahidi sana kuunda ndege kama hiyo inayoweza kuendeshwa kwa urahisi ili kuitumia kutafuta silaha za kemikali na za kibiolojia katika majiji makubwa.
Kuiga Miguu ya Mjusi
Hata wanyama wa nchi kavu hutufunza mengi. Kwa mfano, mjusi ana uwezo wa kupanda kuta na kujishikilia akiwa chini juu kwenye dari. Hata katika nyakati za Biblia kiumbe huyo alijulikana kwa sababu ya uwezo huo wa ajabu. (Methali 30:28) Ni nini kinachomfanya asianguke?
Uwezo wa mjusi wa kujishikilia hata kwenye sehemu zilizo laini kama kioo unatokana na nywele ndogo zinazoitwa setae ambazo hufunika miguu yake. Miguu ya mjusi haitoi gundi. Badala yake, hiyo hutumia nguvu fulani ndogo
za molekuli. Molekuli zilizo kwenye miguu yake na kwenye dari hushikamana kwa sababu ya nguvu ndogo zinazoitwa nguvu za van der Waals. Kwa kawaida nguvu za uvutano huzidi nguvu hizo, na ndiyo sababu wewe huwezi kupanda ukuta kwa kuwekelea mikono yako sambamba ukutani. Hata hivyo, nywele ndogo zilizo kwenye miguu ya mjusi humwezesha kushikilia eneo kubwa zaidi ukutani. Nguvu za van der Waals zinazotokezwa na maelfu ya nywele hizo ndogo hutokeza nguvu za kutosha kumshikilia mjusi ambaye hana uzito mkubwa.Ugunduzi huo unaweza kutumiwaje? Vitu fulani vinavyotengenezwa viwandani kwa kuiga miguu ya mjusi vinaweza kutumiwa badala ya velcro, ambayo pia iliundwa kwa kuiga uumbaji. * Jarida The Economist linamnukuu mtafiti mmoja aliyesema kwamba kishikizo kinachotengenezwa kwa kuiga ubuni wa nywele ndogo kwenye miguu ya mjusi kinaweza kufaa sana katika “matibabu ambapo vishikizo vyenye kemikali haviwezi kutumiwa.”
Ni Nani Anayestahili Kusifiwa?
Wakati huu, shirika la NASA linatengeneza roboti yenye miguu mingi inayotembea kama nge, na mainjinia huko Finland tayari wametengeneza trekta yenye miguu sita ambayo inaweza kupanda kwenye vizuizi kama mdudu mkubwa anavyoweza kufanya. Watafiti wengine wamebuni kitambaa chenye pindo kwa kuiga ubuni wa kifuko cha mbegu za msindano ambacho hujifungua na kujifunga. Watengenezaji wa magari wanaunda gari kwa kuiga ubuni wa samaki anayeitwa boxfish ambaye anasonga kwa wepesi sana. Na watafiti wengine wanachunguza uwezo wa kuhimili mshtuko wa gamba la aina fulani ya konokono, ili kutengeneza mavazi ya kujikinga yaliyo mepesi zaidi.
Miundo mbalimbali imebuniwa kwa kuiga uumbaji hivi kwamba watafiti wameorodhesha maelfu ya mifumo ya kibiolojia. Wanasayansi wanaweza kufanya utafiti kwa kutumia orodha hiyo ili kupata “masuluhisho kutoka kwa vitu vya asili wanapokabili ugumu wa kubuni vitu fulani,” linasema jarida The Economist. Mifumo ya kiasili iliyo katika orodha hiyo husemwa kuwa “haki-miliki ya kibiolojia.” Kwa kawaida, mwenye haki-miliki ni mtu au kampuni iliyo ya kwanza kuandikisha kisheria wazo au mashine mpya. Likizungumza kuhusu orodha hiyo ya haki-miliki ya kibiolojia, jarida The Economist linasema hivi: “Kwa kurejelea vitu vilivyoigwa ambavyo vimebuniwa kwa ustadi kuwa ‘haki-miliki ya kibiolojia’, watafiti wanakazia tu kwamba kwa kweli vitu vya asili ndivyo vilivyo na haki-miliki.”
Ubuni huo wa ajabu katika vitu vya asili ulitokeaje? Watafiti wengi wanaweza kudai kwamba ubuni wote huo ulio katika vitu vya asili ulijitokeza wenyewe kupitia mageuzi ambayo yametukia kwa mamilioni ya miaka. Hata hivyo, watafiti wengine wamekata kauli tofauti. Mnamo 2005 mtaalamu wa biolojia Michael Behe aliandika hivi katika gazeti The New York Times: “Ubuni uliopo [katika vitu vya asili] huandaa hoja rahisi yenye kusadikisha: ikiwa anafanana, anatembea, na kulia kama bata, na ikiwa hakuna hoja zilizo kinyume, basi lazima tukate kauli kwamba ni bata.” Alifikia mkataa gani? “Ubuni wa kitu haupaswi kupuuzwa eti kwa sababu tu uthibitisho unapatikana kwa urahisi.”
Bila shaka, injinia anayebuni bawa la ndege ya abiria lililo salama na linalofanya kazi vizuri zaidi anastahili kusifiwa. Hali kadhalika, mbuni anayevumbua bendeji yenye matumizi mbalimbali, kitambaa laini zaidi, au gari bora zaidi, anastahili kusifiwa kwa sababu ya ubuni wake. Kwa kweli, mtengenezaji wa bidhaa anayeiga ubuni wa mvumbuzi fulani lakini anakataa kumpa sifa mvumbuzi huyo, anaweza kuonwa kuwa mhalifu.
