Kuutazama Ulimwengu
Kuutazama Ulimwengu
▪ “Sasa misiba tisa kati ya kumi inasababishwa na hali ya hewa. Katika miaka 20 ambayo imepita misiba imeongezeka mara mbili kutoka misiba 200 hadi zaidi ya misiba 400 kwa mwaka.”—JOHN HOLMES, MSAIDIZI WA KATIBU-MKUU WA UMOJA WA MATAIFA KWA AJILI YA MSAADA WA KIBINADAMU NA MRATIBU WA MISAADA YA DHARURA.
Wenyeji wa Asili wa Amerika Wapewa Haki Zao
Azimio la Umoja wa Mataifa Kuhusu Haki za Wenyeji wa Asili wa Amerika, lililopitishwa mnamo 2007, sasa limetafsiriwa katika lugha za Maya na Nahuatl, lugha mbili zinazozungumzwa sana na wenyeji hao wanaoishi Mexico. “Watu milioni 10 hivi [nchini Mexico] hawajui haki zao,” linasema gazeti El Universal. “Hivyo, mara nyingi hawajui kwamba wanatendewa vibaya.” Inasemekana kwamba tafsiri hizo zitatumiwa kuwasaidia watu hao wajue jinsi ya kutetea haki zao za msingi.
Kuuza Ubikira
Wanasoshiolojia wanashangazwa sana kwamba vijana fulani nchini Poland wako tayari kuuza ubikira wao, linaripoti gazeti Newsweek Polska. Jacek Kurzępa, mtaalamu wa mambo ya akili katika Chuo Kikuu cha Zielona Góra anasema kwamba “vijana wanasikia kutoka kila mahali kwamba kila kitu kinapaswa kuuzwa.” Wengi zaidi wananadi ubikira wao kwenye Intaneti. Hata hivyo, vijana hao wanapata madhara mengi zaidi kwa kufanya hivyo. “Uamuzi huo unaathiri maisha yao yote na uhusiano wa wakati ujao na mtu atakayekuwa mwenzi wao,” anasema Kurzępa.
Msitu wa Amazoni Uliwahi Kukaliwa
Inasemekana kwamba huenda maeneo makubwa ya Amazoni ya kusini yanayosemwa kuwa hayajawahi kukaliwa na wanadamu yalikuwa na jamii za watu waliostaarabika “wakiwa wamejenga kuta kubwa.” Mtaalamu fulani wa mambo ya wanadamu alifikia mkataa huo alipokuwa akichunguza mambo huko Mato Grosso, Brazili. Waligundua “miji na vijiji vingi vilivyozungukwa na kuta” vikiwa vimefunikwa na misitu mikubwa katika eneo lenye ukubwa wa kilomita 30,000 za mraba. Baadhi ya miji hiyo ilikuwa na ukubwa wa ekari 150. Ripoti ya Chuo Kikuu cha Florida, ambako mtaalamu huyo alitoka, inasema kwamba makazi hayo “ni ya mwaka wa 1250 hadi 1650, wakati ambao huenda wakazi wa miji hiyo waliuawa na wakoloni na magonjwa waliyoleta kutoka Ulaya.”
Mimea Humsaidia Mtu Kupona Baada ya Upasuaji
Imesemwa kwa muda mrefu kwamba mimea inaweza kumsaidia mtu kupunguza mfadhaiko, kumfanya awe na mtazamo mzuri, na kupunguza maumivu ya mgonjwa. Uchunguzi wa hivi karibuni unathibitisha jambo hilo. “Baada ya kupasuliwa wagonjwa waliwekwa katika vyumba mbalimbali vya hospitali vilivyo na mimea na vingine ambavyo havikuwa na mimea,” linasema gazeti Science Daily. Wagonjwa waliokuwa na mimea katika vyumba vyao hawakuwa na maumivu mengi, walihitaji dawa chache zaidi za kupunguza maumivu, mioyo yao ilipiga kwa mwendo unaofaa na walikuwa na shinikizo la kawaida la damu, na waliridhika zaidi na vyumba vyao kuliko wale wasiokuwa na mimea. Asilimia 93 hivi ya wale waliowekwa katika vyumba vyenye mimea walisema kwamba kilichowavutia zaidi katika vyumba vyao ni mimea hiyo.