Sand Cat Paka Asiyeonekana kwa Urahisi
KATIKATI kabisa mwa jangwa, paka anayeitwa sand cat (yaani paka anayeishi mchangani) anatoka kwenye pango lake usiku wa manane kisha anasimama. Anatazama huku na huku na kusikiliza. Kisha, akiwa amechutama, anaanza kutembea kwenye mchanga kimyakimya.
Kwa ghafula, paka huyo anamrukia na kumkamata bukunyika anayeitwa gerbil. Baadaye, anaendelea kuwinda usiku wote huku akiruka hewani mara kwa mara ili kuwakamata wanyama wengine. Akishindwa kumaliza kula windo lake, paka huyo atafukia nyama inayosalia mchangani. Kisha anarudi kwenye pango lake mapema asubuhi na ni vigumu sana kumwona wakati wa mchana. Fikiria mambo fulani yenye kupendeza kuhusu mnyama huyo asiyeonekana kwa urahisi:
Uwezo mkubwa wa kusikia wa sand cat huwasaidia kupata mawindo, hata mnyama anapokuwa chini ya ardhi
Paka wa kiume wa jamii hii hutoa sauti ya juu kana kwamba wanabweka ili kuwavutia paka wa kike. Kwa sababu wana uwezo mkubwa wa kusikia, paka wa kike wanaweza kusikia sauti hiyo wakiwa mbali sana
Manyoya yaliyo chini ya miguu ya paka huyo humzuia asizame kwenye mchanga na pia humzuia asiunguzwe na joto kali la mchanga
Upande wa ndani wa masikio yake umefunikwa kwa manyoya meupe, ambayo huzuia mchanga usiingie
Ni vigumu sana kufuata nyayo za paka huyo kwa kuwa miguu yake imefunikwa kwa manyoya mengi
Sand cat wanaweza kuendelea kuishi kwa kutegemea tu maji wanayopata katika miili ya wanyama wanaowakamata
Kiwango cha joto cha mchanga ulio katika Jangwa la Kara-Kum kinaweza kufikia nyuzi 80 Selsiasi. Lakini nyakati nyingine kiwango cha joto kinaweza kushuka na kufikia nyuzi 25 Selsiasi chini ya sufuri