Njoo Ujionee Soko la Kiafrika
Njoo Ujionee Soko la Kiafrika
NJIA moja nzuri ya kuelewa utamaduni, desturi, na chakula cha nchi yoyote ni kwenda sokoni. Ukiwa huko utawaona watu wa nchi hiyo, uonje chakula chao, na kununua bidhaa zao. Pia utakutana na wauzaji wenye uchangamfu ambao watajitahidi sana kuwasiliana nawe hata uwe unazungumza lugha gani.
Ni vigumu kupata soko lenye kusisimua zaidi kuliko masoko ya Afrika. Yana watu wengi sana na utapata bidhaa za kila aina. Ukiwa huko utahisi msisimko wa Afrika. Tembelea nami soko fulani huko Douala, nchini Kamerun.
Kwenda Sokoni Kama Waafrika
Katika majiji mengi makubwa ya Afrika, kutumia pikipiki ndiyo njia ya haraka zaidi na isiyogharimu ya kwenda sokoni. Karibu kwenye kila kona, kuna watu wanaoweza kukubeba kwa pikipiki. Ukiwa na ujasiri unaweza kumwomba mmoja akubebe. Nchini Kamerun, njia hiyo ya usafiri ndiyo nzuri kwa sababu utasafiri haraka na kwa bei nafuu.
Kwa wale ambao hawataki msisimko wa aina hiyo, kuna teksi nyingi za kawaida. Mara nyingi abiria kadhaa hujazana katika gari moja ili kupunguza gharama.
Vibanda Vingi Sana
Mgeni anayetembelea soko kwa mara ya kwanza anaweza kushangazwa na idadi ya watu na vibanda barabarani. Watu wengi sana kutia ndani watoto, hubeba bidhaa zao vichwani. Unapotazama vizuri utaona kwamba vikapu vyao vina kuku walio hai, machungwa yaliyotolewa maganda, na dawa mbalimbali, pamoja na vitu vingine.
Juu ya meza nyingi za mbao kulikuwa na mboga, kama vile kabeji, karoti, matango, biringani, aina fulani ya maboga, maharagwe ya aina fulani, viazi vitamu, nyanya, viazi vikuu, na aina mbalimbali za letusi. Huenda wageni kutoka mabara mengine wasifahamu vyakula vyote, kwa kuwa vingine havipatikani kwa urahisi nje ya Afrika. Huenda vibanda vyenye kuvutia zaidi vikawa vile vinavyouza pilipili nyekundu na ya manjano, ambazo zimetoka tu kuchunwa hivi kwamba zinang’aa zinapopigwa na jua la asubuhi. Vibanda vingi vina maparachichi, ndizi, mabalungi, matikiti, mananasi machungwa, na limau.
Yanachochea sana hamu ya kula, na yanauzwa kwa bei nafuu! Viazi vikuu, mihogo, na mchele, ambavyo ndivyo vyakula vikuu vinavyokuzwa nchini, vinauzwa pia kwa wingi pamoja na vitunguu na vitunguu saumu viliyoletwa kutoka nchi nyingine.Katika soko moja la Douala, wauzaji wengi ni wa makabila ya Hausa na Fula. Wafanyabiashara hao wanatambulika waziwazi kwa sababu ya nguo zao ndefu nyeupe, za bluu, au manjano zinazoitwa gandouras au boubous na pia kwa sababu ya salamu yao ya kirafiki katika lugha ya Fulfulde. Soko hilo limetulia. Pindi hii, muuzaji mmoja anayeitwa Ibrahim, anachagua vitunguu vitatu vikubwa na kunipa kama zawadi. Ananiambia, “Mwambie mke wako atie wali ulio na vikolezo ndani yake na kuvipika polepole.”
Mbele kidogo kuna mahali ambapo nyama inauzwa—hasa ya ng’ombe na mbuzi—waliotoka tu kuchinjwa. Wanaume wenye nguvu wanabeba wanyama waliochinjwa na kuchunwa ngozi kwenye mabega yao na kuwabwaga juu ya meza. Mabucha wakiwa wameshika visu virefu kwa ustadi, wanawaomba wateja wachague sehemu ya nyama wanayotaka kukatiwa. Pia, kuna mbuzi, kuku, na nguruwe walio hai wanaouzwa kwa ajili ya wateja ambao wanataka kujichinjia.
Njoo Ule Kwenye Mkahawa
Huwezi kukosa mahali pa kula katika soko la Afrika. Nchini Kamerun, vibanda fulani vya kuuza chakula huwa na muziki wenye sauti ya juu ili kuwavutia wateja, lakini pia unaweza kupata vibanda vilivyotulia ambako unaweza kula chakula cha Kiafrika na kukutana na watu wa eneo hilo. Huenda orodha ya vyakula ikawa imeandikwa juu ya ubao mweusi, na mtu ambaye hafahamu vyakula vya kienyeji atahitaji msaada ili aelewe vyakula vinavyotajwa.
Vyakula viwili vya msingi ni wali na fufu, chakula kilichopondwa kutokana na mihogo, ndizi, au viazi vikuu. Pia unaweza kula nyama iliyochomwa ya samaki, ng’ombe, na kuku iliyoandaliwa pamoja na mchuzi wa mbinda, siagi ya karanga, au nyanya. Hakuna haraka ndani ya mikahawa hiyo, na kuna nafasi ya kutosha ya kuzungumza.
Wahudumu wawili wa kike wanakuja kutuhudumia. Mmoja wao amebeba sinia kubwa yenye sahani za chuma zinazotoa moshi zilizojaa wali, maharagwe, na fufu. Vyakula hivyo vimetiwa mchuzi wa mbinda na pia kuna mishikaki ya nyama na ya samaki. Pia kuna bakuli dogo lenye pilipili kali sana kwa ajili ya wale wanaopenda kula vyakula motomoto. Mhudumu wa pili amebeba taulo na beseni lenye maji ili tunawe mikono yetu. Tunahitaji kunawa kwa kuwa vyakula vya kienyeji huliwa bila vijiko. Si ajabu kwa mteja kusali kabla ya kula kisha usikie wateja wengine katika meza zilizo karibu wakijiunga naye kusema “Amina.”
Kuhubiri Habari Njema Sokoni
Kwa muda mrefu, soko limetimiza fungu muhimu katika jamii nyingi. Ni mahali panapofaa si kwa ajili ya kuuza na kununua bidhaa tu, bali pia kwa kupashana habari, kukutana na marafiki, na hata kutafuta kazi. Biblia inasema kwamba Yesu alitembelea masoko mengi na kuwafundisha watu kumhusu Mungu na kuwaponya. Pia mtume Paulo alizungumza “sokoni pamoja na wale waliokuwapo.” (Matendo 17:16, 17; Marko 6:56) Leo pia, Mashahidi wa Yehova nchini Kamerun wanaona kwamba sokoni ni mahali panapofaa kuhubiri habari njema ya Ufalme wa Mungu.—Tumetumiwa makala hii.
[Picha katika ukurasa wa 24]
Pilipili zenye kuvutia