Kuutazama Ulimwengu
Kuutazama Ulimwengu
Kulingana na uchunguzi mmoja, asilimia 10.3 hivi ya wanaume Wabrazili wanaofanya ngono walio na umri wa kati ya miaka 15 hadi 64 wamefanya ngono na angalau mtu mmoja waliyekutana naye kwenye Intaneti katika miezi 12 iliyopita.—WIZARA YA AFYA YA BRAZILI.
Kwa muda mrefu sana Bahari ya Aktiki ilikuwa imefunikwa kwa miamba mikubwa ya barafu yenye upana wa mita 80 hivi. Sasa “miamba hiyo . . . inakaribia kuyeyuka kabisa, jambo la kushangaza ambalo litafanya iwezekane kwa meli kupitia katika maeneo hayo.”—SHIRIKA LA HABARI LA REUTERS, KANADA.
Moscow na Vatikani wametangaza kwamba wataanzisha uhusiano wa kidiplomasia kati yao.—RIA NOVOSTI, URUSI.
Mlima Kilimanjaro ambao ndio mlima mrefu zaidi barani Afrika, “umepoteza asilimia 26 ya barafu yake kati ya mwaka 2000 hadi 2007.”—DAILY NATION, KENYA.
Wenye Ubinafsi Lakini Wameshuka Moyo
Kulingana na watafiti, Waingereza “ndio watu wenye ubinafsi zaidi ulimwenguni, jamii inayokazia faida za kibinafsi kuliko za watu wengine,” linaripoti gazeti Daily Telegraph la London. Uchunguzi mwingine ulionyesha kwamba Waingereza wanapatwa na viwango vya juu vya kushuka moyo na mahangaiko. Wataalamu fulani wanaamini kwamba mambo hayo mawili yanahusiana. Utafiti fulani ulilinganisha jamii mbalimbali, kama zile zinazopatikana katika nchi za Ulaya, na zile za China na Taiwan. Ilionekana kwamba kwa kuwa jamii za China na Taiwan zinakazia ushirikiano katika jamii badala ya ubinafsi, watu wanalindwa wasipatwe na matatizo ya kiakili. Katika nchi za Ulaya, “jamii yenye ubinafsi . . . inatufanya tushuke moyo,” linasema gazeti Telegraph.
Ndoa za Watu wa Jinsia Moja Katika Kanisa la Kilutheri la Sweden
Mnamo Oktoba 2009, Kanisa la Kilutheri la Sweden liliidhinisha kwamba harusi za watu wa jinsia moja zinaweza kufanyiwa kanisani. Uamuzi huo ulifikiwa baada ya bunge la Sweden kupitisha sheria ya kukubali ndoa za jinsia zote miezi kadhaa mapema. “Hilo linamaanisha kwamba Kanisa [la Kilutheri] la Sweden ni moja kati ya makanisa ya kwanza makubwa ulimwenguni kukiuka maoni ya kitamaduni kwamba ndoa ni kifungo kati ya mwanamume na mwanamke,” linasema gazeti Dagens Nyheter.
Watoto Hulia Katika Lugha Gani?
Kulingana na watafiti katika Chuo Kikuu cha Würzburg, Ujerumani, siku mbili hivi baada ya kuzaliwa, watoto hulia katika lugha ya mama. Watafiti hao walirekodi vilio vya watoto 30 Wafaransa na watoto 30 Wajerumani, wakachunguza mawimbi, upatano wa kimelodia, na sauti. Kwa kawaida, vilio vya watoto Wafaransa vilianza kwa sauti ya chini kisha sauti ikapanda, huku vilio vya watoto Wajerumani vilianza kwa sauti ya juu kisha vikashuka. Katika visa vyote viwili, watoto waliiga upatano wa kimelodia wa lugha ya wazazi. Kwa hiyo, inaaminika kwamba watoto huanza kujifunza lugha wakiwa katika tumbo la uzazi na kuizungumza wanapoanza kulia.