Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

“Eneo Lisilojulikana” la Bolivia

“Eneo Lisilojulikana” la Bolivia

“Eneo Lisilojulikana” la Bolivia

MNAMO 1906 msimamizi wa Shirika la Kijiografia la Uingereza alizungumza na Kanali Percy Harrison Fawcett kuhusu uwezo mkubwa wa kiuchumi wa Amerika Kusini. Akimsogezea Fawcett chati fulani ya eneo hilo, msimamizi huyo alimwambia hivi: “Tazama eneo hili! Lina maeneo mengi ambayo hayajatiwa alama kwa kuwa hayajulikani.” Kisha akampa kanali huyo kazi ya kuvumbua eneo hilo. Fawcett alikubali kazi hiyo.

Katika majarida yake, Fawcett alieleza kuhusu eneo lenye milima yenye misitu mikubwa linalojulikana leo kama Uwanda wa Huanchaca nchini Bolivia. Aliliita eneo hilo “eneo lisilojulikana.” * Wengine wanaamini kwamba maandishi na picha za Fawcett zilimchochea mwandishi mashuhuri wa Uingereza Sir Arthur Conan Doyle aandike kitabu The Lost World, ambacho kinafafanua ulimwengu wa kuwaziwa wa “sokwe watu” na dinosa wenye kutisha ambao inasemekana waliishi kufikia nyakati za kisasa. Leo eneo hilo lenye utulivu la Amazoni linatia ndani Mbuga kubwa ya Taifa ya Noel Kempff Mercado nchini Bolivia, ambayo mwaka wa 2000 ilichaguliwa kuwa eneo linalostahili Kuhifadhiwa Ulimwenguni. *

Mbuga hiyo, ambayo iko kaskazini mashariki kabisa ya Bolivia kwenye mpaka wa Brazili, ni nyika yenye ukubwa wa kilomita 15,000 hivi za mraba ambayo haijaathiriwa na utendaji wa wanadamu. Eneo hilo lina mazingira matano ya aina mbalimbali: Nyanda za juu zenye misitu isiyokauka, misitu yenye miti inayopukutika majani yake, nyanda za juu zenye mbuga zilizokauka, mbuga zenye vinamasi, na misitu yenye vinamasi. Uwanda wa Huanchaca una ukubwa wa kilomita 5,180 za mraba na umeinuka kwa kimo cha mita 550 juu ya eneo linalozunguka na umeenea katika eneo lenye urefu wa kilomita 150 kwenye upande wa mashariki wa mbuga hiyo. Mito mingi ambayo hupita katika uwanda huo na eneo linalozunguka ina maporomoko 20 hivi, kutia ndani Maporomoko ya Salto Susana, Maporomoko ya Arco Iris, Maporomoko ya Federico Ahlfeld, Maporomoko ya Gemelas, na Maporomoko ya El Encanto.

Safari Yetu Yaanza

Kwa kuwa mbuga hiyo iko mbali na makao ya watu, inawavutia sana watalii wanaojali mazingira, wengi wao husafiri kwa ndege kutoka Santa Cruz, Bolivia ya kati. Tuliamua kusafiri kilomita hizo 700 kwa gari, na hivyo tukafaulu kuona maeneo ya mashambani ya Bolivia. Tulipofika sehemu fulani, tuliona kitu kama wingu la majani maridadi yaliyokuwa yakipeperushwa barabarani. Hata hivyo, “majani” hayo yalikuwa vipepeo, na si sisi tu tuliowaona. Kikundi cha mijusi wenye njaa walikuwa wakiwakimbiza na kuwala.

Tulipowasili kwenye mbuga hiyo ya taifa, tulikutana na yule ambaye angetutembeza, anayeitwa Guido kwenye kijiji cha La Florida, kilichoko kwenye kingo za Mto Paragua. Guido alituvusha mto huo pamoja na gari letu juu ya feri ya aina fulani na tukasafiri umbali fulani hadi kambi ya Los Fierros. Njiani tulimwona mbweha na ndege fulani maridadi anayeitwa mbarawaji wakivuka mbele yetu barabarani.

Baada ya kulala usiku, tuliamka na kuwasikia kasuku wanne wenye mikia mirefu wenye manyoya ya rangi ya bluu na manjano wakipiga kelele juu ya mti nje ya mahali tulipokuwa tumelala. Ni kana kwamba walikuwa wakituambia, “Karibuni nyumbani kwetu!” Hilo lilionyesha kwamba siku yetu imeanza vizuri na kwamba tutaifurahia.

