Walivyoishi Nyumba Zao
Wakristo wa Karne ya Kwanza
Walivyoishi Nyumba Zao
“Sikuepuka . . . kuwafundisha ninyi hadharani na nyumba kwa nyumba.”—MATENDO 20:20.
UNAPITA lango kubwa sana, na mara moja unaingia katika jiji la karne ya kwanza. Kama majiji mengine mengi, jiji hili limejengwa juu ya kilima. Kwenye upande wa juu wa jiji hili unaona nyumba nyingi nyeupe za kifahari zinazometameta kwenye jua. Nyumba hizi ni za matajiri na nyingi zina bustani zilizozungukwa kwa ua. Chini kidogo, unaona nyumba zenye ukubwa na miundo tofauti-tofauti. Nyumba hizi zenye orofa nyingi ambazo zimejengwa kwa mawe kandokando ya barabara, ni za wafanyabiashara na wamilikaji wa ardhi ambao si matajiri sana. Chini bondeni, unapata nyumba za maskini. Eneo hili lina nyumba ndogo zinazofanana na sanduku ambazo hazivutii sana. Zimejengwa karibu-karibu kuzunguka nyua ndogo.
Unapotembea kwenye barabara zenye watu wengi za eneo hili, sauti na harufu mbalimbali zinavuta fikira zako kwenye shughuli tofauti-tofauti zinazoendelea hapo. Wanawake wanapika na harufu zenye kutamanisha zimejaa hewani. Unasikia sauti za wanyama na za watoto wakicheza. Wanaume nao wanafanya kazi katika karakana zenye kelele na harufu mbaya.
Familia nyingi za Wakristo ziliishi katika nyumba kama hizo. Ibada, mafundisho ya dini, na shughuli za kila siku zilifanywa katika nyumba hizo.
Nyumba Ndogo Kama ilivyo leo, aina ya nyumba na ukubwa wake ulitegemea mahali ilipojengwa na hali ya kifedha ya familia iliyoijenga. Nyumba zilizokuwa ndogo zaidi (1) zilikuwa zenye chumba kimoja tu chenye giza ambamo familia nzima iliishi. Nyumba nyingi ndogo zilijengwa kwa matofali ya udongo yaliyokaushwa juani. Nyingine zilijengwa kwa mawe yasiyochongwa vizuri. Mara nyingi, nyumba za aina hizi mbili zilijengwa juu ya msingi wa mawe.
Nyumba hizo zilihitaji kukarabatiwa wakati wote kwa kuwa zilikuwa na sakafu ya mawe, na upande wa ndani wa kuta zake ulipigwa plasta. Nyumba hizo zilikuwa na shimo dogo la kutolea moshi kwenye paa au ukuta. Hazikuwa na vitu vingi isipokuwa vifaa muhimu vya matumizi ya nyumbani.
Paa la nyumba hizo lilitengenezwa kwa udongo uliowekwa juu ya matawi ya miti na matete, na lilitegemezwa kwa nguzo za mbao. Upande wa ndani wa paa ulipigwa plasta na hilo lilifanya lisivuje maji. Mtu alihitaji ngazi ya nje ili kupanda juu ya paa hilo.
Licha ya msongamano, nyumba za Wakristo zilikuwa makao yenye kupendeza, kwa kuwa hata familia maskini zilizoishi katika nyumba hizo zingeweza kuwa tajiri kiroho na zenye furaha.
Nyumba za Watu Wasio Matajiri Sana Watu wasio matajiri sana walijenga nyumba za mawe za orofa moja (2) ambazo zilikuwa na chumba cha juu cha wageni. (Marko 14:13-16; Matendo 1:13, 14) Chumba hiki kilikuwa kikubwa na kingeweza kutumiwa kwa ajili ya mikutano na mara nyingi kilitumiwa kwa ajili ya sherehe. (Matendo 2:1-4) Nyumba hizi na hata nyumba nyingine kubwa (3) za wafanyabiashara na wamilikaji wa ardhi zilijengwa kwa mawe ya chokaa yaliyounganishwa kwa mchanganyiko wa chokaa na udongo. Sakafu za mawe na upande wa ndani wa kuta ulipigwa plasta; nao upande wa nje wa kuta ulipakwa rangi nyeupe.
Kulikuwa na ngazi ya kupandia kwenda katika vyumba vya juu au kwenye paa. Mapaa yote tambarare yalikuwa na ukuta wa ukingoni wa kumzuia mtu asianguke au asipatwe na misiba mingine. (Kumbukumbu la Torati 22:8) Wakati wa joto la mchana, lingekuwa jambo lenye kufurahisha kuketi kwenye paa chini ya kivuli cha kibanda ili kusoma, kutafakari, kusali, au kupumzika.—Matendo 10:9.
