Kuutazama Ulimwengu
Kuutazama Ulimwengu
“Inakadiriwa kwamba dola bilioni 1464. Zilitumiwa katika shughuli za kijeshi ulimwenguni mnamo 2008. Hilo ni ongezeko . . . la asilimia 45 tangu mwaka wa 1999.”—TAASISI YA UCHUNGUZI WA AMANI YA KIMATAIFA YA STOCKHOLM, SWEDEN.
“Kulingana na kampuni ya Google, mabilioni ya tovuti huongezwa kwenye Intaneti kila siku.”—NEW SCIENTIST, UINGEREZA.
“Ilisemekana kwamba idadi ya watu wanaolala njaa kila siku ingefikia milioni 1 020 katika mwaka wa 2009, idadi ambayo haijawahi kufikiwa katika historia.”—SHIRIKA LA CHAKULA NA KILIMO LA UMOJA WA MATAIFA, ITALIA.
Ngamia wa Kwanza Kutokezwa Katika Maabara
Tangu mwaka wa 1996, watafiti walipotokeza kondoo kwa kutumia chembe za urithi, wanyama kadhaa kutia ndani ng’ombe, mbuzi, na farasi walitokezwa kupitia mbinu hiyohiyo. Wanasayansi katika kituo cha kuwatibu wanyama huko Dubai wamefaulu kwa mara ya kwanza kutokeza ngamia katika maabara. Mtoto huyo wa kike wa ngamia aliitwa Injaz, jina la Kiarabu linalomaanisha “mafanikio.” Gazeti The National la Abu Dhabi lilisema hivi: “Kutokeza wanyama katika maabara . . . kumeacha kuwa jambo linalofanywa kwa ajili ya utafiti tu. Wakati ujao, programu hiyo itachunguza uwezekano wa kutumia mbinu hizo kupata chembe za urithi kutoka kwa ngamia bora zaidi wanaotumiwa katika mashindano ya mbio na kutokeza maziwa.”
“Aksidenti” za Setilaiti
“Njia zinazotumiwa na vifaa vya angani vilivyo juu ya Dunia zimesongamana zaidi kadiri ambavyo miaka imepita, lakini haikuwa hadi Februari [2009] ndipo setilaiti za kwanza zilipopatwa na aksidenti,” linaripoti gazeti Science News. Kilomita 800 hivi juu ya Siberia, setilaiti ya Marekani ya mawasiliano iligongana na kifaa cha kijeshi cha Urusi. Setilaiti hizo zilivunjika-vunjika katika vipande vikubwa 700 hivi. Ikiwa vipande kama hivyo havitaondolewa angani, huenda aksidenti nyingine kama hiyo ikatokea kwa urahisi. Kwa sasa vituo vinavyochunguza jinsi setilaiti zinavyosonga vinaonyesha kwamba kuna vipande 18,000 vya takataka vyenye ukubwa unaozidi sentimita 10 vinavyoelea angani. Hata hivyo, takataka yenye ukubwa wa njegere inayosafiri kwa mwendo wa vyombo vinavyozunguka angani, inaweza kusababisha madhara makubwa inapogongana na setilaiti au hata chombo cha angani kinachoendeshwa na mwanadamu.
Vifaa Vinavyozuia Gari Lisiende
“Watu hulipa pesa wanazodaiwa na kampuni za simu za mkononi, kwa sababu wanajua kuwa simu zao zitaacha kufanya kazi wasipofanya hivyo,” linaripoti gazeti The Wall Street Journal. Sasa kanuni hiyo inatumika kwa magari. “Wauzaji wa magari yaliyotumika wanatia vifaa vya kuzuia gari lisiwake ikiwa mnunuzi hatamaliza malipo katika muda waliokubaliana,” linasema gazeti hilo. Vifaa hivyo huunganishwa kwenye mfumo wa kuwasha gari, navyo hutajwa kwenye mkataba wa kununua gari kwa mkopo kwa ajili ya watu wasio na uwezo wa kulilipia. Vifaa hivyo huondolewa malipo yanapokamilika. Jarida hilo linasema kwamba ni mara chache sana ambapo vifaa hivyo huzuia gari lisiende kwa kuwa “mnunuzi husukumwa akalipe kwa wakati” mara tu anapoona taa na milio ya kumwonya.