Maporomoko ya Maji ya Murchison Nchini Uganda
Maporomoko ya Maji ya Murchison Nchini Uganda
“Hayo ndiyo maporomoko ya maji yenye kustaajabisha zaidi kwenye Mto Nile.”—Mvumbuzi Mwingereza, Sir Samuel White Baker.
MAPOROMOKO ya maji huwavutia na kuwapendeza watu wote. Sauti tulivu ya maji yakiigonga miamba iliyo chini na ukungu unaoinuka kutoka kwenye maporomoko hayo hufanya watalii wastarehe kwa saa kadhaa.
Hali huwa hivyo wanapotembelea Maporomoko ya Maji ya Murchison * nchini Uganda. Mto Nile una urefu wa kilomita zaidi ya 6,400, na watu wengine husema kwamba maporomoko hayo ndiyo sehemu yenye kuvutia zaidi ya mto huo. Ni kweli kwamba maporomoko hayo hayana urefu wa Maporomoko ya Angel huko Amerika Kusini wala hayana maji mengi kama Maporomoko ya Victoria, barani Afrika au Maporomoko ya Niagara, Amerika Kaskazini. Lakini mtu hawezi kusahau kwa urahisi umaridadi na nguvu za maji ya Maporomoko ya Maji ya Murchison.
Historia ya Maporomoko ya Maji ya Murchison
Maporomoko ya Maji ya Murchison ni mojawapo ya sehemu zenye kuvutia za eneo lenye ukubwa wa kilomita 3,841 za mraba linalofanyiza Mbuga ya Taifa ya Maporomoko ya Maji ya Murchison. Mbuga hiyo ambayo iko kaskazini magharibi mwa Uganda ilianzishwa mwaka wa 1952. Baker alitembelea maporomoko hayo mwanzoni mwa miaka ya 1860. Katika kitabu chake, The Albert N’yanza, anaeleza kuhusu mara yake ya kwanza kuona maporomoko hayo.
Aliandika hivi: “Tulipopiga kona fulani tuliona mandhari yenye kustaajabisha. . . . Maporomoko hayo ya maji yaliyokuwa meupe kama theluji, yalionekana maridadi sana kwenye majabali meusi yaliyo kando ya mto huo, huku mitende na migomba ya mwitu ikiongeza umaridadi wa eneo hilo. Hayo ndiyo maporomoko ya maji yenye kustaajabisha zaidi kwenye Mto Nile.” Mwanzoni Baker aliyaita maporomoko hayo Maporomoko ya Maji ya Murchison ili yawe kumbukumbu kwa aliyekuwa msimamizi wa Shirika la Kijiografia la Uingereza.
Njia Mbalimbali za Kuona Maporomoko Hayo
Unaweza kuona maporomoko hayo vizuri zaidi ukitumia mashua. Safari hiyo huanza kwenye kivuko cha Paraa na inawawezesha wageni kusafiri kwenye Mto Nile huku wakitazama wanyama mwitu wakiwa umbali
unaofaa. Unaweza kuona viboko na pia tembo wakubwa wa Afrika, mamba, na nyati. Wanyama hao maridadi wa Mto Nile wanaweza kumfanya mtu asahau kwa muda kwamba kusudi lake lilikuwa kutembelea maporomoko ya Murchison. Lakini mara anapofika kwenye maji hayo meupe kama theluji ambayo yanaonekana ni kana kwamba yanalipuka kutoka kwenye miamba, anaelewa sababu iliyomfanya Baker astaajabu.Ingawa watalii wengi hufurahia sana kuona maporomoko hayo wakiwa kwenye mashua, mandhari hiyo inavutia kwa njia ya pekee wanapoyatazama wakiwa mahali palipoinuka. Wengine wanaona hiyo kuwa ndiyo mandhari bora zaidi. Kutoka mahali hapo palipoinuka, mtu anaweza kuona Mto Nile wenye upana wa mita 49 ukijibana ili upitie kwenye kijia kilicho na upana wa mita 6 na kuporomoka kwa mita 40. Maporomoko hayo yametajwa kuwa “mojawapo ya maporomoko ya maji yenye nguvu zaidi ulimwenguni.” Nyakati nyingine watalii huhisi ardhi ikitetemeka wakati maji hayo yanapoteremka kwa nguvu kupitia kwenye korongo hadi chini.
Baker anaeleza mambo aliyowazia kabla ya kuona maporomoko hayo ya maji. Alisema kwamba alisikia kelele za ngurumo alipokuwa akitembea mapema asubuhi moja. Alidhani kwamba zilikuwa kelele za ngurumo kutoka mbali lakini akashangaa alipogundua kwamba zilikuwa zinatoka kwenye maporomoko hayo ya maji.
Kila mwaka, maelfu ya watu wanavutiwa sana na uzuri usio na kifani na nguvu za maporomoko hayo yenye kustaajabisha. Mtu hawezi kusahau upesi mandhari ya maji hayo yakiporomoka na kugonga chini kwa nguvu. Kwa kweli, Maporomoko ya Maji ya Murchison ni kivutio cha pekee cha Mto Nile.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 4 Yanajulikana pia kama Maporomoko ya Maji ya Kabalega au Kabarega.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 17]
Mbuga ya Taifa ya Maporomoko ya Maji ya Murchison
Hesabu iliyochukuliwa mwaka wa 1969 ilionyesha kwamba kulikuwa na viboko 14,000 hivi, tembo 14,500, na nyati 26,500 katika mbuga hiyo. Lakini katika makumi ya miaka iliyofuata, idadi ya wanyama hao ilianza kupungua sana. Hivi karibuni, kwa sababu ya jitihada zilizofanywa za kuwalinda wanyama hao, idadi yao imeanza kuongezeka. Sasa, kwenye msitu wa mbuga hiyo kuna aina nyingi za nyani kama vile sokwe-mtu, na katika maeneo tambarare yenye malisho kuna twiga na kongoni wanaoitwa Jackson. Zaidi ya spishi 70 za mamalia na zaidi ya spishi 450 za ndege zimegunduliwa katika mbuga hiyo.
[Hisani ya picha katika ukurasa wa 16]
All photos pages 16 and 17: Courtesy of the Uganda Wildlife Authority