SOMO LA 51
Shujaa na Msichana Mdogo
Kulikuwa na msichana mdogo Mwisraeli katika nchi ya Siria aliyekuwa amepelekwa mbali na kwao. Jeshi la Siria lilikuwa limemchukua kutoka kwa familia yao, na sasa alikuwa mtumishi wa mke wa mkuu wa jeshi aliyeitwa Naamani. Msichana huyo mdogo alimwabudu Yehova hata ingawa watu alioishi nao hawakufanya hivyo.
Naamani alikuwa na ugonjwa mbaya wa ngozi, na kila wakati alikuwa na maumivu. Msichana huyo alitaka sana kumsaidia. Alimwambia mke wa Naamani hivi: ‘Ninajua mtu ambaye anaweza kumsaidia mume wako. Kule Israeli, kuna nabii wa Yehova anayeitwa Elisha. Anaweza kumponya mume wako.’
Mke wa Naamani akamwambia mume wake maneno ya yule msichana mdogo. Naamani alikuwa tayari kufanya lolote, kwa hiyo akaenda kwenye nyumba ya Elisha nchini Israeli. Naamani alitazamia kwamba Elisha angempokea kama mtu wa pekee.
Lakini badala ya kuzungumza naye moja kwa moja, Elisha akamtuma mtumishi wake ampe Naamani ujumbe huu: ‘Nenda ukaoge mara saba katika Mto Yordani. Kisha utaponywa.’Naamani akaudhika sana. Akasema hivi: ‘Nilifikiri nabii huyu angeniponya kwa kumwomba Mungu wake na kutikisa mkono wake huku na huku juu yangu. Badala yake, ananiambia niende kwenye mto huu wa Israeli. Kule Siria tuna mito bora kuliko huu. Kwa nini nisiende kuoga huko?’ Naamani akakasirika sana, na kuondoka katika nyumba ya Elisha.
Watumishi wa Naamani wakamsaidia kufikiri vizuri. Wakamwambia hivi: ‘Je, si uko tayari kufanya jambo lolote ili uponywe? Jambo ambalo nabii huyu anakuambia ufanye ni dogo sana. Kwa nini usilifanye tu?’ Naamani akawasikiliza. Akaenda kwenye Mto Yordani na kujitumbukiza mara saba. Baada ya kujitumbukiza mara ya saba, Naamani akatoka majini akiwa ameponywa kabisa. Alifurahi sana, akarudi kwa Elisha na kumshukuru. Naamani akasema: ‘Sasa ninajua kwamba Yehova ndiye Mungu wa kweli.’ Unafikiri yule msichana Mwisraeli alihisije Naamani aliporudi akiwa ameponywa?
“Kutoka katika kinywa cha watoto wadogo na wachanga, umetoa sifa.”—Mathayo 21:16