Msitu Wenye Viumbe Wengi

Mbuga ya Taifa ya Noel Kempff Mercado ina zaidi ya aina 600 za ndege, wanyama 139 tofauti-tofauti (wengi kuliko wanyama wote wanaoishi Amerika Kaskazini), aina 74 za wanyama wanaotambaa, na labda aina 3,000 hivi za vipepeo, bila kuhesabu wadudu. Ndege wanatia ndani zaidi ya aina 20 za kasuku, na vilevile tai anayeitwa harpy, ndege anayeitwa hoatzin, na helmeted manakin. Nick Acheson, mtaalamu wa ndege na mhifadhi wa mazingira, alituambia kwamba “ndege wanaokabili hatari ya kutoweka kama vile pygmy-tyrant mwenye ubavu mwekundu na chiriku mpasua-mbegu huwavutia watu kutoka sehemu zote za dunia wanaopenda kutazama ndege.”

Kati ya wanyama wengi wanaopatikana huko kuna anteater wakubwa, mbwa-mwitu wenye manyoya shingoni, chui wa Amerika Kusini, nguruwe-mwitu, tapir, na mbawala anayeitwa pampas. Mito mingi inayozunguka na kupita katika mbuga hiyo ina viumbe wengi pia, kutia ndani aina 62 za amfibia na aina 254 za samaki, kutia ndani mamba wa Amerika Kusini, fisi-maji wakubwa, mnyama-mgugunaji anayeitwa capybara, na pomboo wenye rangi maridadi ya waridi. Kwa kweli, mbuga hiyo ni paradiso kwa mtu anayependa mazingira!

Kwa sababu kuna wanyama wakubwa wa jamii ya paka katika eneo la Amazoni, watalii wengi huwa na wasiwasi, nasi tulikuwa na woga. Msimamizi wa kambi ya Los Fierros alitueleza kuhusu usiku wake wa kwanza kulala katika mbuga hiyo. “Niliamka usiku wa manane nikihisi kwamba nilikuwa nikitazamwa,” akatueleza. “Nilitazama nje ya dirisha na kumwona chui akinitazama, tukiwa tumetenganishwa tu na wavu! Kwa woga, nilijifungia bafuni hadi asubuhi.” Hilo lilitufanya tuwe na wasiwasi zaidi!

Lakini msimamizi huyo akatuambia: “Niligundua kwamba mnyama huyo hutembelea eneo hilo usiku na si hatari. Kwa kweli, siku zenye joto chui hao huingia kambini na kujilaza kwenye varanda. Kama unavyoweza kuwazia, mgeni anaweza kushtushwa sana na jambo hilo. Zamani, tulibeba bunduki kila mara tulipokuwa tukiwatembeza wageni, hasa usiku, lakini siku hizi hatubebi. Wanyama hawajabadilika; sisi ndio tumebadili mtazamo wetu kuwaelekea.” Hata hivyo, alituonya kwamba tunapaswa kujihadhari na wanyama wote wa mwituni.

Kutembea Msituni Kuelekea Maporomoko ya El Encanto

Maporomoko mengi ya mbuga hiyo huwavutia watu wengi. Tulitoka mapema na kutembea pamoja na Guido aliyekuwa akitutembeza, kuelekea Maporomoko ya El Encanto, yanayoporomoka kwa kina cha mita 80 kutoka kwenye Uwanda wa Huanchaca. Tunapotembea kwa kilomita 6 katika msitu wa mvua, tuliwaona tumbili wa aina mbili wakipiga kelele juu kwenye matawi. Aina moja ya tumbili hao walikuwa na mikono na miguu mirefu na aina ile nyingine hupiga kelele kwa sauti ya juu sana inayoweza kusikika umbali wa kilomita tatu hivi! Mbele kidogo, ndege anayefanana na bata-mzinga alikimbia mbele yetu akitafuta kiamsha-kinywa. Guido alituonyesha alama za nyayo kwenye kingo za kijito kilichokuwa karibu. Alitambua kwamba nyayo hizo zilikuwa za aina mbili tofauti za mbawala, na pia tapir, chui wa Amerika Kusini, na puma. Tulihisi kana kwamba tulikuwa tukitazamwa na wanyama wa aina mbalimbali waliokuwa wamejificha na kwamba usiku na mchana eneo hilo huwa na wanyama wengi.

