Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Urusi: Kuhubiri habari njema jijini Moscow

MATUKIO MUHIMU YA MWAKA ULIOPITA

Ripoti ya Mambo ya Kisheria

Ripoti ya Mambo ya Kisheria

Kusajiliwa Kisheria

Si lazima kwa Mashahidi wa Yehova kusajiliwa ili waendelee na kazi yao. Hata hivyo, kusajiliwa hutuwezesha kununua au kumiliki majengo kwa ajili ya mikutano na kusafirisha machapisho.

  • Mwaka wa 2004, mahakama nchini Urusi zililifuta shirika la kisheria linalotumiwa na Mashahidi wa Yehova jijini Moscow. Hivyo, ndugu zetu jijini humo walikabili upinzani mkali. Polisi waliwanyanyasa, watu waliwashambulia wakiwa utumishi, mikataba ya majengo waliyotumia kwa ajili ya ibada ikasitishwa, na ndugu wakaachwa bila mahali pa ibada. Mwaka wa 2010, hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu (ECHR) ilionyesha kwamba Urusi ilikiuka haki ya Mashahidi wa Yehova jijini Moscow na ikaamuru shirika lao lisajiliwe. Tunafurahi kuwajulisha kwamba Mei 27, 2015, Idara ya Wizara ya Sheria ya Shirikisho la Urusi ya Moscow ililisajili upya Shirika la Kidini la Mashahidi wa Yehova jijini Moscow.

Kodi

Kwa kawaida, Mashirika ya kisheria ya Mashahidi wa Yehova ulimwenguni pote hayatozwi kodi kama ilivyo kwa mashirika mengine ya kidini na misaada. Hata hivyo, nyakati nyingine, serikali hukataa kutupatia vibali vya msamaha wa kodi.

  • Nchini Sweden, serikali inadai kuwa Betheli inaendesha biashara, na kwamba Wanabetheli wameajiriwa. Serikali imeitoza kodi kubwa Betheli na Wanabetheli mmoja-mmoja. Mashahidi nchini humo, wamefungua kesi ya madai katika mahakama na wamepeleka maombi sita katika Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu.

Kutounga Mkono Upande Wowote na Kukataa Kujiunga na Jeshi kwa Sababu ya Dhamiri

Watu wa Yehova wanatii amri ya Biblia ya ‘kufua panga zao ziwe majembe’ na ‘kutojifunza vita tena.’ (Isa. 2:4) Wanadumisha msimamo wao ingawa baadhi ya serikali haziruhusu utumishi mbadala wa kijamii.

  • Nchini Korea Kusini, sheria ya hivi karibuni haitambui haki ya mtu kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri. Kwa kipindi cha miaka 60 iliyopita, wanaume Mashahidi zaidi ya 18,000 wamefungwa kwa sababu ya kukataa kujiunga na jeshi. Karibu kila Shahidi nchini humo ameshuhudia rafiki au ndugu yake akifungwa. Mwaka wa 2004 na 2011, Mahakama ya Kikatiba ya Korea Kusini iliamua kwamba katiba inaruhusu kufungwa. Hata hivyo, Julai 2015, Mahakama ilisikiliza tena ushahidi na kuchunguza upya kesi hiyo. Mashahidi wa Yehova ulimwenguni pote wanasali kuhusu suala hilo la muda mrefu, ili ndugu zetu vijana nchini Korea Kusini wasifungwe kwa sababu ya imani yao.

  • Nchini Eritrea, Mashahidi wa Yehova watatu wamekuwa gerezani kwa miaka 22 kwa kuwa walikataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri. Paulos Eyassu, Negede Teklemariam, na Isaac Mogos hawajawahi kusikilizwa wala kupewa fursa kujitetea mahakamani. Wao pamoja na ndugu na dada wengine 50 wanaendelea kudumisha utimilifu wao licha ya mateso makali na hali mbaya gerezani. Tuna uhakika kwamba Yehova anaona “kuugua” kwa wale waliofungwa kwa sababu ya imani naye atawasaidia.—Zab. 79:11.

  • Mwezi wa Agosti 2014, nchini Ukrainia, Vitaliy Shalaiko aliitwa ili ajiandikishe katika utumishi wa jeshi. Kwa sababu ya dhamiri, alikataa kufanya hivyo, na akaomba afanye utumishi wa kijamii wa badala. Mwendesha mashtaka alimshtaki Ndugu Shalaiko kwa kosa la kukataa kujiunga na jeshi, hata hivyo, mahakama haikumpata na hatia yoyote. Mahakama ya rufaa iliamua kuwa usalama wa Taifa si sababu ya kukiuka haki na ilisema kwamba, “dhamiri ya mtu haipaswi kupuuzwa kwa sababu ya masilahi ya usalama wa taifa.” Mwendesha mashtaka huyo alikata tena rufaa. Juni 23, 2015, Mahakama Kuu ya Pekee ya Ukrainia ya Makosa ya Jinai ilikubaliana na uamuzi wa mahakama za chini. Hivyo ilithibitisha kwamba haki ya kufanya utumishi wa kijamii wa badala unaruhusiwa hata inapohusu matukio ya dharura ya kitaifa.

