Jina la Mungu Lajulishwa Katika Kiswahili
“Kiswahili.” Watu wengi wanaposikia lugha hiyo ikitajwa wanakumbuka Afrika na wanyama wa porini wakitembea-tembea katika mbuga ya Serengeti. Hata hivyo, kuna mengi kuhusu lugha ya Kiswahili na watu wanaoizungumza.
KISWAHILI ni lugha inayozungumzwa na watu milioni 100 katika nchi karibu 12 zilizo Afrika ya kati na mashariki. * Ni lugha ya taifa au lugha rasmi katika nchi kadhaa, kama vile Kenya, Tanzania, na Uganda. Na kwa nchi zilizo karibu, watu wanazungumza Kiswahili wanapofanya biashara na wanapowasiliana.
Kiswahili kimesaidia sana katika kuunganisha watu wa Afrika Mashariki. Kwa mfano, nchini Tanzania pekee kuna makabila ya watu wanaozungumza angalau lugha 114 tofauti-tofauti. Hebu wazia ukisafiri kati ya kilomita 40 hadi 80 kutoka nyumbani kwako na unakutana na watu wanaozungumza lugha tofauti kabisa na lugha yako! Na katika sehemu nyingine, watu wanaozungumza lugha fulani wanaishi katika vijiji vichache vidogo-vidogo. Ungewasilianaje nao? Ni rahisi sasa kuelewa kwa nini ni jambo muhimu kuwa na lugha moja inayojulikana.
Historia ya Kiswahili
Inaaminika ya kwamba Kiswahili kimekuwa kikizungumzwa tangu karne ya kumi. Lugha hiyo ilianza kuandikwa katika karne ya 16. Watu wanaojifunza Kiswahili wanatambua kwamba baadhi ya maneno yana asili ya Kiarabu. Asilimia 20 ya maneno
ya Kiswahili yana asili ya Kiarabu, na asilimia inayobaki yana asili ya Kiafrika. Hivyo, haishangazi kwamba kwa mamia ya miaka Kiswahili kilikuwa kikiandikwa kwa herufi za Kiarabu.Leo, Kiswahili kinaandikwa kwa herufi za Kiroma. Ni nini kilichotokea? Kwa nini kuwe na badiliko hilo? Ili tupate jibu lazima turudi nyuma hadi katikati ya karne ya 19 wakati wamishonari wa kwanza kutoka Ulaya walipofika Afrika Mashariki, wakiwa na kusudi la kuwaeleza wenyeji ujumbe kutoka katika Biblia.
Neno la Mungu Lafika Afrika Mashariki kwa Mara ya Kwanza
Mnamo 1499, wakati wa safari inayojulikana sana ya Vasco da Gama ya kuzunguka ncha ya kusini mwa Afrika, wamishonari Wareno walianzisha dini ya Ukatoliki Afrika Mashariki kwa kujenga nyumba ya wamishonari katika kisiwa cha Zanzibar. Hata hivyo, katika kipindi cha miaka 200, wenyeji waliwafukuza Wareno pamoja na “Ukristo” kutoka katika eneo hilo.
Neno la Mungu lilihubiriwa tena katika Afrika Mashariki baada ya miaka 150. Pindi hiyo, ujumbe huo uliletwa na mmishonari Mjerumani, Johann Ludwig Krapf. Alipowasili Mombasa, Kenya, katika mwaka wa 1844, watu wengi walioishi kwenye pwani ya Afrika Mashariki walikuwa Waislamu, na wengi walioishi mbali na pwani walishikilia dini za kitamaduni za kuabudu mizimu. Krapf aliamini kwamba ni jambo muhimu kila mtu aweze kusoma Biblia.
