Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kitabu Domesday—Ukaguzi wa Kipekee

Kitabu Domesday—Ukaguzi wa Kipekee

Kitabu Domesday​—Ukaguzi wa Kipekee

William, dyuki wa Normandy (eneo fulani nchini Ufaransa), alishinda Uingereza mwaka wa 1066. Miaka 19 baadaye, aliamuru milki yake mpya ikaguliwe. Ukaguzi huo uliandikwa katika kitabu kinachoitwa Domesday. Kwa nini kitabu hicho ni mojawapo ya rekodi muhimu zaidi za kihistoria nchini Uingereza?

WILLIAM alifika karibu na mji wa Hastings, Uingereza mnamo Septemba 1066. Oktoba (Mwezi wa 10) 14, alishinda jeshi la Mfalme Harold wa Uingereza, na akamuua. Siku ya Krismasi mwaka wa 1066, William ambaye baadaye alikuja kuitwa Mshindi, alitawazwa kuwa mfalme huko Westminster Abbey, London. Waingereza wangekuwa na maisha ya aina gani chini ya mtawala huyo mpya?

Ukaguzi Mkuu

Mfalme William wa Kwanza aliharibu kabisa eneo kubwa lililoko kaskazini mwa nchi hiyo na kuliacha ukiwa. Trevor Rowley, aliyekuwa mkufunzi wa wafanyakazi wa Chuo Kikuu cha Oxford, anaandika hivi: “Hata inapolinganishwa na hali zenye ukatili zilizokuwapo nyakati hizo, ule uharibifu mkubwa aliosababisha katika maeneo ya Kaskazini (1068-1070) ulikuwa wa kinyama.” William alikumbwa na uasi wa mara kwa mara, na wanajeshi wake 10,000 hivi, waliishi katikati ya wakazi wenye chuki wapatao milioni mbili hivi. Watu wa Normandy hatimaye walijenga ngome zaidi ya 500 kote nchini—ngome maarufu zaidi ikiwa ile inayoitwa Mnara wa London.

Ilipofika Desemba 1085, miaka 19 baada ya shambulizi lake, William alikaa kwa siku tano pamoja na maofisa wa makao yake ya kifalme huko Gloucester, Uingereza, huku akipanga kufanya ukaguzi wa nchi yote isipokuwa mji wa London na ule wa Winchester. Mwanzoni mwa mwaka uliofuata, makamishna wa mfalme walitumwa wakati uleule mmoja kwenda kwenye maeneo yote saba ya majimbo kukusanya habari kutoka kwa wawakilishi wa majimbo hayo ili waweze kukadiria utajiri wa nchi.

Ilikuwa lazima mfalme atafute pesa za kuwalipa wanajeshi wake. Pia alihitaji kutatua mizozo ya umiliki wa ardhi. Kutimiza miradi hiyo kungehakikisha kwamba watu kutoka Normandy na maeneo mengine ya Ufaransa wangepata makao Uingereza, na hivyo utawala wa Wanormani ungeendelea.

“Domesday”

Punde tu baada ya kuwashinda Waingereza, Mfalme William aliwakabidhi Wanormani wenye vyeo mali zote za wakuu wa Uingereza. Ukaguzi alioufanya William ulifunua kwamba kufikia wakati huo, karibu nusu ya mali ya nchi yote ilikuwa mikononi mwa wanaume wasiozidi 200, na ni 2 tu kati yao waliokuwa Waingereza. Iliwabidi Waingereza 6,000 hivi waliokuwa wakipangisha ardhi walipe ili waweze kuishi kwenye ardhi waliyokuwa wamemiliki kihalali kabla ya mwaka wa 1066, ilhali waliokuwa maskini na wasio na makao walihitaji kutumia kila mbinu ili wakabiliane na hali hiyo.

Ukaguzi huo ulihalalisha unyakuzi wa mali wa Wanormani. Pia ukaguzi huo ulikadiria upya ushuru wa ardhi na wa umiliki wake, pamoja na misitu na maeneo yenye malisho. Pia, kila mnyama—ng’ombe-dume au wa kike, na hata nguruwe—walitiwa ndani ya ukaguzi huo. Waingereza waliokandamizwa walikuwa na wasiwasi sana kuhusu matokeo ya uchunguzi huo, kwa kuwa walijua kwamba hawangeweza kubadili chochote baada ya hapo. Walifananisha ukaguzi huo mkuu na “Siku ya Hukumu,” au “Siku ya Mabaya.” Ndiyo sababu kilikuja kuitwa Kitabu cha Siku ya Hukumu (Domesday Book).

