Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Halfpoint Images/Moment via Getty Images

ENDELEA KUKESHA!

Maofisa wa Afya wa Serikali Waonya Kuhusu Athari za Mitandao ya Kijamii kwa Vijana—Biblia Inasema Nini?

Maofisa wa Afya wa Serikali Waonya Kuhusu Athari za Mitandao ya Kijamii kwa Vijana—Biblia Inasema Nini?

 Mei 23, 2023, ofisa mmoja wa serikali nchini Marekani aliwaonya raia kuhusu mitandao ya kijamii inayowaathiri vijana wengi.

  •   “Ingawa mitandao ya kijamii inaweza kuwasaidia watoto na matineja kwa njia fulani, kuna mambo mengi yanayoonyesha kwamba inaweza pia kuhatarisha afya yao ya akili na ya kimwili.”​—Social Media and Youth Mental Health: The U.S. Surgeon General’s Advisory, 2023.

 Shirika hilo limeonyesha utafiti waliofanya unaoeleza kwa nini tunapaswa kuwa macho.

  •   Matineja wenye umri kati ya miaka 12 na 15 “waliokuwa wakitumia zaidi ya saa 3 kila siku kwenye mitandao ya kijamii walikabili hatari kubwa zaidi ya kutokuwa na afya nzuri ya akili kutia ndani dalili za ugonjwa wa kushuka moyo na wasiwasi mwingi.”

  •   Kati ya vijana wenye umri wa miaka 14 wanaotumia mitandao ya kijamii sana wengi “walikosa usingizi, walionewa na watu mtandaoni, walihangaishwa kuhusu sura zao, walijidharau, na walikuwa na dalili nyingi za kushuka moyo, na idadi kubwa ya vijana hao ilikuwa wasichana.”

 Wazazi wanawezaje kuwalinda watoto wao na hatari hizo? Biblia ina ushauri unaofaa.

Mambo ambayo wazazi wanaweza kufanya

 Fahamu mambo yanayohusika. Ukiwa mzazi, chunguza mtoto wako anaweza kupatwa na athari gani kisha uamue ikiwa mtoto wako anaweza kutumia mitandao ya kijamii au la.

 Ikiwa utamruhusu mtoto wako atumie mitandao ya kijamii, uwe makini kutambua hatari zinazoweza kutokea na ufuatilie mambo ambayo anafanya mtandaoni. Jinsi gani?

 Mlinde mtoto wako kutokana na habari zenye kudhuru. Mzoeze mtoto wako kutambua na kuepuka habari zenye kudhuru.

 Weka mipaka. Kwa mfano, weka sheria zinazoonyesha mtoto wako anaruhusiwa kutumia mitandao ya kijamii kwa muda gani na wakati gani.

  •   Kanuni ya Biblia: “Endeleeni kuangalia sana jinsi mnavyotembea . . . kama watu wenye hekima, mkiutumia vizuri kabisa wakati wenu.”​—Waefeso 5:15, 16.

  •   Tumia vibonzo kwenye ubao Tumia Mitandao ya Kijamii kwa Hekima ili kumsaidia mtoto wako kuelewa umuhimu wa mipaka.