Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Tukawatembelee Sokwe Msituni

Tukawatembelee Sokwe Msituni

Tukawatembelee Sokwe Msituni

TUNAPOTEMBEA kwenye kijia chembamba katika msitu kwenye ikweta ya Afrika, polepole macho yetu yanaanza kuzoea mmweko unaopenya katikati ya majani na matawi mengi yaliyoshikana. Tunastaajabishwa na kelele za nyenje na miti mikubwa iliyofunikwa kwa mimea inayotambaa—ambayo mingine ina urefu wa mita 55. Tunahisi kwamba tunapaswa kutembea tukiwa chonjo bila kelele katika eneo hilo lisilo na mwangaza mwingi. Ghafula tunasikia sauti kubwa ikisema huu, ikifuatiwa na mlio wa kuhema. Kelele ya sauti hizo inazidi kuongezeka na kuwa kubwa sana halafu inakatika mara moja. Tumefika mwisho wa matembezi yetu kwa kuwa tumepata kikundi cha sokwe.

Sokwe huwasiliana au kuita wenzao kwa kutumia sauti kama ile tuliyosikia, kwa kupiga mayowe, na nyakati nyingine kwa kupigapiga shina la mti. Kupatikana kwa tini tamu zilizoiva ndiko kumetokeza kelele hizo tulizosikia sokwe walipokuwa wakiitana. Tunapotazama juu kwenye mtini huo mrefu, tunaona sokwe wengi, labda 20 au 30, wakila tini kwa amani. Manyoya yao meusi yanametameta yanapopigwa na jua. Mmoja wa sokwe hao anaanza kuturushia vijiti, hilo linaonyesha wazi kwamba haturuhusiwi kuonja tini hizo.

Wakati unaofaa zaidi wa kuwaona sokwe ni wakati ambapo kuna matunda mengi. Nyakati nyingine, ni vigumu sana kuwaona kwa kuwa wanaweza kuwa wametawanyika vichakani katika vikundi vidogo. Mara nyingi sokwe wakiwa msituni, wao hufurahia kula siku nzima kwa kuwa wanasafiri mbali sana. Mbali na matunda, chakula cha sokwe ni majani, mbegu, na mashina. Pia wao hula chungu, mayai ya ndege, na mchwa. Mara kwa mara wao huwinda na kuua wanyama wadogo kutia ndani ngedere.

Kwa kuwa inakaribia saa sita mchana, sokwe wanaanza kuhisi kuwa kuna joto kali. Mmoja wao anaanza kuteremka chini, na baada ya muda mfupi wengine wanafanya vivyo hivyo. Kisha, mmoja baada ya mwingine, wanaingia kichakani. Sokwe mmoja mtundu wa kiume anaruka kutoka tawi moja hadi lingine ili atutazame vizuri. Inafurahisha sana kumtazama mnyama huyo mdadisi anayechezacheza.

Sifa Zenye Kuvutia

“Hebu tazama nyuma,” anasema mtu fulani kwenye kikundi chetu tunapoanza kurudi. Tunapogeuka, tunamwona sokwe akituchungulia nyuma ya shina la mti. Amesimama kwa miguu miwili na ana urefu wa mita moja hivi. Tunapomtazama, anaficha kichwa chake nyuma ya mti huo, kisha anachungulia tena baada ya muda mfupi. Ni mdadisi kwelikweli! Sokwe wanaweza kusimama kwa miguu miwili na hata kutembea hivyo kwa mwendo mfupi. Hata hivyo, wao hutembea kwa miguu yote minne ili waweze kutegemeza uzito wao. Uti wa mgongo wa sokwe haujajipinda kwenye sehemu ya chini ya mgongo ili aweze kusimama kama wanadamu wanavyofanya. Kutembea kwa mikono na miguu, au kuruka na kubembea kwenye miti kunawafaa sokwe kwa kuwa misuli ya matako yao ni dhaifu na mikono yao ni mirefu na yenye nguvu kuliko miguu.

Sokwe wanapohitaji kufikia matunda yanayokua kwenye matawi membamba ambayo hayawezi kutegemeza uzito wao, wanatumia mikono yao mirefu pia. Mikono na miguu yao ina umbo linalofaa kabisa kuwawezesha kujishikilia kwenye matawi. Vidole vikubwa vya miguu ni kama vidole gumba navyo humsaidia sokwe kupanda miti au kushika na kubeba vitu kwa urahisi kwa miguu kama tu kwa mikono. Uwezo huo ni muhimu wakati wa kutengeneza kitanda usiku. Wao hukunja na kugeuza majani na matawi, na hivyo wanapata pahali pazuri pa kulala.

