Matumizi ya Vipodozi Katika Nyakati za Biblia
Baada ya kuoga, mwanamke anajipaka mafuta yenye marashi kwenye ngozi yake laini. Kisha, anafungua sanduku maridadi lililo na chupa nyingi ndogo-ndogo na mitungi iliyotengenezwa kwa kioo, pembe za ndovu, makombe, au mawe. Ndani ya vyombo hivyo mna mchanganyiko wa mafuta na marashi ambayo yameongezewa harufu ya zeri, iliki, mdalasini, ubani, asali, manemane, na vitu kama hivyo.
Mwanamke huyo anachukua kutoka ndani ya sanduku hilo vijiko, vyombo, na mabakuli yaliyo na maumbo yenye kupendeza. Anavitumia kuchanganya vipodozi ambavyo amechagua kutumia siku hiyo. Huku akijitazama kwenye kioo kilichotengenezwa kwa shaba, anaendelea kujirembesha kwa makini.
INAONEKANA kwamba tangu zamani za kale, wanawake wamependa sana kujirembesha. Michoro ya zamani iliyo kwenye makaburi, kuta, na nakshi inaonyesha kwamba watu wengi walitumia vipodozi katika maeneo ya kale ya Mesopotamia na Misri. Mapambo ya macho yenye umbo la lozi yaliyo kwenye michoro ya wanawake Wamisri yalipendwa sana.
Namna gani kuhusu Waisraeli? Je, wanawake wa taifa la kale la Israeli walitumia vipodozi? Ikiwa ndivyo, ni vipodozi gani? Bila shaka, hakuna michoro kwenye makaburi au kuta za wakati wa Israeli la kale ambayo tunaweza kurejelea. Lakini masimulizi fulani ya Biblia pamoja na vitu vilivyochimbuliwa katika maeneo ya nyakati za Biblia vinaweza kutusaidia kuelewa matumizi ya vipodozi nyakati hizo.
Vifaa Vilivyotumiwa
Vifaa vingi vinavyohusiana na matumizi ya vipodozi na marashi vimefukuliwa kotekote katika eneo la Israeli. Vitu hivyo vinatia ndani mabakuli ya mawe yaliyotumiwa kusaga na kuchanganya vipodozi, chupa za marashi zenye umbo la karoti, mitungi ya mafuta ya alabasta, na vioo vidogo vilivyotengenezwa kwa shaba inayong’aa. Kijiko fulani kilichotengenezwa kwa pembe ya ndovu kina mchongo wa majani ya mtende upande mmoja wa kushikia na upande wa pili una mchongo wa kichwa cha mwanamke kilichozungukwa na njiwa.
Inaonekana makombe yaliyorembeshwa yalikuwa vifaa vya kubebea vipodozi vilivyotumiwa sana na matajiri. Vijiko vidogo vya kujipodoa vilivyotengenezwa kwa pembe za ndovu au mbao, vingine vikiwa na mchongo wa wasichana wanaoogelea na mapambo mengine maridadi, vimepatikana pia kwenye maeneo ya Wamisri na Wakanaani. Yote hayo yanathibitisha kwamba wanawake wa nyakati hizo walitumia sana vipodozi.
Vipodozi vya Macho
Katika Biblia, mmoja wa binti za Ayubu anaitwa “Kereni-hapuku.” Katika Kiebrania, huenda jina hilo linamaanisha “Pembe ya Rangi Nyeusi (ya Macho),” yaani, kikasha au kisanduku kilichotumiwa kubebea vipodozi labda wanja, au vipodozi vya macho. (Ayubu 42:14) Inawezekana kwamba jina hilo linaonyesha urembo wake kwa ujumla, lakini pia linaweza kuonyesha kwamba matumizi ya vipodozi yalijulikana wakati huo.
Biblia inapotaja mapambo ya macho nyakati zote inahusianisha zoea hilo na wanawake 2 Wafalme 9:30; Yeremia 4:30; Ezekieli 23:40) Kutokana na idadi kubwa ya vyombo vilivyotengenezwa kwa kioo au mawe na vifaa vidogo vya kupaka wanja wa macho ambavyo vimefukuliwa, inaelekea kwamba wanawake wengi katika taifa lililoasi la Israeli, hasa katika makao ya mfalme na matajiri, walikuwa wameiga zoea hilo la kujirembesha kupita kiasi wakitumia mapambo ya macho na vipodozi vingine.
waovu kama vile Malkia Yezebeli mwenye hila na jiji la Yerusalemu lililokosa uaminifu, ambalo manabii Yeremia na Ezekieli walililinganisha na kahaba. (Mafuta Yenye Marashi kwa Ajili ya Ibada na Matumizi Mengine
Marashi yaliyotengenezwa kwa mafuta ya zeituni yalianza kutumiwa zamani katika Israeli la kale. Kitabu cha Biblia cha Kutoka kina mwongozo wa kutengeneza mafuta matakatifu yaliyotiwa marashi ambayo yalitumiwa na makuhani katika utumishi wao hekaluni. Yalitengenezwa kwa mchanganyiko wa mdalasini, manemane, na mimea mingine yenye harufu nzuri. (Kutoka 30:22-25) Huko Yerusalemu, wachimbuaji wa vitu vya kale wamepata jengo ambalo wanaamini lilitumiwa kutengeneza marashi na uvumba uliotumiwa hekaluni katika karne ya kwanza W.K. Biblia inataja mara nyingi mafuta yenye marashi, ambayo yalitumiwa katika ibada na matumizi mengine.—2 Mambo ya Nyakati 16:14; Luka 7:37-46; 23:56.