Ukraine: Vitaliy Shalaiko akifurahia kuhubiri

Ndugu Shalaiko anasema hivi kuhusu matokeo ya kesi hiyo: “Niliimarishwa na maneno ya Yeremia 1:19. Nilikuwa nimejitayarisha kwa lolote, na muhimu zaidi ni kuwa mwaminifu kwa Yehova. Nina uhakika kwamba hataniacha kamwe naye atanipa nguvu za kuendelea kuwa imara. Mambo yalikuwa tofauti na nilivyotarajia. Mahakama zote tatu hazikunipata na hatia. Wakati wa kesi, ndugu walikuwa pamoja nami. Hawakuniacha kamwe.”

Kutounga Mkono Upande Wowote na Sherehe za Kizalendo

Sherehe za kizalendo ni changamoto ambayo Wakristo hukabili inapohusu kutounga mkono upande wowote. Vijana hasa hushinikizwa kuvunja utimilifu wao kwa Yehova walimu wanapowalazimisha waimbe wimbo wa taifa au kusalimu bendera.

  • Katika wilaya ya Karongi nchini Rwanda, walimu waliwashtaki wanafunzi kadhaa Mashahidi kwamba hawaheshimu taifa kwa kuwa hawakuimba wimbo wa taifa. Wanafunzi hao wakafukuzwa shule na kufungwa. Novemba 28, 2014, Mahakama ya Wilaya ya Karongi iliwaondolea mashtaka wanafunzi hao na ikaamua kwamba kutoimba wimbo wa taifa si tendo la dharau. Katika nchi nyingine za Afrika, kama vile Guinea ya Ikweta, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kameruni, na Malawi, Mashahidi vijana wamekabili suala hilo, na katika visa fulani wamefukuzwa shule. Ndugu zetu katika nchi hizo wanajitahidi kuwaeleza viongozi wa shule na serikali kuhusu msimamo wa Mashahidi wa Yehova.

  • Nchini Honduras, Mirna Paz na Bessy Serrano wakiwa na vyeti vyao vya diploma

    Mwezi wa Desemba 2013, shule ya serikali huko Lepaera, Honduras, ilikataa kuwapatia vyeti vya diploma wanafunzi wawili Mashahidi kwa kuwa hawakuimba wimbo wa taifa na kuapa kiapo cha ushikamanifu mbele ya bendera. Ili kutatua suala hilo, wanasheria wawili ambao ni Mashahidi wa Yehova, walikutana na mwakilishi wa Wizara ya Elimu na kumweleza mifano ya nchi zinazounga mkono msimamo wa wanafunzi Mashahidi. Ofisa huyo aliwasikiliza na akakubali wanafunzi na wazazi waandike maelezo yao kwa mwanasheria wa Elimu nchini Honduras. Baada ya kuchunguza madai yao, Julai 29, 2014, alitoa mwongozo unaosema kwamba “[kila mtu] katika jamii ana haki ya kupata elimu bila ubaguzi wa aina yoyote ile” na akaamuru wanafunzi hao Mashahidi wapewe diploma.

Ubaguzi wa Serikali

Tukiwa Mashahidi wa Yehova kutoka katika mataifa yote, tunatii amri ya Yesu ya kuwahubiria majirani zetu habari njema za Ufalme, tunakusanyika pamoja na waabudu wenzetu, na kujifunza Neno la Mungu kwa ukawaida. Pia, tunakazia sheria ya Yehova katika mioyo ya watoto kwa kuwafundisha watii amri ya Biblia ya ‘kujiepusha . . . na damu.’ (Mdo. 15:20; Kum. 6:5-7) Nyakati nyingine, tunapotii amri hizo tunakabili upinzani kutoka kwa serikali zisizoelewa vizuri msimamo wetu.

  • Katika jimbo la Florida, nchini Marekani, hakimu alimpa mama ambaye si Shahidi haki ya kuwafundisha watoto wake watatu mambo ya dini. Baba ambaye ni Shahidi hakuruhusiwa kuwafundisha imani yoyote inayotofautiana na imani ya Katoliki. Baba huyo aliamua kukata rufaa na Agosti 18, 2014, mahakama ya rufaa ilitengua masharti hayo. Kwa kutumia mifano ya kesi zilizotangulia, mahakama hiyo ya rufaa iliandika hivi: “Masharti ya haki ya mzazi asiye mlezi kuwafundisha watoto imani yake ya kidini yamekiukwa bila ushahidi wowote wa kwamba shughuli za dini zitawadhuru watoto.”

