Tovuti ya JW.ORG Sasa Inapatikana Katika Lugha Zaidi ya 300!
Unapobofya sehemu ya lugha katika ukurasa huu wa tovuti ya jw.org, utaona orodha ya zaidi ya lugha 300, jambo ambalo huwezi kulipata katika tovuti nyinginezo!
Hebu linganisha idadi hiyo ya lugha na za tovuti nyinginezo zinazojulikana sana. Kufikia Julai 2013, habari katika tovuti ya Shirika la Umoja wa Mataifa zilikuwa zikisomwa katika lugha sita tu. Tovuti inayoitwa Europa, ambayo ndiyo tovuti rasmi ya Muungano wa Ulaya, inaweza kusomwa katika lugha 24. Unaweza kutafuta habari katika lugha 71 kwenye mtandao wa kutafuta habari wa Google na lugha 287 katika mtandao wa Wikipedia.
Muda mwingi sana hutumika kutafsiri habari za tovuti katika lugha zaidi ya 300! Sehemu kubwa ya kazi hiyo hufanywa na mamia ya Mashahidi wa Yehova kote ulimwenguni ambao wameazimia kumsifu Yehova. Wanafanya kazi katika vikundi vilivyopangwa vizuri, wakitumia ustadi wao kutafsiri maandishi ya Kiingereza katika lugha mbalimbali.
Tovuti ya jw.org ina kurasa nyingi sana za habari ambazo zimetafsiriwa katika lugha zaidi ya 300. Isitoshe, tayari kurasa zaidi ya 200,000 zimeshatafsiriwa!
Mbali na kuwa habari katika tovuti hiyo zinaweza kusomwa katika lugha nyingi, watu wengi sana huitembelea tovuti hiyo. Ukweli wa jambo hilo unaonekana kupitia uchunguzi uliofanywa na kampuni inayoitwa Alexa, ambayo huchunguza utendaji wa Intaneti kote duniani. Katika kitengo kimoja cha uchunguzi wake kinachoitwa “Dini na Hali ya Kiroho” kuna orodha ya tovuti 87,000, zinazotia ndani tovuti za dini kuu mbalimbali duniani, tovuti za wachapishaji wa vitabu vya dini na mashirika mengine ya kidini. Kufikia Julai 2013, Tovuti ya jw.org ilikuwa ya pili katika orodha hiyo! Ya kwanza katika orodha ilikuwa tovuti moja ya mambo ya biashara inayomruhusu mtumiaji apate Biblia zilizotafsiriwa katika lugha mbalimbali.
Kufikia Oktoba 2013, takriban watu 890,000 walikuwa wakitembelea tovuti ya jw.org kila siku. Tutaendelea kuweka habari zinazowasaidia watu maishani mwao, bila kutoza kitu chochote.