Kuutazama Ulimwengu
“Mwanzoni mwa mwaka wa 2011, kulikuwa na wateja bilioni 5.4 ulimwenguni pote wa simu za mkononi.”—UN CHRONICLE, MAREKANI.
Kwa kipindi cha miaka kumi iliyopita, “misiba ya asili imesababisha vifo vya zaidi ya watu 780,000, na karibu asilimia 60 ya vifo vyote hivyo vimesababishwa na matetemeko ya nchi.”—THE LANCET, UINGEREZA.
“Katika kipindi cha miaka 20 iliyopita, karibu watu 800,000 nchini Urusi wamejiua.”—ROSSIISKAYA GAZETA, URUSI.
Nchini Filipino, ambako talaka haikubaliwi kisheria, idadi ya wanawake wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 49 wanaoishi pamoja na “wenzi ambao hawajafunga ndoa nao . . . , imeongezeka zaidi ya mara mbili kati ya mwaka wa 1993 na 2008.”—THE PHILIPPINE STAR, FILIPINO.
Katika Jamhuri ya Georgia, “asilimia 79.2 ya watu wameathiriwa . . . na moshi unaotolewa na wavuta sigara.” Kwenye mji mkuu, Tbilisi, “asilimia 87.7 ya watoto wameathiriwa.”—TABULA, GEORGIA.
Kutalii Ili Kutafuta Matibabu Huko Asia
Watu wengi zaidi kutoka sehemu mbalimbali za ulimwengu wanasafiri kwenda nchi za ng’ambo ili kupata matibabu bora, mara nyingi kwa gharama ndogo ikilinganishwa na kiwango ambacho wangelipa wakiwa katika nchi za kwao. Gazeti Business World linasema kwamba kufikia mwaka wa 2015, idadi ya ‘watalii’ ambao wanatarajiwa nchini Filipino itafikia zaidi ya milioni moja kwa mwaka, na idadi kama hiyo pia inatarajiwa huko Korea Kusini kufikia mwaka wa 2020. Nchi nyingine pia kama vile India, Malasia, Singapore, na Thailand ni maarufu kwa watalii wa aina hiyo. Si watu kutoka nchi za Magharibi pekee ambao hutembelea huko ili kupata matibabu kama vile ya mifupa na ya moyo. Wachina wengi pia ambao wamekuwa matajiri hivi karibuni wanaenda huko ili kutafuta huduma kwenye vituo vya upasuaji wa kurekebisha maumbile wakiwa na “picha za watu maarufu ambao wangependa kufanana nao,” inasema taarifa hiyo.
Wanaofanya Mambo Kadhaa kwa Wakati Mmoja Hawafaulu
Mara nyingi, maendeleo katika teknolojia yanawafanya wafanyakazi kushughulikia mambo mawili au zaidi kwa wakati uleule na kujibu maswali upesi. Hata hivyo, “wafanyakazi wanaofanya mambo kadhaa kwa wakati mmoja hawayafanyi kwa njia inayofaa,” anasema Clifford Nass, mkurugenzi wa Mawasiliano ya Wanadamu na Matumizi ya Vifaa vya Kielektroniki katika Chuo Kikuu cha Stanford, Marekani. Inasemekana kwamba watu wanaofanya mambo kwa njia hiyo mara nyingi huwa na mkazo, wanakengeushwa na mambo yasiyo muhimu, hawafikiri kwa kina na kwa sababu hiyo hawafanyi mambo kwa umakini. Nass anapendekeza hivi: “Unapoanza kufanya jambo fulani, lifanye kwa muda wa dakika 20 bila kufanya jambo lingine lolote. Kufanya hivyo kutakuzoeza kukaza fikira na kufikiri kwa kina.”