Unaweza Kuboresha Afya Yako
Unaweza Kuboresha Afya Yako
RUSTAM, anayeishi Urusi ana maisha yenye shughuli nyingi sana. Zamani alikuwa na mazoea yasiyofaa, lakini akagundua kwamba yanaathiri afya yake. Aliacha kuvuta sigara na kunywa kileo kupita kiasi. Lakini bado alijihisi akiwa mchovu sana baada ya kufanya kazi siku nzima mbele ya kompyuta yake.
Ingawa Rustam alianza kazi saa mbili asubuhi, alijihisi ni kana kwamba bado hajaamka hadi saa nne asubuhi, na alikuwa mgonjwa mara kwa mara. Kwa sababu hiyo, alifanya mabadiliko katika ratiba yake. Matokeo yakawa nini? Anasema hivi: “Katika muda wa miaka saba iliyopita, sijakosa kazi kwa zaidi ya siku mbili kwa mwaka kwa sababu ya ugonjwa. Ninajihisi nikiwa mzima kabisa—nikiwa macho na makini—na ninafurahia maisha!”
Ram, mke wake, na watoto wao wawili wanaishi Nepal. Eneo wanaloishi si safi na limejaa mbu na nzi. Zamani, Ram na familia yake waliugua mara kwa mara kutokana na magonjwa ya mfumo wa kupumua na maambukizo ya macho. Wao pia walifanya mabadiliko ambayo yaliboresha sana afya yao.
Chukua Hatua za Kuboresha Afya Yako!
Iwe mtu ni tajiri au maskini, watu wengi hawaoni jinsi mazoea yao yanavyoathiri afya yao. Wao huona kwamba wanaweza kuwa na afya nzuri bila jitihada zozote. Maoni hayo yasiyofaa huwafanya watu wengi wasijitahidi kuboresha afya yao na kuishi maisha yenye kuridhisha.
Kwa kweli, uwe tajiri au maskini, kuna mambo ya msingi unayoweza kufanya ili kulinda na kuboresha afya yako na ya familia yako. Je, kuna faida zozote za kujitahidi kufanya hivyo? Bila shaka! Unaweza kuboresha maisha yako na kuepuka kuyafupisha.
Kwa maneno na matendo, wazazi wanaweza kuwafundisha watoto wao kuwa na mazoea mazuri, na hilo litawasaidia kuwa na afya nzuri. Hata ikiwa watatumia wakati na pesa kufanya hivyo, faida ni kwamba watapunguza kuteseka, watapunguza wakati unaopotea kutibu ugonjwa, na hawatatumia pesa nyingi kulipia gharama za matibabu. Kuna msemo unaosema, Heri kuzuia kuliko kuponya.
Katika habari zinazofuata, tutazungumzia njia tano za msingi ambazo zimewasaidia Rustam, Ram, na wengine wengi. Njia hizo zinaweza kukusaidia wewe pia!
[Picha katika ukurasa wa 3]
Rustam
[Picha katika ukurasa wa 3]
Ram na familia yake wakiteka maji safi ya kunywa