Unapowatazama sokwe msituni wanavutia kwa sababu ya sifa zao zenye kupendeza na wanafanana na wanadamu katika umbo na tabia. Hata hivyo, watu wengine hupendezwa na sokwe kwa sababu tu wanataka kuwafanyia utafiti utakaounga mkono hoja zao za kwamba mwanadamu alitokana na sokwe. Hivyo, maswali yafuatayo huzuka: Ni nini huwafanya wanadamu kuwa tofauti kabisa na sokwe? Tofauti na wanyama, ni katika njia gani wanadamu waliumbwa kwa “mfano wa Mungu”?—Mwanzo 1:27.

Safari Ambayo Hatutaisahau

Si rahisi kuwaona sokwe msituni kwa kuwa wao hujificha wanapowaona wanadamu. Hata hivyo, ili kuwalinda na kuwahifadhi, sokwe fulani wamezoezwa kutowaogopa wanadamu.

Hatutasahau safari yetu fupi ya kuwatembelea sokwe msituni. Imetusaidia kujifunza kuwahusu sokwe wakiwa katika mazingira yao ya asili tofauti kabisa na wale walio katika hifadhi za wanyama au maabara. Sokwe ni wanyama wenye kupendeza nao ni kati ya ‘wanyama wanaotambaa na wanyama-mwitu wa dunia’ ambao Mungu aliumba. Mungu alipotazama aliona kuwa kila kitu ni chema kwa kuwa kilifaa katika mazingira aliyokuwa ameumba.—Mwanzo 1:24, 25.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 14, 15]

SOKWE NA MWANADAMU

Katika kitabu chake In the Shadow of Man, mtaalamu wa viumbe Dakt. Jane Goodall aliandika kwamba katika miaka ya 1960 alipowachunguza sokwe ambao “wanatengeneza vifaa . . . alifaulu kuwasadikisha wanasayansi kadhaa kwamba ingefaa kuwaona wanadamu kuwa viumbe tata zaidi kuliko walivyofikiri zamani.” Ilishangaza sana kugundua kwamba sokwe hutumia majani kama godoro, mawe au matawi kuvunja kokwa, na kuchana majani kutoka kwa kijiti ili kuwatoa mchwa ndani ya kilima chao. Hata hivyo, katika nyakati za kisasa imekuwa wazi kwamba wanyama wengi wana ustadi wa ajabu wa kutengeneza vifaa. Dakt. T. X. Barber ambaye aliandika kitabu The Human Nature of Birds—A Scientific Discovery With Startling Implications, anasema hivi: “Wanyama wote ambao wamechunguzwa kwa undani, si sokwe na pomboo tu, bali pia chungu na nyuki, wameonyesha kwamba wanajifahamu na wanatumia akili inayotumika.”

Bado mwanadamu ni mtu wa kipekee. Profesa David Premack aliandika hivi: “Sarufi au muundo wa sentensi ya lugha ya wanadamu ni ya kipekee sana.” Kwa kweli utata wa lugha ya wanadamu kutia ndani tamaduni zao ambazo hasa zinatokezwa na lugha na usemi zinaonyesha wazi kwamba wanadamu ni tofauti na wanyama.

Baada ya kufanya utafiti kwa miaka kadhaa akiwachunguza sokwe msituni, Dakt. Jane Goodall aliandika hivi: “Siwezi kuwazia sokwe wakiwaonyesha wenzao hisia ambazo zinaweza kulinganishwa na upendo wa wanadamu ambao huonyeshwa kwa undani na hisia ya wororo, kuwalinda wenzao, kuvumiliana, na kuridhika.” Pia aliandika hivi: “Mwanadamu ana uwezo mkubwa wa kujitambua kuliko ule wa wanyama. Mwanadamu anatamani sana kujua jinsi alivyotokea na kuuelewa ulimwengu wa ajabu unaomzunguka.”

Biblia inaeleza tofauti iliopo kati ya wanyama na wanadamu inaposema kwamba mwanadamu aliumbwa “kwa mfano Mungu.” (Mwanzo 1:27) Hivyo, tofauti na wanyama mwanadamu huonyesha sifa kama za Muumba, sifa kuu ikiwa upendo. Mwanadamu pia ana uwezo wa kujifunza mambo mengi na kutumia akili kwa njia inayopita ile ya wanyama. Pia mwanadamu aliumbwa akiwa na uwezo wa kutenda kulingana na uhuru wake wa kuchagua, na si kwa kuongozwa na silika tu.

[Picha katika ukurasa wa 15]

Sokwe ni wanyama wadadisi na wanaopenda kucheza na walioumbwa kulingana na mazingira yao

[Hisani]

Chimpanzees, top right: Corbis/Punchstock/Getty Images; lower left and right: SuperStock RF/SuperStock; Jane Goodall: © Martin Engelmann/age fotostock

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 13]

© Photononstop/SuperStock