Ingawa mara nyingi wenye nyumba walikaribisha watu wa ukoo kukaa nao, nyumba hizi imara zenye vyumba vikubwa zilikuwa na nafasi ya ziada ya kukaa, vyumba vya kulala, na chumba kikubwa cha kupikia na cha kulia chakula.
Nyumba za Kifahari Zaidi Nyumba hizi zilizojengwa kwa mtindo wa Waroma (4) zilitofautiana sana kwa ukubwa na jinsi zilivyojengwa. Zilikuwa na vyumba vilivyojengwa kuzunguka chumba kikubwa cha kulia chakula, ambapo shughuli nyingi za familia zilifanywa. Baadhi ya nyumba hizi zilikuwa na orofa moja au mbili (5) au zilikuwa na bustani maridadi zilizozingirwa kwa ukuta.
Yaelekea nyumba zilizokuwa za kifahari zaidi zilikuwa na vitu vya hali ya juu, vingine vikiwa vimepambwa kwa pembe za ndovu na dhahabu. Matendo 20:9, 10.
Nyumba hizi zilikuwa na maji ya bomba na bafu. Huenda sakafu zilitengenezwa kwa mbao au mawe ya marumaru ya rangi mbalimbali, nazo kuta zilifunikwa kwa mbao za mwerezi. Majiko ya makaa ya mawe yalitumiwa kupashia nyumba joto. Viunzi ambavyo kwa kawaida vilitengenezwa kwa mbao viliwekwa kwenye dirisha kwa ajili ya usalama, nayo mapazia yaliwapa watu kiasi fulani cha faragha. Viti vya dirishani vilikatwa kwenye kuta pana za mawe.—Hata nyumba zao ziwe zilikuwa na ukubwa au muundo wa aina gani, Wakristo wa karne ya kwanza walikuwa wakarimu sana. Waangalizi wanaosafiri hawakuwa na tatizo la kupata familia yenye upendo na ukarimu ambayo ingewakaribisha wakae nyumbani mwao wakati wote wa huduma yao katika jiji au mji wao.—Mathayo 10:11; Matendo 16:14, 15.
“Nyumba ya Simoni na Andrea” Yesu alikaribishwa vizuri katika “nyumba ya Simoni na Andrea” iliyokuwa Kapernaumu, karibu na Bahari ya Galilaya. (Marko 1:29-31) Huenda nyumba ya wavuvi hawa ilikuwa mojawapo ya nyumba za hali ya chini (6) zilizojengwa karibu-karibu kuzunguka ua wa mawe.
Katika nyumba hizo milango na dirisha zilielekea ua, ambapo watu walifanyia shughuli zao za kila siku kama vile kupika, kuoka, kusaga nafaka, kuzungumza na marafiki, na kula.
Nyumba hizo jijini Kapernaumu zilijengwa kwa mawe ya volkano yasiyochongwa. Upande wa nje kulikuwa na ngazi zilizoelekea kwenye paa tambarare. Paa hilo lilitengenezwa kwa udongo au vigae, ambavyo viliwekwa juu ya matete na maboriti yaliyotegemezwa kwa nguzo za mbao. (Marko 2:1-5) Sakafu zilikuwa zimetengenezwa kwa mawe na mara nyingi zilifunikwa kwa mikeka iliyofumwa.
Nyumba zilizokuwa karibu na Bahari ya Galilaya zilijengwa karibu-karibu, na katikati ya nyumba hizo kulikuwa na barabara na vijia. Kapernaumu lilikuwa eneo zuri kwa wavuvi ambao walipata riziki yao kwa kuvua samaki baharini.
“Nyumba kwa Nyumba” Kwa ufupi, Wakristo wa karne ya kwanza waliishi katika nyumba aina tofauti-tofauti. Baadhi yao waliishi katika nyumba zenye chumba kimoja zilizojengwa kwa matofali ya udongo, na wengine katika nyumba kubwa na za kifahari zilizojengwa kwa mawe.
Familia hazikutumia nyumba hizo kama mahali pa kuishi tu. Zilikuwa pia mahali pa kujifunzia mambo ya kiroho. Familia iliabudu pamoja katika nyumba hizo. Zilikusanyika katika nyumba za watu binafsi ili kujifunza Maandiko na kufurahia ushirika pamoja na waamini wenzao. Mambo waliyojifunza katika nyumba zao waliyatumia walipoendelea na kazi yao muhimu ya kuhubiri na kufundisha “nyumba kwa nyumba” katika milki yote ya Roma.—Matendo 20:20.