Mara moja, Krapf alianza kujifunza lugha ya Kiswahili. Mwezi wa Juni 1844, muda mfupi baada ya kuwasili, alianza kazi ngumu ya kutafsiri Biblia. Jambo la kusikitisha ni kwamba mwezi uliofuata alipatwa na misiba mikubwa—mke wake ambaye walikuwa wamefunga ndoa kwa miaka miwili alikufa, na siku chache baadaye binti yake mchanga pia akafa. Hata ingawa alihuzunishwa na misiba hiyo, bado aliendelea na kazi muhimu ya kutafsiri Biblia. Katika mwaka wa 1847, sura tatu za kwanza za kitabu cha Mwanzo zilichapishwa na kuwa maandishi ya kwanza kuchapishwa katika Kiswahili.
Krapf alikuwa wa kwanza kutumia herufi za Kiroma katika kuandika Kiswahili badala ya herufi za Kiarabu zilizotumiwa na watu wengi. Kati ya sababu alizotoa za kutotumia herufi za Kiarabu ni kwamba “herufi za Kiarabu zingewatatanisha watu kutoka Ulaya” ambao baadaye wangejifunza lugha hiyo na pia “herufi za Kiroma zingewasaidia ‘Wenyeji katika kujifunza lugha za Ulaya.’” Herufi za Kiarabu ziliendelea kutumiwa kwa miaka mingi; sehemu fulani za Biblia zilichapishwa katika herufi
hizo. Hata hivyo, kutumia herufi za Kiroma kumewasaidia watu wengi wajifunze Kiswahili. Kwa sababu hiyo wamishonari wengi na wanafunzi wengine wa lugha ya Kiswahili wanafurahi kwamba badiliko hilo lilifanywa.Zaidi ya kuwa wa kwanza kutafsiri Neno la Mungu katika Kiswahili, Krapf aliweka msingi mzuri kwa ajili ya watafsiri wa baadaye. Aliandika kamusi na kitabu cha kwanza cha sarufi ya Kiswahili.
Jina la Mungu Katika Kiswahili
Katika nakala ya awali ya zile sura tatu za kwanza za kitabu cha Mwanzo, jina la Mungu lilitafsiriwa kuwa “Mungu Mweza Yote.” Hata hivyo, kuelekea mwishoni mwa karne ya 19, wanaume kadhaa waliwasili Afrika Mashariki na kuendeleza kazi ya kutafsiri Biblia nzima katika Kiswahili. Wanaume hao walikuwa Johann Rebmann, William Taylor, Harry Binns, Edward Steere, Francis Hodgson, na Arthur Madan.
Jambo la kupendekeza ni kwamba baadhi ya tafsiri hizo za mapema zilikuwa na jina la Mungu, si katika sehemu chache tu bali katika sehemu zote za Maandiko ya Kiebrania! Watafsiri waliokuwa Zanzibar walitafsiri jina la Mungu kuwa “Yahuwa,” ilihali watafsiri waliokuwa Mombasa walitafsiri kuwa “Jehova.”
Kufikia mwaka wa 1895 Biblia nzima ilikuwa inapatikana katika Kiswahili. Miongo kadhaa baadaye tafsiri nyingine zilichapishwa, ingawa baadhi ya tafsiri hizo hazikusambazwa sana. Mwanzoni mwa karne ya 20, jitihada nyingi zilifanywa ili kufanya Kiswahili cha Afrika Mashariki kilingane katika nchi zote. Jitihada hizo ziliwezesha Biblia tafsiri ya Union Version ichapishwe katika mwaka wa 1952. Hiyo ndiyo tafsiri iliyosambazwa zaidi. Pia, jitihada hizo zilifanya “Yehova” kuwa tafsiri iliyokubaliwa ya jina la Mungu katika Kiswahili.