Hivyo, je, unaona kwamba inapatana na akili kwa watafiti walio na elimu ya hali ya juu kuiga mifumo ya asili kutatua matatizo magumu ya kiinjinia na kusema kwamba ubuni huo wa hali ya juu ulitokana na mageuzi bila akili yoyote? Ikiwa lazima kuwe na mbuni mwenye akili ili kutokeza nakala, vipi kuvumbua kitu chenyewe? Kwa kweli, ni nani anayestahili kusifiwa
zaidi, msanii mkuu au mwanafunzi anayeiga ubuni wa msanii?Mkataa Unaopatana na Akili
Baada ya kuchunguza uthibitisho uliopo kwamba vitu vya asili vilibuniwa, watu wengi wamekata kauli inayopatana na ile ya mtunga-zaburi aliyeandika hivi: “Jinsi kazi zako zilivyo nyingi, Ee Yehova! Zote umezifanya kwa hekima. Dunia imejaa vitu ulivyotokeza.” (Zaburi 104:24) Paulo ambaye pia aliandika Biblia alikata kauli kama hiyo. Alisema: “Kwa maana sifa [za Mungu] ambazo hazionekani, zinaonekana waziwazi tangu kuumbwa kwa ulimwengu na kuendelea, kwa sababu zinaeleweka kwa vitu vilivyofanywa, yaani, nguvu zake za milele na Uungu.”—Waroma 1:19, 20.
Hata hivyo, watu wengi wanyoofu ambao wanaiheshimu Biblia na wanaamini kwamba kuna Mungu wanaweza kusema kwamba huenda Mungu aliumba vitu vyote vya asili kupitia mageuzi. Lakini, Biblia inafundisha nini?
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 15 Velcro ni aina ya kishikizo cha kubandika na kubandua kinachoundwa kwa kuiga ubuni wa mbegu za mmea unaoitwa burdock.
[Blabu katika ukurasa wa 5]
Ubuni wa ajabu katika vitu vya asili ulitokeaje?
[Blabu katika ukurasa wa 6]
Ni nani aliye na hati-miliki ya vitu vya asili?
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 7]
Ikiwa lazima kuwe na mbuni mwenye akili ili kutokeza nakala, vipi kuvumbua kitu chenyewe?
Ndege inayoweza kuendeshwa kwa urahisi imebuniwa kwa kuiga bawa la korongo
Miguu ya mjusi haiwezi kuchafuka wala kuacha alama, nayo hujishikilia kwenye sehemu yoyote isipokuwa “Teflon” na inaweza kushikilia na kuacha kitu bila tatizo. Watafiti wanajaribu kuiga miguu hiyo
Ubuni wa samaki anayeitwa “boxfish” anayesonga kwa wepesi sana ulichochea kubuniwa kwa gari fulani
[Hisani]
Airplane: Kristen Bartlett/ University of Florida; gecko foot: Breck P. Kent; box fish and car: Mercedes-Benz USA
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8]
WASAFIRI WENYE HEKIMA YA KISILIKA
Viumbe wengi hutumia “hekima ya kisilika” kusafiri huku na huku duniani. (Methali 30:24, 25) Fikiria mifano miwili.
▪ Chungu Hujiongozaje Barabarani? Chungu wanaotoka kutafuta chakula hujuaje njia ya kurudi kwenye makao yao? Watafiti huko Uingereza waligundua kwamba mbali na kuacha harufu kwenye njia, chungu fulani hutumia hesabu za maumbo kuweka alama zinazowasaidia kurudi kwenye makao yao. Kwa mfano, gazeti New Scientist linasema kwamba chungu wanaoitwa pharaoh “wanapotoka katika makao yao wao huacha mistari inayongaa ambayo inaachana kwa pembe ya digrii 50 au 60.” Ni nini kinachostaajabisha kuhusu tabia hiyo? Chungu anapokuwa njiani kurudi nyumbani na afike kwenye njia panda, kisilika yeye hutumia njia ambayo haitampoteza sana lakini mwishowe itamfikisha nyumbani. Makala hiyo inasema: “Jambo hilo huwasaidia chungu wasipotee njia na hivyo wasitumie nguvu nyingi wanapotafuta njia ya kurudi nyumbani.”
▪ Dira ya Ndege Ndege wengi wanaweza kutambua wanakoelekea kwa usahihi wa hali ya juu wanapofunga safari ndefu haidhuru hali ya hewa. Jinsi gani? Ndege wanaweza kuhisi nguvu ya sumaku ya dunia. Hata hivyo, jarida Science linasema “mistari ya nguvu ya sumaku [ya dunia] hutofautiana kutoka mahali pamoja kwenda pengine na nyakati nyingine haielekezi kaskazini kabisa.” Ni nini huwasaidia ndege wanaosafiri wasipotee njia? Kila jioni ndege hurekebisha dira yao ya kiasili kulingana na jua linavyotua. Kwa kuwa jua hutua sehemu mbalimbali ikitegemea mabadiliko ya latitudo na majira, watafiti wanafikiri kwamba ni lazima ndege hao wawe na uwezo wa kufanya mabadiliko kwa kutumia “saa ya kiasili ambayo huwawezesha kujua wakati hususa wa mwaka,” linasema jarida Science.
Chungu walipataje uwezo wa kufanya hesabu za maumbo? Ndege walipataje dira, saa ya kiasili, na ubongo unaoweza kuchanganua habari hiyo? Je, ni kutokana na mageuzi? Au ni kutoka kwa Muumba mwenye akili?
[Hisani]
© E.J.H. Robinson 2004