Kulikuwa na tatizo la maji katika maeneo hayo, na hivyo mafuta yenye marashi yalisaidia kudumisha usafi. Mafuta hayakutumiwa tu kulinda ngozi wakati wa majira ya joto kali bali pia yalitumiwa kama vipodozi. (Ruthu 3:3; 2 Samweli 12:20) Kabla mwanamwali Myahudi aliyeitwa Esta kuletwa mbele ya Mfalme Ahasuero, alipakwa vipodozi mwilini kwa miezi 12, kwanza alipakwa mafuta ya manemane kwa miezi sita, kisha akapakwa mafuta ya zeri kwa miezi mingine sita.—Esta 2:12.
Marashi au mafuta yaliyotiwa marashi yalikuwa bidhaa muhimu yenye thamani kama fedha na dhahabu. Wakati malkia wa Sheba alipofunga safari ya kumtembelea Mfalme Sulemani, zawadi zenye thamani alizoleta zilitia ndani dhahabu, mawe ya thamani, na mafuta ya zeri. (1 Wafalme 10:2, 10) Mfalme Hezekia alipowaonyesha wajumbe kutoka Babiloni hazina za nyumba yake, “mafuta ya zeri na mafuta mazuri” yalikuwa yamewekwa kando ya fedha, dhahabu, na ghala lake lote la silaha.—Isaya 39:1, 2.
Ni kiwango kidogo tu cha marashi au mafuta ambacho kilitolewa kwenye maua, matunda, utomvu, au maganda ya miti. Biblia inataja baadhi ya mimea hiyo yenye harufu nzuri, kama vile udi, zeri, ulimbo wa bedola, kane, kida, mdalasini, ubani, manemane, zafarani, na nardo. Baadhi ya mimea hiyo ilipatikana katika eneo hilo na ilikua katika Bonde la Yordani. Mingine ililetwa kutoka India, Arabia Kusini, na maeneo mengine kupitia biashara ya ubani iliyojulikana sana.
Fumbo la Mafuta ya Zeri
Biblia inataja mafuta ya zeri kwenye masimulizi kuhusu Malkia Esta, malkia wa Sheba, na Mfalme Hezekia, kama ilivyotajwa mapema. Mwaka wa 1988 gudulia dogo la mafuta lilichimbuliwa katika pango lililo karibu na Qumran, kwenye ufuo wa magharibi wa Bahari ya Chumvi. Mafuta hayo yalitokeza maswali mengi. Je, hayo ndiyo mafuta ya mwisho ya zeri yaliyojulikana sana? Watafiti hawana jibu kamili. Mpaka leo hii, bado wakulima wanajaribu kutokeza miti ya zeri iliyojulikana.
Inaelekea uthibitisho unaonyesha kwamba mafuta ya zeri yanayotajwa katika Biblia yalitengenezewa katika maeneo yaliyo karibu na En-Gedi. Wachimbuaji wamefukua tanuru, magudulia, vyuma mbalimbali, na vifaa vilivyotengenezwa kwa mifupa, vya karne ya sita K.W.K., ambavyo vinafanana na vile vilivyotumiwa katika maeneo mengine ambako marashi yalitengenezwa. Wasomi wengi wanaamini kwamba asili ya mimea ya zeri ni Arabia au Afrika. Marashi yalitolewa kwenye utomvu wa mimea hiyo. Mafuta ya zeri yalikuwa na thamani sana hivi kwamba njia za kukuza mmea huo na kutengeneza mafuta zilikuwa siri.
Hata zeri ilitumiwa ili kutafuta suluhisho katika mapambano ya kisiasa. Kwa mfano, kulingana na mwanahistoria Yosefo, Mark Antony alinunua shamba zima la mimea hiyo yenye thamani na akalitoa kama zawadi kwa Malkia Cleopatra wa Misri. Mwanahistoria Mroma, Plini, alitaja kwamba wakati wa Vita vya Wayahudi katika karne ya kwanza W.K., wapiganaji Wayahudi walijaribu kuharibu mimea yote ya zeri ili kuzuia Waroma waliokuwa wakivamia wasiichukue.
Kutokana na masimulizi ya Biblia na uvumbuzi wa watafiti, tunaweza kutambua jinsi ambavyo watu walioishi katika nyakati za Biblia walitumia vipodozi. Badala ya kukataza matumizi ya vipodozi na mapambo mengine, Biblia inakazia kwamba vitu hivyo vinapaswa kutumiwa kwa kiasi na kwa utimamu wa akili. (1 Timotheo 2:9) Mtume Petro alitaja kuwa jambo lenye “thamani kubwa machoni pa Mungu” ni “roho ya utulivu na ya upole.” Kwa sababu ya mitindo inayozidi kubadilika ya mavazi na mapambo, kwa kweli huo ni ushauri mzuri kwa wanawake Wakristo, iwe ni vijana au wazee.—1 Petro 3:3, 4.