Wanyama hao wana vichaka vingi vya kujificha, kwa kuwa maeneo mbalimbali ya mbuga hiyo yana mimea ya aina nyingi sana. Kwa kweli, inakadiriwa kwamba kuna aina 4,000 za mimea katika eneo hilo, kutia ndani zaidi ya aina 100 za okidi, na vilevile aina nyingi za miti, mikangaga, bromeliad, na mimea inayotambaa. Macho yetu yalivutiwa na rangi maridadi ya mimea hiyo, pua zetu zikanusa harufu yake nzuri, nasi tukala matunda yake yaliyokuwa kando ya barabara. Matunda hayo yalitia ndani tunda la mangaba, linalokua juu ya mti, na karakara linalokua kwenye mmea unaotambaa.

Mwishowe, tulipokuwa tukivuka kijito fulani, tulianza kusikia kwa mbali sauti ya maporomoko ya maji, na kila hatua tuliyopiga sauti hiyo iliongezeka. Kisha kwa ghafula, tulitokea eneo la wazi, na mbele yetu tuliona Maporomoko makubwa ya El Encanto, sehemu yake ya chini ikiwa imefichwa kwa ukungu. Mikangaga na bromeliad imekua kwenye miamba inayozunguka dimbwi la maji safi sana ya maporomoko hayo. Guido alituambia, “Katika siku zenye joto, tumbili huingia ndani ya maji hayo ili kujiburudisha.” Tulitambua alichokuwa akijaribu kutuambia, kwa hiyo sisi tukafanya hivyo pia, huku tukifurahia utulivu wa eneo hilo maridadi na sauti ya maji yanayoporomoka.

Kuhifadhi Mazingira—Kazi Iliyoanzishwa na Noel Kempff Mercado

Mhifadhi wa mazingira, Noel Kempff Mercado, alikufa mnamo 1986. Hata hivyo, kazi aliyoanzisha ya kuhifadhi eneo hilo la Bolivia inaendelea. Mnamo 1996, serikali ya Bolivia na ya Marekani zilifanya mkataba wa kuhifadhi ekari milioni 2.2 za msitu na wakaanzisha mradi wa kupunguza gesi zinazoongeza kiwango cha joto duniani. Mwaka uliofuata, serikali ya Bolivia na kampuni tatu za kutokeza nishati zikaanzisha Mradi wa Noel Kempff wa Kuboresha Hali ya Hewa, ambao ulivunja mikataba ya kukata miti kwenye ekari milioni 2.2 za msitu huo. Eneo hilo liliunganishwa na mbuga hiyo na hivyo kuongeza ukubwa wa mbuga hiyo mara mbili.

Kutembelea kwetu eneo hilo maridadi kuliongeza uthamini wetu kwa Muumba na vitu maridadi na vya aina mbalimbali ambavyo ameweka kwenye Dunia. Zaburi 104:24 inasema hivi: “Jinsi kazi zako zilivyo nyingi, Ee Yehova! Zote umezifanya kwa hekima. Dunia imejaa vitu ulivyotokeza.” Kwa kweli, tulipotembea katika ‘eneo hilo lisilojulikana’ ambalo halijaharibiwa na utendaji wa wanadamu, tulitamani kutembea bila kelele, tukitafakari umaridadi wake, na kutoka bila kitu chochote ila picha kwenye kamera zetu na kumbukumbu moyoni mwetu.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 3 Mnamo Mei (Mwezi wa 5) 1925, Fawcett alimwandikia mke wake kuhusu safari yake. Hiyo ndiyo iliyokuwa mara yake ya mwisho kuwasiliana na bado haijulikani jinsi alivyopotea.

^ fu. 3 Ilipoanzishwa mwaka wa 1979, mbuga hiyo iliitwa Mbuga ya Taifa ya Huanchaca. Jina lake lilibadilishwa mwaka wa 1988 na kuitwa Noel Kempff Mercado ili kumkumbuka mwanabiolojia huyo wa Bolivia, aliyeuawa kwenye nyanda hizo na walanguzi wa madawa ya kulevya baada ya yeye kugundua bila kujua maabara ya kutengeneza kokeini.

[Picha katika ukurasa wa 16]

Okidi za zambarau na nyekundu

[Picha katika ukurasa wa 16, 17]

Maporomoko ya Ahlfeld, ndani ya mbuga ya taifa

[Picha katika ukurasa wa 17]

Kasuku

[Picha katika ukurasa wa 17]

Maporomoko ya El Encanto

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 15]

Aerial: ® 2004 Hermes Justiniano/BoliviaNature.com

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 17]

Orchid, Ahlfeld Falls, and macaws: ® 2004 Hermes Justiniano/BoliviaNature.com