SEHEMU YA 10
Sulemani Atawala kwa Hekima
Yehova ampa Mfalme Sulemani moyo wa hekima; wakati wa utawala wa Sulemani, Waisraeli waishi kwa amani na ufanisi usio na kifani
MAISHA yangekuwaje ikiwa taifa zima na mtawala wake wangemtambua Yehova kuwa Mwenye Enzi Kuu na kutii sheria Zake? Ndivyo ilivyokuwa wakati wa utawala wa miaka 40 ya Mfalme Sulemani.
Kabla ya Daudi kufa, alimteua Sulemani atawale baada yake. Katika ndoto, Mungu alimwambia Sulemani aombe anachotaka. Sulemani aliomba hekima na ujuzi wa kuwahukumu watu kwa haki na busara. Yehova alipendezwa na jibu lake naye akampa Sulemani moyo wenye hekima na uelewaji. Pia, Yehova alimwahidi utajiri, utukufu, na maisha marefu maadamu angeendelea kuwa mtiifu.
Sulemani alipata umaarufu kwa sababu ya hekima yake katika kuhukumu. Katika kisa kimoja, wanawake wawili walikuwa wakibishania mtoto mvulana, kila mmoja akidai kuwa mama yake. Sulemani aliagiza mtoto huyo akatwe vipande viwili na kila mwanamke apewe nusu ya mtoto huyo. Mwanamke wa kwanza akakubali, lakini mara moja mama halisi ya mtoto huyo akaanza kusihi mtoto huyo akabidhiwe mwanamke yule mwingine. Sulemani akaona wazi kwamba mwanamke mwenye huruma ndiye mama ya mtoto huyo, akamkabidhi. Muda si muda taifa zima la Israeli likasikia kuhusu uamuzi huo wa kihukumu, na watu wakatambua kwamba Sulemani ana hekima kutoka kwa Mungu.
Mojawapo ya mafanikio makuu ya Sulemani ni ujenzi wa hekalu la Yehova—jengo lenye fahari jijini Yerusalemu ambalo lingekuwa kituo cha ibada katika taifa la Israeli. Wakati wa kuzinduliwa kwa hekalu hilo, Sulemani alisali hivi: “Tazama! Mbingu, ndiyo, mbingu za mbingu, haziwezi kukutosha; jinsi gani basi, nyumba hii ambayo nimeijenga!”—1 Wafalme 8:27.
Sifa za Sulemani zilifika katika nchi za mbali, hata kufikia Sheba, Uarabuni. Malkia wa Sheba alisafiri kwenda kuuona utukufu na utajiri wa Sulemani, na kupima hekima yake. Malkia huyo alivutiwa sana na hekima ya Sulemani na ufanisi wa taifa la Israeli hivi kwamba akamsifu Yehova kwa kumtawaza mfalme mwenye hekima hivyo. Kwa kweli, Yehova aliubariki utawala wa Sulemani, nao ukawa utawala wenye ufanisi na amani zaidi katika historia yote ya taifa la kale la Israeli.
Kwa kusikitisha, Sulemani hakuendelea kutenda kulingana na hekima ya Yehova. Alipuuza amri ya Mungu, akaoa mamia ya wanawake, kutia ndani wengi waliokuwa wakiabudu miungu ya kigeni. Pole kwa pole wake zake wakaugeuza moyo wake kutoka kwa Yehova, akaanza kuabudu sanamu. Yehova akamwambia Sulemani kwamba atanyang’anywa sehemu ya ufalme. Sehemu ndogo tu ndiyo ingebaki katika familia yake, kwa sababu ya ahadi ambayo Mungu alimtolea Daudi, baba ya Sulemani. Licha ya kutotii kwa Sulemani, Yehova aliendelea kuwa mshikamanifu kwa agano la Ufalme alilofanya na Daudi.
—Inatoka kwenye 1 Wafalme, sura ya 1 hadi 11; 2 Nyakati, sura ya 1 hadi 9; Kumbukumbu la Torati 17:17.