Kitabu Domesday kilifanyizwa kwa mabuku mawili yaliyoandikwa katika Kilatini kwenye vipande vya ngozi. Buku moja lililoitwa Great Domesday, lilikuwa na karatasi kubwa 413 za ngozi, na Little Domesday lilikuwa na karatasi ndogo 475 za ngozi. * Kitabu hicho hakikuwa kimekamilishwa wakati William alipokufa mwaka wa 1087. Mambo hayo yote yalitimizwa kwa njia gani katika muda wa mwaka mmoja?

Wanormani walirithi rekodi za serikali ya Uingereza zilizokuwa na habari kuhusu wamiliki na waliopangisha mashamba, pamoja na rekodi kuhusu mambo ya kifedha na ya ushuru. Kwa msingi huo, Wanormani walikagua upya ushuru ambao watu walipaswa kutozwa kwa kuwatuma maafisa kwenye kila jimbo ili wakusanye habari.

Kitabu Hicho Leo

Wakati wa Enzi za Kati, mara nyingi familia ya kifalme ilisafiri na kitabu Domesday popote walipoenda. Mwanzoni kilitumiwa hasa kutatua mizozo kuhusu umiliki wa ardhi, ingawa katika karne ya 18, yule mwanasheria maarufu Sir William Blackstone alikirejezea ili kuthibitisha haki za kupiga kura za baadhi ya watu waliokuwa wamekodi ardhi. Kimekuwa kwenye hifadhi mbalimbali ingawa sasa kiko kwenye Hifadhi ya Nyaraka za Kitaifa nchini Uingereza.

Mnamo 1986, ili kuadhimisha miaka 900 tangu kitabu hicho kilipoandikwa, kilijalidiwa upya katika mabuku matano. Tafsiri iliyorekebishwa ya maandishi hayo katika Kiingereza inaweza kupatikana kwa ajili ya wanahistoria na wasomi wengine. Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) lilisema kwamba hiyo ndiyo “hati ya kwanza kuwekwa katika hifadhi ya nyaraka za kitaifa na . . . bado inatumika kuthibitisha umiliki wa ardhi.” Katika mwaka wa 1958, kilitumiwa kuthibitisha haki ya mji fulani wa kale kuwa na soko katika eneo lake.

Wataalamu wa vitu vya kale hukirejezea kitabu cha Domesday ili kutambua maeneo ambayo Waingereza na Wanormani wa Enzi za Kati waliishi. Katika njia ya pekee, kitabu hicho ni chanzo muhimu cha habari za msingi za kuchipuka kwa taifa la Uingereza.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 11 Buku la Great Domesday lilikuwa na orodha iliyofupishwa ya mali zinazoweza kutozwa ushuru, ilhali orodha ya Little Domesday haikufupishwa wala kuongezwa kwenye lile buku kubwa.

[Sanduku/​Picha katika ukurasa wa 23]

VITA VYA KIDINI VYA WILLIAM

William alimwomba papa akweze uvamizi aliokuwa akifanya uwe vita vya kidini, na akamwahidi kwamba angelifanya kanisa la Uingereza lililoasi lirudi chini ya udhibiti wa papa. Papa alikubali haraka. Hiyo ilikuwa “mbinu ya ujanja wa kidiplomasia” ya William, anaandika Profesa David C. Douglas. Mwanahistoria mwingine mashuhuri anayeitwa George M. Trevelyan, katika kitabu chake History of England, alisema kwamba “bendera na baraka kutoka kwa Papa ilikuwa yenye thamani sana kwa William hasa inapozingatiwa kwamba jambo alilokuwa akifanya lilionekana wazi kuwa wizi wa kimabavu badala ya pambano la kidini.”

[Hisani]

© The Bridgeman Art Library

[Ramani katika ukurasa wa 22]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

UINGEREZA

LONDON

Hastings

Mlango-Bahari wa Uingereza

NORMANDY

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 22]

Book: Mary Evans/The National Archives, London, England