Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Ustadi wa Kuchimba wa Chaza

Ustadi wa Kuchimba wa Chaza

Je, Ni Kazi ya Ubuni?

Ustadi wa Kuchimba wa Chaza

● Ingawa anaonekana kuwa hana nguvu za kuchimba kwenye mchanga, chaza anayeitwa razor (wembe) anaweza kuchimba mchanga mgumu upesi sana hivi kwamba ameitwa “Ferrari ya wachimbaji wa chini ya maji.” Watafiti walishangazwa sana. “Tulijua kwamba wanafanya jambo fulani lenye kustaajabisha,” akasema Anette Hosoi, profesa katika Taasisi ya Teknolojia ya Massachusetts. Ni nini siri ya chaza huyo?

Fikiria hili: Chaza huyo huingiza mguu wake mchangani na kuuzungusha kama skurubu na kufanyiza kitu kama kifuko ambacho hujaa maji na mchanga upesi. Kisha chaza huyo husogeza mwili wake juu chini huku akifungua na kufunga koa lake. Hilo hufanya kuwe na mchanganyiko wenye majimaji ambao chaza anaweza kuchimbua kwa urahisi. Chaza huyo anaweza kuchimba shimo lenye kina cha sentimita 70 hivi kwa mwendo wa sentimita 1 kwa sekunde. Chaza huyo akichimba na kuingia, ni vigumu sana kumvuta nje. Kwa kweli, unapofikiria nguvu anazotumia kuchimba pamoja na nguvu anazotumia kujishikilia mchangani, chaza huyo ana uwezo mara kumi zaidi ya nanga bora zaidi zilizotengenezwa na mwanadamu.

Mainjinia wamechochewa na chaza huyo ili kubuni nanga yenye uwezo kama wake. Nanga hiyo “inafunguka na kufunga, inasonga juu na chini, kama chaza anavyofanya,” anasema Hosoi. Nanga kama hiyo iliyo na nguvu na isiyotumia nishati nyingi inaweza kutumika sana katika vyombo vya chini ya maji vya kufanyia utafiti, visima vya mafuta vilivyo baharini, na vifaa vya kuchimba vinavyotumiwa kuharibu mabomu yaliyotegwa chini ya ardhi.

Una maoni gani? Je, ustadi wa kuchimba wa chaza anayeitwa razor ulijitokeza wenyewe? Au ulibuniwa?

[Picha katika ukurasa wa 23]

Muundo huu ni wa nanga inayotumia mbinu ya kuchimba ya chaza

[Hisani]

Razor clams: © Philippe Clement/naturepl.com; “smart” anchor: Courtesy of Donna Coveney, Massachusetts Institute of Technology