    Uamuzi huo umewapa watoto hao haki ya kufaidika na mafundisho na mwongozo wa Yehova Mungu. Wototo hao wanafanya maendeleo ya kiroho kwa kuwa wanashirikiana na kutaniko la kwao. Baba huyo alisema hivi: “Kwa hakika kuvumilia hali hii kumenisaidia kuwa imara. Nimekabili majaribu, lakini Yehova amenisaidia kuwa imara! Ninajua kwamba minyanyaso ni sehemu ya maisha tunapoamua kumtumikia Yehova.”

  • Namibia: Efigenia Semente akiwa na watoto wake watatu

    Dada Efigenia Semente, mama mwenye watoto watatu aishiye nchini Namibia, alikabili jaribu kubwa la utimilifu wake. Alipokuwa akijifungua mtoto wa tatu, alipata tatizo na baadhi ya wahudumu wa hospitali na ndugu zake ambao si Mashahidi waliomba kibali cha mahakama ili kulazimisha atiwe damu mishipani. Dada Semente alikataa kutiwa damu na akachukua hatua za kisheria kutetea haki yake ya kuchagua matibabu. Juni 24, 2015, Mahakama Kuu ya Namibia ilimuunga mkono Dada Semente, na kueleza kwamba “hakuna mtu, iwe ni mzazi au mtu mwingine yeyote ambaye ana haki ya kuchagua jambo la kufanya kwenye mwili wa mtu mwingine.” Dada Semente alisema hivi baadaye: “Mkono wa Yehova ulikuwa wazi kuliko wakati mwingine wowote. Ninafurahi kuwa sehemu ya tengenezo hili. Kwa kweli, Yehova anatujali sana.”

  • Mashahidi nchini Uswisi wamekuwa wakifurahia mahubiri ya hadharani katika miji mikubwa. Hata hivyo, jiji la Geneva lilipiga marufuku kutumia “meza au vigari ili kueneza habari za dini moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja kwenye maeneo ya umma.” Mashahidi walifungua kesi mahakamani ili kupinga marufuku hiyo kwa sababu “inapinga uhuru wa dini na uhuru wa kujieleza.” Mahakama ilikubali ombi lao, na Mashahidi wameshirikiana na wenye mamlaka kutafuta maeneo na kupanga wakati unaofaa kwa ajili mahubiri ya hadharani ya meza na vigari.

  • Maofisa wa serikali nchini Azerbaijan wamezidi kuzuia utendaji wa Mashahidi wa Yehova. Wizara ya Usalama wa Taifa imewahoji mara kadhaa Mashahidi mmoja-mmoja. Pia, polisi huchunguza nyumba za Mashahidi wakitafuta machapisho ambayo yamezuiwa kuingizwa nchini. Februari 2015, jumuiya ya kimataifa ilishangazwa sana na uamuzi wa Wizara ya Usalama wa Taifa kuwafunga Mashahidi wawili, Irina Zakharchenko na Valida Jabrayilova, kwa sababu tu waliwafundisha jirani zao Biblia. Ingawa tunahuzunishwa sana na mateso hayo, tunashangilia kuona wahubiri nchini Azerbaijan wakiendelea kudumisha bidii ya kuwahubiria jirani zao “habari njema ya Ufalme.”—Mt. 24:14.

  • Mashahidi wa Yehova nchini Urusi wanakabili upinzani mkali kutoka serikalini kwa sababu ya kazi yao. Kufikia sasa, Shirikisho la Urusi limetangaza machapisho 80 ya Mashahidi wa Yehova kuwa yana “msimamo mkali.” Hilo linamaanisha kwamba kugawa au kuwa na vitabu, kama vile Kitabu Changu cha Hadithi za Biblia, ni kuvunja sheria. Pia, Desemba 2014, Mahakama Kuu ya Shirikisho la Urusi ilitangaza kwamba tovuti yetu ya jw.org ni yenye “msimamo mkali.” Mawakala wa huduma za intaneti nchini Urusi wameifungia tovuti ya jw.org, na kuitangaza ni kuvunja sheria. Tangu Machi 2015, maofisa wa forodha wamezuia machapisho yote ya Mashahidi kuingia nchini, kutia ndani Biblia na machapisho mengine ambayo mahakama za Urusi ziliyachunguza na kuyatangaza kwamba hayana msimamo mkali.

Katika jiji la Taganrog, wenye mamlaka wamewashtaki wahubiri 16 kwa “kosa” la kupanga na kuhudhuria mikutano ya dini. Katika jiji la Samara, wenye mamlaka waliomba kibali cha mahakama kufuta shirika letu la kisheria kwa madai ya kuwa lina “msimamo mkali.” Licha ya changamoto hizo, ndugu na dada zetu nchini Urusi wameazimia kuendelea kumtolea “Mungu vitu vya Mungu.”—Mt. 22:21.