Inasikitisha kwamba kadiri tafsiri hizo za kale zilivyoacha kuchapishwa, ndivyo jina la Mungu lilivyoacha kutumiwa. Baadhi ya watafsiri wa hivi karibuni wameondoa jina hilo kabisa, na wengine wameliacha katika sehemu kadhaa tu. Kwa mfano, katika tafsiri ya Union Version, jina la Mungu linapatikana mara 15 peke yake, na katika nakala ya mwaka wa 2006 iliyofanyiwa marekebisho, jina hilo linapatikana mara 11 tu. *
Ingawa jina la Mungu limeondolewa karibu kila mahali katika tafsiri hiyo, bado ina jambo fulani lenye kupendeza. Kwenye mojawapo ya kurasa za kwanza-kwanza, kuna maneno yanayosema waziwazi kwamba jina la Mungu ni Yehova. Jambo hilo limewasaidia sana wale wanaotafuta kweli wajifunze kwa kutumia nakala zao wenyewe za Biblia jina la kibinafsi la Baba yetu wa mbinguni.
Hata hivyo, huo si mwisho wa habari. Mwaka
wa 1996, Biblia Tafsiri ya Ulimwengu Mpya ya Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo ilitolewa katika Kiswahili. Hiyo ndiyo iliyokuwa tafsiri ya kwanza ya Kiswahili iliyorudisha jina la Yehova mara 237 kuanzia Mathayo hadi Ufunuo. Baadaye, mwaka wa 2003, Biblia nzima ilitolewa katika Kiswahili, Biblia Takatifu—Tafsiri ya Ulimwengu Mpya. Kufikia leo, jumla ya nakala 900,000 hivi za Biblia hiyo zimechapishwa katika Kiswahili.Jina la Mungu halikubadilishwa tena na majina ya cheo au kufafanuliwa katika maelezo ya kurasa za kwanza-kwanza. Sasa watu wenye mioyo minyoofu wanapofungua Tafsiri ya Ulimwengu Mpya ya Kiswahili, wanavutwa karibu na Yehova kila wakati wanaposoma mojawapo ya sehemu zaidi ya 7,000 zinazotaja jina lake.
Pia, tafsiri hii imetumia Kiswahili cha kisasa ambacho kinaeleweka kwa urahisi na watu wengi wanaoishi Afrika Mashariki. Vilevile, makosa kadhaa ya Kimaandiko yaliyo katika tafsiri nyingine nyingi yameondolewa. Mambo hayo yanamfanya msomaji awe na uhakika kwamba anasoma “maneno sahihi ya kweli” kama yalivyoandikwa chini ya mwongozo wa Muumba wetu, Yehova Mungu.—Mhubiri 12:10.
Watu wengi wameeleza jinsi wanavyothamini Tafsiri ya Ulimwengu Mpya katika Kiswahili. Vicent, mhubiri wa wakati wote wa Mashahidi wa Yehova aliye na umri wa miaka 21, alisema, “Nimejawa na furaha kwa sababu ya Kiswahili rahisi ambacho Tafsiri ya Ulimwengu Mpya imetumia na pia jina la Mungu limerudishwa katika sehemu ambazo tafsiri nyingine zimeliondoa.” Frieda, mama aliye na watoto watatu, anahisi kwamba tafsiri hii imefanya iwe rahisi kuwaeleza watu kweli za Biblia.
Kutoka kwa chanzo kidogo, kazi ya kutafsiri Neno la Mungu katika Kiswahili imeendelea kwa zaidi ya miaka 150. Yesu alisema kwamba alikuwa ‘amelifunua jina la Baba yake.’ (Yohana 17:6) Sasa, kwa kutumia Tafsiri ya Ulimwengu Mpya, Mashahidi wa Yehova zaidi ya 76,000 wa Afrika mashariki na kati wanaozungumza Kiswahili wanafurahia kushiriki katika kufanya jina la Yehova lijulikane na watu wote.
^ fu. 3 Kiswahili kinazungumzwa kwa lahaja mbalimbali katika nchi hizo.
^ fu. 18 Linapatikana katika Mwanzo 22:14; Kutoka 6:2-8 (mara mbili); 17:15 (linatajwa kuwa Yahweh); Waamuzi 6:24; Zaburi 68:20; 83:18; Isaya 12:2; 26:4; 49:14; na Yeremia 16:21.