Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kutoa Msaada wa Dharura

Kutoa Msaada wa Dharura

Kutoa Msaada wa Dharura

● Mwanamke mja-mzito alikuwa ameketi katika jumba kubwa akisikiliza programu ya mafundisho ya Biblia. Ghafula, akashikwa na uchungu wa kuzaa. Lakini hali hiyo ilishughulikiwa kwa njia inayofaa. Kulikuwa na ambulansi karibu, na baada ya dakika chache, mwanamke huyo na mume wake walifika hospitalini. Alizaa binti mrembo.

Leo, ambulansi zinazowahudumia wagonjwa mahututi hutimiza fungu muhimu katika mfumo wa huduma za afya za nchi nyingi. Magari hayo huwa na wahudumu wenye ujuzi wa kushughulikia hali za dharura, kama vile, madaktari, wauguzi, na madereva wenye ujuzi. * Yana vifaa maalumu vya kushughulikia hali za dharura kama vile aksidenti za barabarani, mshtuko wa moyo, kiharusi, au akina mama waliopatwa na uchungu wa kuzaa. Kila mwaka maelfu ya watu huokolewa kupitia huduma hii ya kutoa msaada wa dharura.

Treni za abiria ziliposhambuliwa huko Madrid, Hispania, mnamo 2004 watu 400 hivi waliokolewa kwa sababu wafanyakazi wa ambulansi walitenda upesi na kwa ustadi. * Dakt. Ervigio Corral Torres, msimamizi wa kitengo cha huduma za dharura cha Madrid, anakumbuka tukio hilo lenye kuogopesha. “Matukio kama hayo ndiyo huwavutia waandishi wa habari,” anaeleza, “lakini sisi hufanya kazi yetu kwa ustadi zaidi tunaposhughulikia hali za dharura za kila siku. Hiyo ndiyo sehemu bora zaidi ya huduma hii, kuokoa maisha ya watu ambao huenda hawangekuwa hai leo.”

Alipoulizwa ni nini ambacho kinahitajiwa ili kuwasaidia kufanya kazi yao vizuri zaidi, Dakt. Corral Torres alisema hivi: “Ingekuwa vizuri zaidi ikiwa watu wangetupigia simu wakati tu kuna sababu ya kufanya hivyo.” Aliongezea hivi: “Lengo letu ni kuwahudumia watu kwa njia bora zaidi popote walipo, wakati wowote, na haraka iwezekanavyo mara tu tunapopokea simu ya kuomba msaada.” Katika majiji makubwa, ambulansi huwafikia watu baada ya dakika kumi hivi.

Katika majiji fulani yenye watu wengi sana, kama vile, São Paulo, Brazili, msongamano wa magari hufanya kazi ya madereva wa ambulansi iwe ngumu, kwa hiyo wahudumu wa afya hutumia pikipiki. Wakitumia pikipiki wanaweza kufika kabla ya ambulansi ili wachunguze na kupunguza hatari ambayo mgonjwa anakabili. Majiji mengine yametumia mbinu hiyo ya kutoa huduma za dharura kama vile London, Uingereza; Kuala Lumpur, Malaysia; na Miami, Marekani.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 3 Lazima madereva wa ambulansi wajue jinsi ya kutumia vifaa vya ambulansi na jinsi ya kuendesha gari hilo ikitegemea wamebeba mgonjwa aliye na tatizo gani.

^ fu. 4 Ona Amkeni! la Novemba 8, 2004 (8/11/2004), ukurasa wa 14.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 11]

JINSI UNAVYOWEZA KUSAIDIA

Unaweza kufanya mambo fulani ya msingi kunapokuwa na hali ya dharura ili kuwasaidia watoaji wa huduma za dharura wafanye kazi yao ya kuokoa uhai:

1. Piga namba ya simu ya dharura haraka. Katika Muungano wa Ulaya namba hiyo ni 112, Marekani ni 911, Kenya ni 999, na Tanzania ni 115.

2. Sema waziwazi mahali ambapo hali ya dharura imetukia.

3. Taja dalili zinazoonekana waziwazi. Kwa mfano, je, mtu huyo anapumua? Je, amepoteza fahamu? Je, anatokwa na damu?

4. Ikiwa ana majeraha kadhaa, usimsogeze kwani kufanya hivyo kutazidisha majeraha hayo.

5. Ikiwa mtu huyo anatapika, mlaze upande mmoja ili asisakamwe.